ARUSHA.
MFANYABIASHARA maarufu wa madini aina ya tanzanite jijini
Arusha, Erasto Msuya, ameuawa kikatili kwa kumiminiwa risasi takriban
kumi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Tukio hilo lililogubikwa na utata wa hali ya juu kutokana na mazingira
yake, lilitokea jana mchana eneo la Mijoholoni, wilayani Hai, wakati
marehemu akiwa njiani kutokea Arusha.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, zilisema kuwa mfanyabiashara huyo
bilionea alikutwa na mauti hayo akiwa na gari lake la kifahari aina ya
Range Rover lenye namba za usajili T 800 CKF.
Hata hivyo, Kamanda Boaz hakuweza kutoa taarifa zaidi juu ya mauaji
hayo kutokana na kile alichodai alikuwa akielekea eneo la tukio na
kuahidi kutoa taarifa mara baada ya kurejea kutoka eneo hilo la tukio.
Taarifa zaidi zilidai kuwa Msuya alipigwa
risasi na watu wawili waliokuwa wamepanda pikipiki na kupita eneo
alilokuwa amesimama nje ya gari lake akizungumza kwa simu.
Baadhi ya marafiki zake jijini Arusha waliokuwa naye muda mfupi kabla
ya tukio hilo walidai kuwa alipigiwa simu akiitwa eneo hilo kwa ajili ya
kumuuzia madini.
Katika hali inayoacha maswali kuhusu tukio hilo, wauaji hao
hawakuchukua kitu chochote kuanzia gari, fedha sh milioni 100 zilizokuwa
ndani, simu za mkononi pamoja na ipad.
Mara baada ya kupigwa risasi.
Chanzo chetu cha habari kilidokeza kuwa tukio hilo huenda limepangwa
ili kuzima vuguvugu la tuhuma za mauaji ya mchimbaji mmoja aliyeuawa
hivi karibuni kwenye machimbo ya Mererani.
Kwa mujibu wa watoa habari walioomba kuhifadhiwa majina yao, sakata la
kesi hiyo limekuwa na utata mkubwa kutokana na Jeshi la Polisi mkoani
Arusha kutaka kumkumbatia mtuhumiwa wa mauaji hayo, kwa kutomfikisha
mahakamani.
Marehemu Msuya anatajwa kama mmoja wa wachimbaji waliokuwa mstari wa
mbele kuwashinikiza polisi kuhakikisha kesi hiyo inafikishwa mahakamani
ili haki itendeke kwa wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Tukio hilo limeanza kuibua hofu miongoni mwa wananchi wa kawaida na
wafanyabiashara juu ya kurejea kwa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha
uliokuwa umepoa kwa muda katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Tanzania Dama jana, wamedai
kuwa tukio hilo bado limegubikwa na utata kutokana na mazingira yake,
kwani gari la marehemu lilikutwa limeegeshwa pembeni mwa barabara kuu ya
Arusha - Moshi kana kwamba kulikuwa na mazungumzo baina ya marehemu na
wauaji.
Credit : 2jiachie


No comments:
Post a Comment