JESHI la Polisi limemwondoa hospitalini kimyakimya Katibu wa
Taasisi na Jumuiya za Kiislam, Sheikh Ponda Isa Ponda, na kumpeleka
katika gereza la Segerea bila ndugu zake kuwa na taarifa.
Ponda (54) ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mpya ya kufanya
uchochezi katika maeneo mbalimbali nchini alisomewa shtaka hilo juzi
katika wodi ya Kitengo cha Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa
Mishipa ya Fahamu (MOI) alipokuwa akipatiwa matibabu.
Wakili wake, Nassor Jumaa, aliliambia gazeti hili jana saa 7:00 mchana
nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa
amesikitishwa na hatua ya vyombo vya dola kumuondoa mteja wake asubuhi
na kumhamishia gerezani.
Alisema kuwa amesikitishwa na kitendo hicho kwani Hakimu Hellen Riwa,
muda mfupi baada ya wakili mwandamizi wa serikali, Tumaini Kweka,
kumaliza kumsomea shtaka Ponda juzi, alitoa amri ya mteja wake kuendelea
kukaa chini ya ulinzi.
“Wanausalama wamemtoa wodini na kumpeleka katika gereza la Segerea na
sasa atalazimika kurudishwa tena mahakamani siku kesi yake itakapojatwa
Agosti 28 mwaka huu.
“Kwa kweli kitendo hicho kimenisikitisha na kunishtua sana ila
tunatafakari ni hatua gani za kisheria tutazichukua siku za usoni,”
alisema.
Polisi wafafanua
Jeshi la Polisi nchini limetoa taarifa kuwa Sheikh Ponda anajulikana
alikopelekwa na kukanusha uvumi kuwa hajulikani alikopelekwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji mkuu wa jeshi hilo, Advera
Senso, alisema wametimiza maelezo ya hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu.
Katika hatua nyingine, Senso alisema wanamshikilia askari wake
mmoja kwa tuhuma za kufyatua risasi hewani wakati wa purukushani za
kurushiana mawe na wafuasi wa Sheikh Ponda wiki iliyopita mkoani
Morogoro.
“Tayari timu imeanza kazi na inaendelea vizuri kufuatilia na
kuchunguza hali halisi ilivyokuwa kabla na baada ya purukushani hizo
zilizohusisha wafuasi wa Ponda kurusha mawe na polisi kufyatua risasi
hewani,” alisema.
Senso alikanusha kuwa risasi iliyofyatuliwa siyo iliyomlenga Ponda, na
kusisitiza kuwa kanuni na taratibu za jeshi zinaelekeza kwamba
kutafunguliwa jalada la uchunguzi kwa askari yeyote anapofyatua risasi
iwe ni bahati mbaya au katika mazingira yanayolazimu.
Katika hatua nyingine, Senso alisema kuwa Julai 30, mwaka huu, saa
moja jioni maeneo ya Vingunguti majambazi sita yalikurupushwa na polisi
na kutelekeza begi lao ambalo ndani lilikutwa na bomu la kurushwa kwa
mkono lililotengenezwa nchini Urusi.
Alifafanua kuwa katika sakata hilo watuhumiwa wanne wanashikiliwa na polisi.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kukutwa na bunduki yenye namba 11276,
magazine yenye risasi 23 na kwamba jeshi linaendelea kumtafuta raia wa
kigeni anayedhaniwa kuwa ni Mtutsi ambaye anadaiwa kuingiza mabomu hayo
nchini.
Senso alisema wanachunguza bomu hilo kuona kama lina uhusiano wowote na mabomu yaliyolipuka mkoani Arusha.
CREDIT: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment