LONDON, ENGLAND
WAKATI nyota wa Brazil, Neymar, akisubiri
kutambulishwa rasmi kwenye kikosi cha Barcelona keshokutwa Jumatatu,
habari mpya ni kuwa nyota huyo ameshukiwa na neema baada ya kampuni
inayomiliki matangazo ya David Beckham kuingia naye mkataba wa haki za
picha.
Simon Oliveira ambaye ni mmoja wa viongozi wa
kampuni ya Doyen Group, alisema Neymar amesaini mkataba utakaodumu mpaka
mwaka 2017.
Oliveira alisema kampuni hiyo itakuwa na kazi ya kusaka wadhamini kwa ajili matangazo ya picha ya Neymar nje ya Brazil.
Neymar ambaye amesaini mkataba wa kujiunga na Barcelona ni mchezaji wa tano kwa kupata fedha nyingi miongoni mwa wanasoka ambapo anapata kiasi cha Euro 20 milioni kwa mwaka.
“Kazi yetu ya kwanza itakuwa ni kutengeneza jina la Neymar huko Asia, tunaamini tutapata mafanikio,” alisema Oliveira.
Neymar tayari ana mikataba na kampuni kadhaa za Brazil ikiwa ni pamoja na kampuni ya Nike Inc.
Imefahamika kuwa kampuni zimemiminika kutaka kufanya naye kazi baada ya kubainika kuwa nyota huyo ana marafiki zaidi ya milioni moja kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram na kitendo cha kuhamia Barcelona pia kimempa nafasi ya kusakwa na kampuni zaidi.
“Nimefurahi kufanya kazi na Doyen,” alisema Neymar
ambaye tayari ana mikataba na kampuni kumi ikiwa ni pamoja na Nike,
Volkswagen AG (VOW) na Unilever NV (UNA).
Kiwango cha mchezaji huyo kimeifanya Santos
iingize pesa nyingi kutokana na matangazo na hata wanachama wameongezeka
kutoka 17,000 mwaka 2009 mpaka 65,000 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment