Na IRENE MWAMFUPE NDAUKA
“KAMA kuna watu hawayajui haya nitakayoyaongea basi nawataka
kuanzia sasa wajue kwamba, hapa Dar kuna mambo makubwa sana ambayo ukisimuliwa
unaweza kusema si kweli, lakini wale wanaoyapata wanajua. Ila wewe omba
yasikukute hata siku moja...”
Ndivyo alivyoanza kusimulia Bw. Humuli Samaki (43), mkazi wa
Buguruni (kwa sasa) ambaye alipata mkasa mzito akidai alipanga nyumba moja na
majini Magomeni, Dar es Salaam. Anaendelea…
“Si zamani sana mkasa huu uliponitokea, ilikuwa mwaka 2009 tu. Kwa
hiyo naweza kusema ni juzijuzi. Kwa sasa naishi hapa Buguruni, baada ya
kuhama kutoka Magomeni ambako nilipataka mkasa huo mzito na wa kuogopesha.
Nilipanga nyumba moja na majini.”
Awali nilikuwa nikiishi Mwananyamala Mwinjuma, jirani kabisa na
Makao Makuu ya Bendi ya TOT, hata Kapteni John Komba nilizoeana naye kwa
kuonanaonana pale CCM-Mwinjuma, ingawa jina langu najua hakuwa akilifahamu.
Nyumba niliyokuwa nikiishi Mwananyamala iliingia kwenye mgogoro wa
mirathi, familia ilifika mahakamani. Hukumu ilipotoka ikaamriwa iuzwe kisha
ndugu wagawane fedha.
Kwa maana hiyo, mimi na wapangaji wenzangu watano, tulipewa notisi
ya kuhama baada ya mteja kupatikana. Huyu mteja anaitwa Masawe anafanya kazi
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lakini sijui ofisi za wapi.
Ilibidi mimi niangalie mwelekeo mwingine, niliamua nibadili upepo,
nikatamani kwenda kuishi Magomeni. Kwa wakati huo nilikuwa sina familia. Sina
mke wala mtoto, hata wa kusingiziwa. Kwa hiyo nilikuwa naishi peke yangu. Ni
mwaka jana ndiyo nimeoa mke wangu huyu.
Rafiki yangu mmoja anaitwa Mohammed Kombe alinipa namba ya dalali
kwani yeye anaishi Magomeni hata sasa. Nilimpigia simu dalali wake, anaitwa
Yusuf Mwamba, akaniita Magomeni pale kwenye nyumba wanayosema aliwahi kuishi
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Nilikwenda mpaka pale, nilimkuta amesimama nje ya nyumba hiyo,
tukasalimiana, akaniuliza nataka nyumba yenye sifa gani, nikamweleza.
Akasema nyumba ya aina hiyo ipo moja mitaa ya katikati kama
unatokea pale tulipo kuelekea kwa Sheikh Yahya Hussein (marehemu).
Tulikwenda kuiona hiyo nyumba. Wakati tukiwa tunaifikia,
nilishangaa kuwaona majirani wakitukodolea macho si kawaida, sikushangaa sana
nikijua ni mambo ya mjini kitu kidogo tu watu kibao.
Yule dalali alifungua mlango, tukaingia ndani. Tulipita sebuleni,
tukaenda kwenye vyumba viwili, tukaelekea jikoni, chooni na kumalizia
bafuni. Ni nyumba iliyojitegemea kwa maana kwamba, ilikuwa na ua wake na mtu
akiwa uani hakuna kuona nje. Mlango wa kuingilia ndani ni mmoja tu.
Kulikuwa na vyumba vingine viwili ambavyo toka mwanzo dalali
aliniambia chumba kuna mwanaume anaishi na mkewe. Chumba kimoja wanalala,
kingine wamekifanya sebuleni, lakini hawana watoto kama mimi.
Nilijiridhisha kwamba ni pazuri, dalali akaniuliza kuhusu malipo,
nikamwambia tuongozane nikachukue pesa Magomeni Mapipa kwenye Benki ya
Barclays, akasema wakati mimi nakwenda kutoa hizo pesa, yeye anakwenda Dawasco
Tawi la Magomeni na shida muhimu pale.
Tukiwa tunaelekea Magomeni Mapipa, nilimuuliza wenye vile vyumba
wanafanya kazi wapi? Akajibu wafanyabiashara, lakini hata yeye hajui ni wapi.
Nilimuuliza imekuwaje ana funguo, wale wapangaji wengine wakirudi je, akajibu
wana funguo yao na ile yeye alipewa na mwenye nyumba kwa ajili ya kutafutia
mpangaji mwingine. Nilikubaliana naye.
***
Baada ya nusu saa nilitoka benki nikiwa na hela, nikampigia simu,
akasema na yeye alishatoka Dawasco na wakati huo alikuwa anakunywa soda kwenye
Hoteli ya Shibam, ipo palepale Mapipa. Nilimfuata pale, nikampa fedha, akatoa
mkataba, nikajaza kwani yeye ndiye aliyepewa jukumu lote na mwenye nyumba.
“Kwa hiyo upo huru kwenda kuhamia,” dalali aliniambia huku
akinikabidhi funguo.
“Sawa, nitahamia usiku wa leo.”
Nilirudi nyumbani kwa awali na kupangapanga vitu tayari kwa usiku
kuhamia makazi mapya, Magomeni. Niliwaambia wapangaji wenzangu wote, nao
wakanitakia maisha mema huku wakisema tukumbukane kwani hata wao walikuwa
kwenye mchakato wa kuhama kwenye nyumba ile.
***
Saa mbili usiku nilikuwa juu ya lori tukipeleka mizigo makazi
mapya, lakini moyoni nilikuwa na maswali mengi ambayo mpaka leo hii siyakumbuki
na yalikosa majibu. Pia, nilijikuta nakosa amani ya moyo na sikujua ni kwanini!
Nje, nilikuta taa inawaka, ndani pia taa inawaka, lakini si
sebuleni bali kwenye korido. Hii iliashiria kwamba, wale wapangaji wenzangu
walisharudi kutoka kwenye biashara zao.
Nilishusha vyombo kwa kusaidiwa na wasaidizi wa dereva wa lile
lori, lakini nilishangaa sana kuona kila nikiingia na mizigo, wale wapangaji
wenzangu wanacheka sana chumbani kwao. Maana yangu ni kwamba, kwa kawaida
walitakiwa hata watoke na kunisalimia ili tufahamiane. Tena kwa wengine, mume
angetoka na kunisaidia kubeba hata stuli tu.
Ilifika mahali, wale vijana waliokuwa wakinisaidia waliniuliza:
“Hivi hao majirani zako mbona hawatoki, wanacheka tu chumbani.”
Niliwajibu mimi mwenyewe sijui, lakini sikumaindi sana. Akaja mama
mmoja aliyesema anaishi nyumba ya pili, akasalimia na kuniuliza maswali.
“Hamjambo wanangu?”
Tuliitikia wote, akauliza nani anahamia pale kati ya sisi wote,
tulikuwa watano mbali na dereva.
“Ni mimi.”
“Ooo, mzima baba?”
“Mimi mzima mama.”
“Unaitwa nani?”
“Humuli Samaki.”
“Unahamia peke yako au uko na mke na watoto?”
“Peke yangu mama.”
“Humuli Samaki ni
mwanyeji wa wapi?”
“Usukumani.”
“Haya, naamini uliaga wakati unaondoka nyumbani.”
“Hilo lilikuwa la kwanza mama.”
“Haya, kila la kheri.”
Tuliendelea na kazi ya kuingiza vyombi ndani hadi tukamaliza. Wale
wenye gari wakaondoka, nikabaki mimi peke yangu.
Nilijiwekea malengo kwamba, nihakikishe naweka sawa kila kitu ili
kesho yake nisiwe na kazi hiyo zaidi ya kwenda kazini. Niliifanya kazi kwa muda
wa saa tatu, mpaka kwenye saa saba na nusu usiku nikamaliza.
Nilibadili nguo, nikavaa taulo na kwenda kuoga. Nilikuta bafu
limetoka kutumika kama dakika kumi nyuma, sikushangaa kwani si kuna wapangaji
wengine ambao tulitakuwa kutumia bafu moja.
Usiku kabla ya kuzima taa, nilizima taa, nikapanda nitandani.
Kabla sijapata usingizi, niliwasikia wenzangu wakicheka sana na kuongea huku
wameweka muziki. Lakini ule muziki haukuwa wa kiarabu, kizungu wala kiswahili.
Hata maongezo yao, mimi nilisikia sauti tu lakini kusema walikuwa
wanatumia lugha gani si rahisi. Kuna wakati kama walikuwa wakiongea kihindi,
pia niliwasikia kama wanaongea kiarabu, nikajua ni watu wa namna hiyo.
Lakini sikulala mpaka nikampigia simu dalala kumuuliza kama wale
wapangaji wenzangu ni weupe au waswahili kama mimi, akasema hata yeye hajui
kwani hakuwahi kuwaona hata siku moja.
Basi, nililala. Asubuhi niliamka nikiwa nimechoka sana. Wakati
nakwenda bafuni kuoga niligundua ni mimi peke yangu ndiye niliyekuwa
nimetangulia kuamka, kwani bafuni hakukuwa na maji yaliyomwagika kwa muda huo.
Baada ya kuoga nilirudi chumbani kwangu kujiandaa kwenda kazini.
Wakati najiandaa, nilisikia mlango ukifunguliwa, nikajua ni wenzangu wanakwenda
kuoga au chooni kama ilivyo kawaida kwa wanadamu wakiamka asubuhi.
