Habari Sitta Tumma, Mwanza wa Tanzania Daima.
JIJI la Mwanza juzi liligeuka kuwa uwanja wa kivita, baada ya
kutokea mashambulizi makali ya risasi baina ya askari polisi na kundi la
watu wanaodhaniwa kuwa majambazi yaliyokuwa yakijihami kwa silaha za
kivita.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima Jumatano kutoka eneo la tukio
zinaeleza kwamba mashambulizi hayo yaliyodumu kwa takribani dakika kumi
yalitokana na kundi hilo la majambazi kutaka kuvamia kituo cha mafuta
cha GBP, kilichopo kando kando ya barabara ya Kenyatta, Igogo jijini
Mwanza majira ya saa mbili usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, na Naibu Kamishna Ernest Mangu
alithibitisha kutokea kwa tukio ambalo inaaminika majambazi hao walikuwa
na silaha nzito za kivita. Majambazi watatu waliuawa katika mapambanao
hayo.
Alisema polisi walipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema dhidi ya
majambazi hayo, na walifika eneo la kituo hicho cha mafuta kisha
kuyakuta majambazi hayo yakijiandaa kuvamia.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari, Kamanda Mangu alisema
majambazi hayo yalilazimika kujibu mapigo ya polisi kwa kutumia silaha
nzito za kivita aina ya SMG na kufanikiwa kuwaua watatu na wengine
wakikimbia kusikojulikana.
“Idadi halisi ya majambazi haijafahamika hasa. Maana yalitokea
majibizano makali ya risasi.
Lakini askari walikuwa makini na
wakafanikiwa kuyaua matatu na mengine yakakimbia,” alisema Kamanda
Mangu.
Alisema katika mapambano hayo polisi walifanikiwa kukamata bunduki
moja aina ya
SMG yenye namba za usajili 2916 pamoja na risasi saba, na
kwamba taarifa walizonazo majambazi hayo yanatoka Wilaya ya Ngara mkoani
Kagera.
“Baada ya majibizano makali ya risasi, katika eneo la tukio yaliokotwa
maganda ya risasi 22. Miili ya hawa jamaa imehifadhiwa Hospitali ya
Rufaa ya Bugando,” alisema.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mangu ametoa wito kwa wananchi kuendelea
kutoa taarifa za siri kwa jeshi hilo dhidi ya wahalifu ili wahusika
waweze kudhibitiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika tukio jingine, watu wasiojulikana wameteketeza kwa moto nyumba
tisa za nyasi za familia moja, katika Kijiji cha Nyehunge wilayani
Sengerema mkoani Mwanza.
Kamanda Mangu alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 11, mwaka
huu majira ya saa 10 na 12 jioni, na chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni
imani za kishirikina.
“Kuna kijana Severine Renatus (14), mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Nyehunge alipotea kwa muda wa siku nne.
“Baada ya kupatikana kwa mwanafunzi huyo na kuhojiwa na wazazi wake,
alisema alifichwa kwenye nyumba hizo, ndipo wazazi walipotoa taarifa kwa
sungusungu wa kijiji hicho, ambao waliamua kukusanyika na wanakijiji
wengine kisha kwenda kwenye nyumba hizo, na wenye nyumba hizo waliamua
kukimbia,” alisema Kamanda Mangu.
Hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, lakini polisi wanaendelea na upelelezi.
No comments:
Post a Comment