HATIMAYE serikali imeridhia uamuzi wa wabunge na kukubali kufuta
pendekezo la kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya dizeli na
petroli.
Katika marekebisho hayo, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa
alikuwa amependekeza kuongeza ushuru wa mafuta hayo kwa sh 2 kwenye
dizeli na sh 61 kwenye petroli kwa lita.
Kwa mantiki hiyo, alisema kuwa wataendelea kutoza ushuru wa bidhaa wa
sh 333 kwa lita katika mafuta ya petroli na sh 215 kwa lita kwenye
dizeli.
Wakijadili muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013, wabunge walipinga
mapendekezo hayo na kuishauri serikali itafute mapato kutoka kwenye
vyanzo vipya vilivyoanishwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti badala ya
kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.
Akijibu hoja za wabunge jana kabla ya kupitishwa kwa muswada huo kuwa
sheria itakayoanza kutumika Julai mosi mwaka huu, Waziri Mgimwa alisema
walikubali ushauri huo ili kuleta unafuu kwa wananchi na kuzuia mfumuko
wa bei unaoweza kujitokeza.
Alisema serikali iteendelea kutoza ushuru wa sasa bila kuongeza hata
senti, lakini wameongeza ushuru wa mafuta ya taa kufikia sh 425 kwa lita
badala ya sh 400.30 zinazotozwa sasa hivi.
Alisema kuwa hatua hizo ni pamoja na kudhibiti uchakachuaji wa dizeli
uliokuwa ukifanywa kwa kutumia mafuta ya taa na hivyo kuingiza nchi
katika hatari zaidi.
Pia Waziri Mgimwa alisema kuwa serikali imeongeza ushuru wa mafuta ya
petroli (fuel levy) kutoka sh 200 hadi 263 kwa lita ikiwa ni lengo la
kuongeza mapato ya mfuko wa barabara nchini ili kugharamia barabara
zinazopaswa kujengwa.
“Tumeongeza ushuru wa mafuta ya dizeli (fuel levy) kutoka sh 200 hadi
263 kwa lita. Lengo hili mbali na kuongeza mapato pia nazo zitasaidia
kugharamia ukarabati wa barabara,” alisema.
Waziri pia alifafanua kuwa ushuru wa bidhaa kwenye simu hautatozwa
kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha bali kwenye huduma zingine kama
kupiga, kutuma ujumbe mfupi au picha.
“Baada ya kuchunguza kwa undani na kupokea maoni ya kamati ya bajeti,
tumeona kweli kuna uwezekano wa mtu kutozwa kodi mara mbili pale
anapokuwa ameunganishwa kutoka mtandao mmoja wa simu mwingine. Hilo
tutakaa na wenzetu wa TCRA kuliangalia,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali imeafikiana na kamati ya bajeti kwamba
mapendekezo ya msamaha wa kodi ya zuio kwa ndege za kukodi yasogezwe
mbele hadi mwaka ujao wa fedha ili kutoa muda kwa serikali na
wafanyabiashara wa sekta ya anga kuendelea kujadiliana.
“Serikali pia imeridhia mapendekezo ya kamati ya bajeti ya kukusanya
mapato kutoka uvuvi wa bahari kuu na sasa linafanyiwa kazi ili kiwe moja
ya vyanza vipya vya mapato vitakavyotupa mapato makubwa pamoja na
uwekezaji kwenye migodi mikubwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment