Habari na Tanzania Daima.
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk. Shukuru
Kawambwa, jana alipata wakati mgumu wa kuondoka baada ya kuzindua
Utekelezaji wa Mikakati ya Matokeo Makubwa Sasa katika Sekta ya Elimu,
baada ya wakazi wa Kibamba, Mloganzila Kazamoyo, kuvamia eneo hilo kwa
lengo la kumuona.
Tanzania Daima ilishuhudia wakazi hao wakiwa wametawanyika katika
viwanja vya ukumbi huo na wengine kukaa mbele ya bango kubwa la uzinduzi
huo, kwa madai kuwa wanataka kulipwa fidia baada ya nyumba zao kuvunjwa
mwaka mmoja uliopita, ili kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Baada ya uzinduzi huo, gari la Naibu Naziri wa Elimu Philip Mulugo,
Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim
Majaliwa, walianza kuondoka eneo hilo na kufuatia gari la Kawambwa bila
wenyewe kuwemo.
Baada ya watu kuanza kutawanyika katika ukumbi huo, wahanga wanawake
ambao nyumba 91 zilibomolewa, walianza kuangua vilio visiokwisha,
wengine wakigalagala chini kwa madai kuwa wako tayari kugongwa na gari
kama haki yao haitapatikana.
“Tumechoka kuzungushwa, tumefuatilia haki zetu Wizara ya Ardhi na
Makazi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, chuo kikuu (Muhas) na ikulu
bila mafanikio kwa maelezo kuwa fidia yetu itatolewa na Wizara ya
Elimu,” alisema Maria Khalfan kiongozi wa wahanga hao.
Alisema tathmini ya nyumba zao ilifanyika Julai 26 mwaka jana na siku hiyo hiyo wakavunjiwa.
“Tunaishi nje, tunalala nje na watoto wetu wameshakuwa machokoraa hawaendi shule,” alisema.
Akijibu malalamiko hayo alipoulizwa na waandishi wa habari akiwa ndani
ya jengo, Kawambwa alisema wizara yake haipaswi kulipa fidia hiyo.
“Elimu siyo Wizara ya Fedha, wala ya Ardhi, tangu lini Wizara ya Elimu ikalipa madeni?” alihoji Kawambwa.
Hadi Tanzania Daima inaondoka eneo hilo iliwaacha wakazi hao wakiwa bado wanaomboleza kwa kushindwa kumuona Kawambwa.
Awali, Dk. Kawambwa alizindua Mpango wa Utekelezaji wa Mikakati ya
Matokeo Makubwa Sasa katika Sekta ya Elimu, ambapo alisema kuwa sekta
hiyo ni miongoni mwa wizara sita zilizochaguliwa na serikali kwa lengo
la kuleta matokeo makubwa sasa.
Alisema kwa miaka kumi, juhudi kubwa imefanyika katika sekta hiyo
hususan kuongeza uandikishaji katika ngazi zote za elimu, lakini imekuwa
ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimeathiri utoaji wa elimu
bora.
No comments:
Post a Comment