Habari na Zawadi Chogogwe wa Tanzania Daima.
MADIWANI wa Halmashauri ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wamelaani 
kitendo cha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) kufika katika vijiji 
vya Bagamoyo  na kuwatumikisha wananchi kazi za  miradi mbalimbali huku 
fedha wakichukua wao.
Madiwani hao waliibua hayo mjini Bagamoyo juzi katika kikao cha baraza
 la madiwani  cha robo ya nne ya mwaka 2012 na 2013 kilichofanyika 
katika ofisi za mkurugenzi wa halmashauri hiyo ambacho kilihudhuriwa na 
wataalamu mbalimbali.
Diwani wa Kilomo, Hassan Usinga, alisema Tasaf wamekuwa  na tabia ya 
kutofika kwa watendaji wa vijiji  pindi wanapofanya kazi zao za miradi  
na  badala yake wanaenda moja kwa moja kwa wanakijiji na kuwatumikisha  
katika miradi ya maendeleo huku wakiwalipa fedha kidogo.
“Kitendo cha kwenda kwa wanakijiji kuwafanyisha kazi na kuwalipa fedha
 kidogo kumechangia miradi mingi kuwa mibovu huku mingine ikiwa imekufa 
kama vile  miradi  ya kuku,” alisema Usinga.
Alisema taarifa za maendeleo ya vijiji zinaonyesha kuwa dawa za mifugo
 na matumizi zimetolewa kwa wanakijiji  na kueleza kuwa taarifa hizo 
zikiwa hazina ukweli.
“Kutowashirikisha watendaji wa vijiji katika mikutano ya maendeleo 
kumepelekea kukosa wanakijiji wengi kushiriki katika mikutano yao,” 
alisema.
Alisema wanaoshiriki wanakuwa wachache hali inayowafanya Tasaf 
kuwavalisha fulana na kofia huku wakiwapiga picha na kuzipeleka kwa 
wafadhili kwa kuonyesha ushahidi kuwa wanakijiji wameshiriki mkutano huo
 wakati sio kweli.
Aliongeza kusema sh milioni 27 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo ya 
barabara za 
 Tukamisasa kwenda Mbuyu, katika kata ya Ubena lakini cha 
kushangaza barabara hiyo haijajengwa kwa kiwango kutokana na wananchi 
kulazimika kuitengeneza kwa majembe baada ya kuona hakuna juhudi zozote 
za mamlaka husika.
“Tunaiomba Tasaf  iache kutuchezea mchezo mchafu sisi watu wa  
Bagamoyo kwa kuwatumia wanavijiji kwa manufaa yao wenyewe,” alisema.
  Wakati huohuo, madiwani hao walilalamika kuwa watumishi wa halmashauri
 hiyo hawana nyumba za kuishi za kiofisi, hali inayowafanya waishi 
katika nyumba za kupanga.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Fukayosi, Ally Issa, alisema
 inatia aibu kuona watumishi  wa Halmashauri ya Bagamoyo wakiishi katika
 nyumba za kupanga badala ya nyumba za kiofisi.
“Halmashauri inakusanya mamilioni ya fedha lakini inashindwa 
kuwajengea watumishi wake nyumba za kuishi. Mkurugenzi acha mambo ya 
siasa tunachotaka ni kuona nyumba za watumishi zinajengwa na 
kukabidhiwa,” alisema Issa.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Samwel Sariaga, alisema katika bajeti 
ya mwaka huu watajenga nyumba nne za watumishi ambazo kila moja 
itagharimu sh milioni 40.
Katika hatua nyingine, madiwani hao wametishia kuiburuza Bima ya Afya 
mahakamani, kwa kitendo cha kuwakata  asilimia 5 kila mwezi  ndani ya 
miaka mitatu bila kuwapatia kadi za matibabu.
Diwani wa Viti Maalum, Hapsa Jumam, alisema wakati wanaingia 
madarakani waliahidiwa watapewa kadi za matibabu, lakini cha kushangaza 
mpaka sasa hawajapewa.
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment