MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemhukumu
kutumikia kifungo cha miezi sita jela mshitakiwa Lupembe Majebele (25),
mkazi wa Kijiji cha Lutende, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa kosa la
kuendesha pikipiki bila leseni.
Awali akisomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Wilaya ya Igunga, Ajali Milanzi, Mwendesha Mashtaka wa Polisi
Dezidery Kaigwa aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa anakabiliwa na
makosa mawili.
Aliiambia mahakama kuwa kosa la kwanza ni kuendesha chombo cha moto
bila leseni kinyume na sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1963
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inayozuia kufanya makosa kama hayo
na kosa la pili ni kumgonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo
chake.
Mwendesha mashitaka huyo aliendelea kuiambia mahakama kuwa mnamo
Septemba 10 mwaka huu, majira ya saa 4:00 asubuhi katika Tarafa ya
Simbo wilayani hapa, mshitakiwa akiwa anaendesha pikipiki yenye namba
za usajili T 200 BZT aina ya Sanlg aliendesha kwa uzembe na kumgonga
Kulwa Robert mkazi wa Simbo na kusababisha kifo chake.
Baada ya kusomewa mashitaka yote mawili, mshitakiwa alikana shitaka
la kuua na kukiri shitaka la kuendesha chombo cha moto bila leseni.
Baada kukiri kosa hilo moja, mahakama ilimtia hatiani kutumikia
adhabu ya kifungo cha miezi sita jela na kesi ya kuua bado inaendelea.
Itatajwa tena Oktoba 10, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment