NAAM
kama kawaida tumekutana tena kwenye safu yetu ya Mapenzi na Uhusiano
kama ilivyo ada ili kumbushana mawili matatu yahusuyo mahaba hasa yale
yanayokwaza na kuondoa maana halisi ya mapenzi.
Napenda kutoa pole nyingi kwa familia ya aliyekuwa mchezaji wa zamani
Abdallah Msamba na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Langa Kileo ambao
waliwapoteza ndugu zao hao wiki iliyopita. Inaonekana upepo mbaya
umekuwa ukivuma kwa sasa, lakini wote tuamini hili nalo litapita, la
muhimu kuwaombea marehemu wote wapumzike kwa amani. Baada ya kusema
hayo, tuendelea na mada yetu ya leo, wote tunajua mapenzi yanajumlisha
upendo wa pande mbili kati ya mwanamke na mwanaume wala hakuna
aliyeumbwa kwa ajili ya kupendwa au kupenda vitu hivyo havipo.
Maana halisi ya mapenzi ni kupendana, siyo dhambi kumuonyesha mwenzio
unavyo mpenda au mwenzio kuonyesha anavyokupenda. Hii ndiyo sababu ya
kuwa wawili lazima mjiulize kuna wanaume na wanawake wangapi lakini
amekuchagua wewe! Upendo wa dhati dunia ya leo imekuwa adimu kama maji
jangwani, sasa hivi mapenzi yamekuwa shaghalabaghala yamebakia mapenzi
ya mtu kitu, asiye na kitu hajui mapenzi au kwa wenye umbile na sura
nzuri, wenzangu na mimi tulie tu.
Tumeona wengi wakilia baada kupanda mbegu ya mapenzi pasipo na
mapenzi, lakini walio bahatika kupata wenye mapenzi ya kweli wamesahau
nini maana ya mapenzi na kujikuta wameyageuza badala ya kuwa furaha
yanakuwa mateso kwa wenzao kwa vile wameonyesha kuwa wanapendwa. Siku
zote anayependa ndiye anayeteseka kwa kujitahidi kuonyesha upendo wake
ambao hauthaminiwi.
Mateso huja pale anapoamini kuna kitu anakosea katika penzi lenu bila
kujua aliyempa penzi lake hajui thamani yake. Penzi linakuwa na
masharti kibao kwa kujua huwezi kukataa kwa vile unampenda au linakuwa
la gharama kwa kutaka vitu vya thamani ambavyo wakati mwingine vinakuwa
nje ya uwezo wako. Jua kuwa ni kosa kumfanya mpenzi wako ajute kuwa na
wewe, siku zote penzi tamu ni kwa mpenzi wako kukuona kama tulizo la
moyo wake, kato la uchovu wa kutwa nzima.
Mfanye mpenzi wako akiwa mbali nawe akuwaze au ukikumbuka, atabasamu
na kuwa na hamu ya kukuona. Kila akikukumbuka au akisikia jina lako
likitajwa atamani muda ufike upesi ili awe pamoja nawe. Siyo kila
akisikia jina lako au kila akikukumbuka moyo wake unamlipuka na kujuta
kwa nini alikupenda au amekaa na wewe. Heshimu na kuthamini upendo
unaopewa na mpenzi wako, kama mwenzako kaonyesha anakupenda jua una deni
la kulipa upendo huo.
Usiwe mwizi wa fadhila kupewa pendo kulipa maudhi mpende akupendaye.
Mwisho narudia kwa kusema kumbuka karaha katika mapenzi humtia mtu sugu
katika moyo wake na kufikia kukuchukia na kukuona adui wa moyo wake. Ipo
siku mapenzi hutoweka na kukuona adui yake namba moja kuliko kifo.
Aliyekuwa akikupenda siku akikuchukia huwa hana msamaha atakufukuza
kama mbwa na kushangaa, kisha atajiuliza ni kweli ni yeye ndiye
uliyekuwa ukimpeleka puta kama saa mbovu! Upendwapo, pendeka utakuja
penda pasipo penzi utatamani ardhi ikumeze
No comments:
Post a Comment