SWALI la nani atatwaa taji la Miss Universe Tanzania 2013,
linatarajiwa kupata jibu leo wakati warembo 15 kutoka mikoa mbalimbali
ya Tanzania watakapochuana kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, mkabala
na IFM jijini Dar es Salaam kuanzia saa moja kamili usiku.
Warembo hao mbali ya kuwania taji la Miss Universe Tanzania, ambalo
kwa sasa linashikiliwa na Winfrida Dominique, pia watawania taji la Miss
Earth Tanzania na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano
ya kimataifa.
Warembo hao kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakitambiana huku kila mmoja
akijigamba kutwaa taji hilo na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya
dunia yaliyopangwa kufanyika jijini Moscow, Russia Novemba 9.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Compass Communications inayoandaa mashindano
hayo, Maria Sarungi, alisema kuwa kila kitu kimekamilika na warembo
wamepania kufanya makubwa jukwaani, ambapo warembo wote wana ari ya juu
na kila mmoja akiwa na shauku ya kutwaa taji hilo.
“Kwa upande wetu, kila kitu kiko tayari, warembo wamejiandaa vilivyo
na tumeandaa shoo bora na fupi, hivyo mashabiki wa masuala ya urembo
wanatakiwa kufika mapema ili kuona nani anatwaa taji na kupata tiketi ya
kuiwakilisha nchi kimataifa,” alisema Maria.Warembo watakaochuana leo
ni Aziza Victoria, Irene Nsiima, Betty Boniface, Kundi Mlingwa, Mariam
Ngwangwa, Naomi Kisaka, Glady Msemo, Salsha Lukiko, Upendo Dickson,
Vestina Mhagama, Angela Lutataza, Consolata Mosha, Clara Noor, Agnes
Thobias, Dinah David na Clara Noor.
No comments:
Post a Comment