SOKO la Kariakoo jijini Dar es Salaam limeelemewa na wateja 
kutokana na idadi kubwa ya watu 62,000 wanaoingia na kutoka kila siku 
kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Meneja Mkuu wa soko hilo, Florence Seiya, alibainisha hayo 
alipozungumza  ofisini kwake jana na kusema kwa siku 
soko hilo linahudumia watu 62,000.
Alisema mbali na kuelemewa  na wateja, soko hilo linahitaji ukarabati utakaogharimu sh bilioni moja.
Alisema soko hilo lililojengwa miaka 39 iliyopita lina wafanyabiashara
 halali 1,558,  mbali na wale wanaouza biashara za mkononi wanaojulikana
 kama ‘wamachinga’.
“Wafanyabiashara waliomo shimoni ni 600, walioko nje soko dogo ni 190,
 walioko ndani soko dogo ni 289, soko kubwa ni 189 waliobaki ni Mtaa wa 
Swahili eneo la soko,” alisema Seiya.
Seiya alisema kadiri siku zinavyokwenda nafasi inazidi kuwa ndogo, 
baada ya Shirika la Masoko Kariakoo kushindwa kujenga soko jingine la 
ghorofa  la kisasa litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 
4,000 kwa wakati mmoja.
Pia alisema kumekuwapo na ufinyu wa barabara za kuingilia sokoni hapo 
kutokana na magari mengi yanayoegeshwa katika soko hilo, mikokoteni, 
pikipiki na wale wafanyabiashara wanaofanya biashara zao kwenye barabara
 za lami.
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment