Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afrika
Mashariki, Dk. Abdulla Juma Saadalla wakati akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalumu, Rukia Kassim Ahmed (CUF).
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali wa
kuanzisha kitengo cha wagonjwa wa saratani katika mikoa mingine.
Dk. Saadalla alisema mashine hizo za kutibu kansa kwa mionzi
zinatarajiwa kuwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Agosti mwaka
huu.
Alisema baada ya mashine hizo kuwasili, wagonjwa wenye matatizo ya
saratani kutoka Kanda ya Ziwa wanaohitaji mionzi hawatalazimika kwenda
Dar es Salaam kupata huduma hiyo.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa kupeleka huduma hizo karibu na
wananchi, serikali kwa kushirikiana na hospitali hiyo imeanzisha huduma
za ngazi ya kitaifa katika hospitali hiyo ya Bugando.
“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo na uagizaji wa vifaa na mashine
tiba kwa ajili ya huduma hizo imekamilika, mpaka sasa wagonjwa 4,000
wameshatibiwa,” alisema.
Alisema serikali itaendelea na juhudi za kusogeza huduma za afya za
rufaa karibu na wanapoishi wananchi katika kanda nyingine na ngazi zote
kadiri hali ya uchumi na mapato yatakavyoruhusu.
Alisema kwa sasa huduma kwa wagonjwa wa kansa zinatolewa kila
hospitali za mikoa ingawa kwa viwango tofauti, na kwamba wagonjwa ambao
hawawezi kutibiwa katika hospitali hizo hupewa rufaa katika hospitali za
ngazi za juu ikiwemo Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.
No comments:
Post a Comment