RAIS Barack Hussein Obama wa Marekani anaanza ziara ya siku mbili nchini Tanzania leo akitokea Afrika Kusini kwenye mfululizo wa ziara zake barani Afrika akianzia Senegal, Ijumaa Wikienda linakuhabarisha kilichopo nyuma ya ziara hiyo.
Wakati Obama akitua Bongo, mwandishi wetu aliyepo jijini Nairobi, Kenya amesema kuwa baadhi ya Wakenya wamekinunia kitendo cha kiongozi huyo mkubwa duniani kutofika nchini humo ambako ndiko kwenye chimbuko lake.
Baba wa Barack, marehemu Sir Hussein Obama alizaliwa Kenya katika Kijiji cha Nyang’oma, Kogelo, Wilaya ya Siaya. Kabila lake ni Mluo kwa hiyo Obama ni Mluo (Mjaluo).
KWA NINI WANUNE?
Kwa mujibu wa paparazi wetu nchini humo, baadhi ya Wakenya wanahoji iweje Rais Obama atue Tanzania kwa ziara na kuiacha pembeni nchi yake ya Kenya?
“Nimeongea na baadhi ya Wakenya, wanahoji ni kwa nini Obama asifike kwao? Wanasema afadhali angepanga ziara ya nchi zote mbili kuliko kuipitia pembeni Kenya na kutua huko Bongo.
“Lakini wapo Wakenya wenye uelewa ambao wametambua kwamba ziara ya Obama nchini Tanzania ni ya kiserikali, hakuwa na ratiba ya Kenya. Kama atataka kuja Kenya kumsalimia bibi yake atafanya hivyo binafsi siku nyingine,” alisema paparazi wetu akiwakariri watu aliozungumza nao nchini humo.
KWA NINI KAIKWEPA KENYA?
Akizungumza na Amka na BBC kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC Jumamosi iliyopita, profesa mmoja alisema Obama hatafika Kenya kwa sababu viongozi waliopo madarakani kwa sasa, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wana kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita iliyopo jijini The Hague, Uholanzi.
“Si rahisi Obama kwenda Kenya kwa sababu viongozi wake, Uhuru na Ruto wana kesi kwenye Mahakama ya The Hague…,” alisema profesa huyo.
KIKWETE KAANDIKA HISTORIA AFRIKA
Ujio wa Obama Tanzania umeandika historia ya pekee kwa Rais Jakaya Kikwete barani Afrika kwani katika kipindi cha utawala wake, marais wawili wa Marekani walio madarakani wameitembelea nchi anayoiongoza.
Mwaka 2008, Rais wa 34 wa Marekani, George Walker Bush (67) aliitembelea Tanzania na kukutana na Kikwete kama mwenyeji wake.
TANZANIA NDIYO NCHI BORA AFRIKA
Mbali na Kikwete kupokea marais wawili wa Marekani, lakini Tanzania inaonekana ndiyo nchi bora zaidi barani Afrika kwa vile ndiyo pekee iliyotembelewa na marais wengi kutoka Marekani.
Mwaka 1999, William Jefferson ‘Bill’ Clinton (67) akiwa Rais wa 42 wa Marekani alitua nchini kwa ziara ya kiserikali na hivyo kuanzisha mfululizo wa waliomfuatia, Bush na Obama.
Clinton aliwahi kuja tena Bongo baada ya kuachia madaraka, Bush naye anaingia nchini leo akiwa ameongozana na mkewe, Laura ambapo Julai 2 na 3, 2013 anatarajiwa kuhutubia kongamano litakalojadili wajibu wa wake wa marais katika kuinua wanawake duniani. Mke wa Obama, Michelle atahudhuria.
NI OBAMA DAY
Jijini Dar es Salaam, hali si ile iliyozoeleka. Tangu harakati za maandalizi ya ujio wa Obama uanze, jiji limekuwa safi kwa kuwaondoa wafanyabiashara wadogo na wale ombaomba wazoefu.
Maeneo ya katikati ya jiji, baadhi ya wafanyakazi waliozungumza na Wikienda, Jumamosi iliyopita walisema wana uhakika kwa siku ambazo Obama atakuwepo Bongo, kazi zitasimama kutokana na kukosekana kwa usafiri na kuwepo kwa foleni za kusubiri misafara.
“Jumatatu na Jumanne naamini hakutakuwa na kazi, Obama amesababisha mabasi yasije mjini tangu juzi (Alhamisi). Mji ni mweupe. Mi nadhani hii tuiite Obama Day,” alisema Samson Isaya anayefanya kazi katikati ya Jiji la Dar.
KUMBE JIJI LINAWEZA KUFANYA USAFI!
Cha ajabu, ni Manispaa za Jiji la Dar es Salaam, hasa Ilala na Kinondoni zilivyoweza kulisafisha jiji na kuwa safi kiasi cha kuvutia.
Wasomaji wengi wa gazeti hili walisema kumbe Dar kuwa chafu ni uamuzi wa wahusika wenyewe na si wakazi wake kwani wahusika hao wameweza kuingia mitaani na kufanya usafi kwa zana zilezile za siku zote.
“Sasa jiji wanachoshindwa ni nini? Mbona jiji ni jeupe? Nenda Posta, nenda Mwenge, angalia pale Stesheni, kweupe. Siku nyingine wanasema vifaa hakuna, sasa hivi vimetoka wapi? Kama mimi ndiyo JK (Kikwete) nawaambia jiji liwe hivi kila siku,” alisema mama Swebe wa Magomeni, Dar.
Credit:GLP
No comments:
Post a Comment