HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam imeingia
katika kashfa nzito baada ya kuvunja nyumba ya mwanamke mmoja Ashura
Swed mkazi wa Upanga kwa maelezo kuwa ipo barabarani.
Katika hali ya kushangaza, manispaa hiyo imemruhusu kujenga eneo hilo
hilo mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Bahadur Dewji mwenye asili
ya Asia.
Akizungumza na Tanzania Daima, mjukuu wa Ashura, Shamsa Salim ameiomba
serikali kuingilia kati sakata hilo ili kuzuia kile alichodai kuwa
uonevu wanaofanyiwa na watu wenye uwezo wa pesa.
Akisimulia huku akibubujikwa na machozi, Shamsa alisema Alhamisi ya
wiki iliyopita walishangaa kuona nyumba yao namba 897 iliyoko Mtaa wa
Mfaume, Upanga ikivunjwa huku wao wakiwa hawana taaarifa yoyote juu ya
ubomoaji huo kwa madai kuwa ipo barabarani.
“Ilikuwa Alhamisi, wiki jana, majira ya saa tano asubuhi tulishtuka na
kushangaa kuona kundi la watu waliojitambulisha kuwa wafanyakazi wa
Manispaa ya Ilala wakivunja nyumba yetu. Tulipowaomba watupatie amri ya
mahakama inayowaruhusu kuvunja nyumba yetu hawakutuonyesha badala yake
waliendelea kuvunja tu.
“Kama wanadai kuwa nyumba yetu ipo barabarani, mbona jengo la SIDO
halijabomolewa? Kama sio uonevu huu, ni nini jamani?” alisema kwa
uchungu Shamsa.
Alisema kuwa bibi yake ambaye ni ajuza mjane, ni mmiliki halali wa
nyumba hiyo hata kabla ya mumewe kufariki dunia Juni, 2009 na kuongeza
kuwa kuvunjwa kwa madai kuwa wamevamia barabara na eneo lao kupewa mtu
mwingine ni uonevu wa dhahiri kwa Mtanzania mnyonge.
Alisema wamefuatilia kwa siku kadhaa tangu wiki iliyopita walipoona
ujenzi wa haraka unaanza na kubaini kuwa kuwa unafanywa na Dewji ambaye
alidai anawanyima amani kwani amefikia hata kupiga risasi ili kuwatisha
wasidai haki yao.
“Tulipoona tunanyang’anywa haki yetu tulienda kuchukua RB, tunayo na
sasa tumefungua kesi, na kama huyo Dewji hilo ni eneo lake kwanini
anafanya mambo ya ajabu ya kutunyima amani? Nina imani haki ya mtu
haipotei, kwa kuwa sisi ni wamiliki halali wa eneo hili, na watu
wasitumie fedha zao kutunyanyasa sisi wanyonge jamani,” alibainisha
Shamsa.
Alisema kuwa walipoona hali si shwari usiku wa kuamkia Jumatatu, wiki
hii walimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi
ili awape msaada baada ya Dewji kufyatua risasi nne kuelekea katika
nyumba yao.
Shamsa alisema kuwa Kamanda Minangi alifika kwa wakati katika eneo
hilo akiwa na askari wake, lakini walishangaa kuona wakishindwa
kumkamata mtuhumiwa wao na badala yake askari mmoja alianza kuwasihi
walitupe ganda la risasi walilookota kwa maelezo kuwa wanaweza kugeuziwa
kibao wakapata matatizo makubwa.
Amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka kuingilia kati ili haki ipatikane.
Tanzania Daima lilimtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala
Mwendahasara Maganga ili kutolea ufafanuzi tuhuma hizo ambapo alisema
kuwa hakuwa na taarifa yoyote kuhusu suala hilo na kumtaka mwandishi
ampe muda ili alifuatilie kwa wasaidizi wake.
“Kwa kweli sina taarifa kabisa na suala unalonieleza, nipe muda
niwasiliane na wasaidizi wangu, lakini ninachoweza kukuhakikishia ni
kwamba sisi ni taasisi inayofanya kazi kwa utaratibu, hatuwezi kumpa mtu
au taasisi yoyote kibali cha kujenga eneo ambalo ni barabara. Huyo
jamaa aliwaonyesha kibali cha kuruhusiwa kujenga? Kama hakuwaonyesha
basi huyo ni mhuni tu, nipe nafasi nilifanyie kazi,” alifafanua Maganga.
Kwa upande wake Dewji anayedai kuwa mfanyakazi wa Aghakan Foundation,
amedai kuwa eneo hilo wamepewa kihalali na manispaa ili wajenge barabara
ya kutokea wanafunzi wa Sekondari ya Aghakan.
Naye Kamanda Minangi alikiri kupigiwa simu na Shamsa kupewa taarifa za
Dewji kurusha risasi, lakini akadai kuwa taarifa hizo zilikuwa za
uongo.
Lakini katika hali ya kushangaza Tanzania Daima lilipofika eneo la
tukio liliona askari polisi wakiwa wamewekwa hapo kupiga doria, hali
iliyothibitisha madai ya Shamsa kuwa kulikuwa na tatizo kubwa eneo hilo
tofauti na maelezo ya kamanda Minangi.
No comments:
Post a Comment