WASANII wa filamu mkoani hapa, wametakiwa kufanya kazi zao kwa
ushirikiano na kuaminiana ili zipate kujulikana kitaifa na kimataifa,
hivyo kujiongezea kipato.
Hayo yamesemwa jana na Mwenyekiti wa Muda wa Shirikisho la Filamu
Mkoa wa Iringa,
Daudi Masasi, kwenye kikao cha kuandaa rasimu ya katiba
ya shirikisho hilo ambapo wasanii wa filamu mkoani hapa walikutana
kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa.
Masasi aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa gazeti la Tabasamu na mtunzi
mahiri wa hadithi, alisema Mkoa wa Iringa una wasanii wengi wenye
vipaji ila kutokana na kutokuwa na umoja na kutojiamini, wameshindwa
kujulikana kitaifa hadi wakimbilie jijini Dar es Salaam.
“Kutokana na kukosa ushirikiano, kujiamini na uaminifu
unaosababishwa na ujuaji wa wasanii wa hapa, ndiyo maana tunashindwa
kufanikiwa na kujulikana licha ya wengi kutoa filamu na kushindwa
kufanya vizuri katika soko,” alisema Masasi.
Aliongeza kuwa lengo la kuanzisha Shirikisho la Wacheza Filamu Mkoa
wa Iringa ni kuleta umoja ili kazi zao zijulikane na kupendwa na
watazamaji na kujiongezea kipato.
Aidha, alisema lengo la shirikisho ni kuwatetea wasanii haki zao na
kupata maslahi wakati wa uchezaji wa filamu kutokana na wengi wao
kutolipwa malipo mara baada ya kucheza filamu husika.
Naye Katibu wa Muda wa Shirikisho hilo, Shabani Mwinyikayoka alisema
umoja ni kitu muhimu katika kukuza tasnia hiyo mkoani hapa, hivyo ni
muhimu wasanii wajikite kwenye ubora wa kazi.
Aliongeza kuwa wasanii wa Mkoa wa Iringa wameshindwa kupiga hatua
kutokana na ubinafsi, hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto
zinazowakabili.
Alitaja changamoto nyingine ni kukosekana kwa elimu miongoni mwao,
ikiwemo ile ya darasani, hivyo kushindwa kupata mafanikio katika kazi
hiyo.
“Nimeanza kazi ya sanaa tangu mdogo, hivyo najua ni kiasi gani
wasanii wasivyokuwa na upeo wa sanaa hii, na kama huna la kusema acha
kusema na ukisema utasema lisilo la maana. Wasanii twendeni shule kuweza
kuwa na upeo wa sanaa hii,” alisema Mwinyikayoka.
Aliwaomba wasanii zaidi ya 80 waliojitokeza katika mkutano wao
kuishi maisha ya nidhamu, heshima kama wanavyoigiza kutokana na jamii
kuiamini sana kazi ya sanaa.
Aidha, alisema shirikisho litakuwa na mikutano ya mara kwa mara na
kuanzisha bonanza la kila wiki na kufanyika kila Jumamosi katika Uwanja
wa Samora lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kujenga upendo
miongoni mwa wasanii.
Mlezi wa shirikisho hilo, Fedrick Mwakalebela aliahidi kutoa vifaa
vya michezo kwa shirikisho hilo ikiwemo mipira ya soka, mipira wa
mikono, jezi na msaada wa fedha katika usajili wa shirikisho hilo.
Alisema sanaa ya filamu mkoani hapa iko chini sana, hivyo ni jukumu
la wadau wote kuwasaidia wasanii mkoani hapa na kuzalisha ajira kwa njia
ya filamu.
“Nitajitolea vifaa vyote vinavyohitajika, na nitakuwa mlezi wao
katika kuwatafutia masoko ndani na nje ya Tanzania. Kwa kuanza nitatoa
vifaa vya michezo,” alisema Mwakalebela.
No comments:
Post a Comment