Niliamua kutumia nafasi hiyo kuwatambua. Nilivizia pale
niliposikia mlio wa maji bafuni na mimi nikatoka kwenda kupiga mswaki kwa mara
ya pili. Sehemu niliyosimama, mtu akitoka bafuni kwenda ndani ilikuwa lazima
nimuone kwani ilikuwa kiasi cha kugeuka tu.
Lakini cha kushangaza, nilikuwa sisikii maji kumwagika, nikageuka
na kuuna mlango wa bafuni upo wazi. Mbali na mlango kuwa wazi, pia chini
nikaona alama za kandambili nne zikiwa zimekanyaga, nikajua wametoka.
“Lakini wamepitaje hapa?” nilijiuliza.
Nilirudi ndani, mlangoni kwao nilikuta kandambili pea mbili zikiwa
bado na majimaji kwa mbali, jambo hili lilinifanya nijiuliuze sana.
Nilijipa ujasiri na kuamua kuchungulia ndani ya chumba hicho kwa
kutumia nafasi ya katikati ya mlango ambapo niliweza kuona hadi kitanda lakini
sikumwona mtu mwingine.
Niliingia kwangu, nikaweka mswaki, nikava vizuri na kuondoka
zangu. Nilitegemea wenzangu nimewaacha ndani, kwani nilipofika mlangoni
nilikuta umefunguliwa na upo wazi. Nilirudi ndani hadi kwenye mlango wao.
“Wa ndugu,” niliita kwa sauti.
“Jamani wa ndugu.”
Ukimya ndiyo ulinifanya nibaini walishaondoka. Kwani kulikuwa
kimya sana na kandambili zilikuwa pembeni ya mlango si pale pa kwanza.
Nilifunga mlango mkubwa nikaondoka, mbele nilimwona yule mama
aliyekuja usiku kuniuliza maswali. Alikuwa amesimama nje ya nyumba yake,
aliponiona akashutuka na kuita majina mawili ya watu. Wakatoka watoto wake
wawili, ni mabinti wenye miaka kama kumi na nane na ishirini na mbili hivi.
“Hujambo kijana?” yule mama alinisalimia kwa furaha.
“Sijambo mama, shikamoo.”
“Marhaba.” Kisha akawaambia kitu wale watoto wake nao wakanikazia
macho.
“Mama umewaona majirani zangu hapa?”
“Majirani zako akina nani?”
“Wapangaji wenzangu.”
“Kijana, kua uyaone ya dunia. We si umeshakua, utayaona ya dunia.”
Kauli hiyo iliniogopesha sana, nikashtuka na kumuuliza mama.
“Mama una maana gani?”
“Sisi hatutaki umbeya kijana.”
“We si umeambiwa utayaona kwa hiyo subiri tu,” alidakia binti yake
mkubwa.
Miguu ilitetemeka, mwili uliisha nguvu, nikajikuta nataka kukaa,
lakini sikuweza. Nilichoamua ni kuondoka huku nampigia simu yule dalali.
“Vipi hujambo bwana?”
“Mimi sijambo.”
“Za makazi mapya.”
“Si nzuri bwana.”
“Kwanini tena?”
“Sielewielewi.”
“Kivipi?”
“Kuna mambo kama si ya kawaida.”
“Yapi hayo?”
“Wale wapangaji wenzangu siwaelewi kabisa.”
“Kivipi?”
“Ah! Watu gani mimi mgeni nimehamia washindwe kutoka kunisalimia
ili angalau tufahamiane?”
Dalali alicheka sana kisha akasema:
“Wale ndivyo walivyo bwana, si unajua tena malezi, mwingine
kalelewa vile, mwingine hivi. Ila ulichokisema ni kweli, haiwezekani nyumba
mnayoishi mpate mgeni halafu msitambuane, sasa mkikutana njiani je?”
“Si ndiyo hapo sasa,” nilisema nikijifanya lawama zangu ni kwa
ajili ya hilo tu, lakini kumbe nilikuwa na zaidi ya hapo.
Kazini siku hiyo nilishinda sina amani, sina raha, mwili ulikuwa
kama umetoka kufanya kazi nzito ambayo sijawahi kuifanya kwa siku nyingi,
wenyeji wa Pwani wanaita mavune.
Kwa upande mwingine nilitamani sana jioni ifike ili nikaone siku
hiyo kitatokea kitu gani kipya kwenye nyumba ile. Jioni ilifika, nikaondoka
kazini, sikutaka kupitia popote, dukuduku langu lilikuwa kwenda nyumbani tu.
Nilichukua kama saa moja kutoka kazini hadi kufika nyumbani. Nje
nilikuta mfuko wa rambo mweusi, ndani yake ulionekana kuwa na kitu kwani
ulikuwa umetuna sana. Niliinama kuipekenyua ili nijue ndani kulikuwa na nini,
nilishangaa kuona ni vipande vya nyama za kuchoma tena vilikuwa na moto.
“Kha! Atakuwa nani
ameweka?”
Usikose sehemu O2 wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment