HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam imetangaza
kuyahamisha makaburi 250 yaliyopo ndani ya eneo la mradi wa upanuzi wa
njia za umeme Kata ya Manzese na Kata ya Ubungo, Mtaa wa Ubungo
Kisiwani.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mhandisi
Mussa Natty katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baada ya kupata
taarifa ya kuhamisha makaburi hayo kutoka Shirika la Umeme
Nchini(TANESCO).
Kutokana na hatua hiyo, amewataka watu wote wenye ndugu au jamaa
waliozikwa kwenye eneo hilo kwenda kwenye ofisi za Ofisa Mtendaji wa
Kata ya Manzese na Ubungo kujiandikisha wakiwa na barua ya utambulisho
kutoka ofisi ya mtaa wanakoishi kabla ya Julai 25.
“Mkurugenzi wa TANESCO anawatangazia ndugu na jamaa za marehemu
waliozikwa kwenye makaburi yaliyopo ndani ya eneo la mradi wa upanuzi wa
njia za umeme Kata ya Manzese, Mtaa wa Madizini na Kata ya Ubungo Mtaa
wa Ubungo Kisiwani, kwamba anakusudia kuhamisha makaburi 250 ili
shughuli ya upanuzi wa njia ya umeme iweze kuanza,” alisema Natty katika
taarifa yake.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya mitaa (Mamlaka za Miji) ya mwaka 1982,
kanuni ya mwaka 2008 namba 46(c) Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
itasimamia zoezi hilo kwa kutumia wataalamu wake.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, makaburi hayo yatahamishiwa katika
makaburi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yaliyopo Tegeta Kata ya
Kunduchi baada ya tararibu zote kukamilika.
No comments:
Post a Comment