Bunge jana lilipitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2013/14 ambapo kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama
vingi nchini mwaka 1993, Bajeti hiyo ilipitishwa pasipo kwanza kusoma na
kujadili Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Sio nia yetu kujadili mazingira yaliyosababisha hali hiyo kwa sababu tayari vyombo vya habari vimetoa taarifa za kutosha kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, yafaa tuseme hapa angalao kwa muhtasari tu kwamba wabunge wa Chadema ambacho ndicho kinachoongoza kambi ya upinzani Bungeni walikuwa jijini Arusha kuhudhuria mazishi ya watu waliokufa kutokana na bomu lililorushwa wakati wa kufunga kampeni za udiwani za chama hicho.
Sisi tunadhani kutosomwa kwa Bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kisingizio kwamba wabunge wa Chadema hawakuwapo Bungeni ilikuwa ni kasoro kubwa ambayo ilionyesha udhaifu katika uendeshaji wa Bunge la Bajeti. Kanuni za Bunge zinaelekeza wazi kwamba maoni ya kambi hiyo lazima yasomwe kabla bajeti ya kila wizara ya Serikali haijajadiliwa.
Hivyo, Bajeti ya Serikali isingejadiliwa kabla kambi hiyo haijawasilisha maoni yake. Tunadhani busara ingetumika kwa upande wa uongozi wa Bunge ili kuepusha hali hiyo ya aibu kutokana na ukweli kwamba walioathirika na kutosomwa kwa Bajeti hiyo sio wabunge wa Chadema au wa vyama vingine kikiwamo CCM, bali wananchi wote kwa jumla ambao hawakuwa na namna nyingine ya kujua nini kilikuwamo katika Bajeti mbadala ya kambi hiyo.
Tukizingatia kasoro hiyo na nyingine nyingi zilizojitokeza tangu Bunge hilo la Bajeti lilipoanza Mkutano wa 11 mjini Dodoma, tunalazimika kusema kwamba Bunge hilo la Bajeti halikuwa na tija kwa Watanzania. Mbali na wabunge wengi kuendeleza tabia za utoro na kuchapa usingizi, mijadala mingi muhimu kuhusu bajeti za wizara ilitawaliwa na jazba za kisiasa badala ya kujikita katika uzito wa hoja.
Kilichoangaliwa zaidi ni mtoa hoja anatoka chama gani pasipo kutilia maanani umuhimu wa hoja.
Wabunge kadhaa, wakiwamo James Mbatia, John Mnyika, Zitto Kabwe na Tundu Lissu walitoa hoja mbalimbali kuhusu masuala muhimu, lakini hoja hizo ziliwekwa kando kwa sababu dhaifu. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge, tulishuhudia baadhi ya wabunge kwa nyakati tofauti wakiporomosha matusi ya nguoni ambayo hayatamkiki, huku kiti cha Spika kikikaa kimya pasipo kuchukua hatua stahiki.
Pamoja na Spika kuunda Kamati ya Bajeti chini ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ili kuishauri Serikali kabla haijawasilisha Bajeti yake Bungeni, Kamati hiyo haikupewa ushirikiano. Matokeo yake ni Bajeti isiyokuwa na mwelekeo wala ubunifu, yenye vipaumbele vingi, vyanzo vipya vya mapato vichache na ushuru na kodi zikiongezwa kwa bidhaa kama petroli na dizeli zinazowagusa wananchi maskini moja kwa moja.
Ndio maana mijadala mizito haikuelekezwa katika masuala nyeti ya kitaifa kama Deni la Taifa linaloendelea kupaa, kilimo duni, ajira kwa vijana, kushuka kwa elimu, mfumuko wa bei, mchango wa madini kwenye Bajeti na kadhalika. Serikali ilipongezwa eti kwa kuwa sikivu kwa kufuta ushuru na kodi kwenye bodaboda na bajaji. Bahati mbaya hawakujua kwamba waliosamehewa kodi na ushuru sio vijana wanaoendesha vyombo hivyo, bali wamiliki wake ambao ni matajiri.
No comments:
Post a Comment