KINYANG’ANYIRO cha Ligi Kuu ya Vodacom kiliendelea jana kwenye
viwanja mbalimbali nchini, huku ikishuhudiwa Simba ya jijini Dar es
Salaam ikiwafanyia mauaji maafande wa Mgambo JKT ya Tanga kwa kuipa
kichapo cha mabao 6-0.
Wakati Simba ikitakata kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam,
watani zao Yanga jinamizi la sare liliendelea kuwaandama kwenye Uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya, baada ya kutoka sare ya 1-1 na wenyeji,
Tanzania Prisons.
Jijini Dar es Salaam, Simba ilianza pambano kwa kasi na dakika ya
pili tu, Amis Tambwe nusura aipatie bao baada ya shuti lake ndani ya
boksi kupaa sentimita chache, kabla ya kurekebisha makosa dakika ya
tano na kufunga bao maridadi kwa kichwa akiunganisha krosi ya Issa
Rashid ‘Baba Ubaya’.
Dakika ya 34, Simba ilipata bao la pili likifungwa na chipukizi
Haruna Chanongo baada ya kuwalamba chenga mabeki na kipa Kulwa Manzi
kutokana na shambulizi la pamoja kati yake na Tambwe.
Bao hilo, lilikuja dakika tatu tu tangu Betram Mwombeki aliposhindwa
kuitendea haki krosi safi ya Chanongo wakati kipa akiwa amekwishapotea
langoni.
Dakika ya 24, Tambwe alipachika bao la tatu akitumia
vema udhaifu wa Manzi kudaka mpira kisha kumponyoka, kabla ya dakika ya
44, kukandamiza la nne, likiwa la tatu kwake katika mechi hiyo.
Hadi dakika 45 zinakamilika, Simba ilitoka uwanjani ikiongoza 4-0
huku ikiwa imetawala kipindi cha kwanza kwa asilimia kubwa.
Kutokana na mabao hayo ya kipindi cha kwanza, Kocha Mohamed Kampira
wa Mgambo, alilazimika kumtoa kipa Manzi na kumuingiza Tony Kavishe.
Licha ya Mgambo kutawala dakika za mwanzo kipindi cha pili na
kushindwa kuzitumia nafasi za kufunga dakika ya 49 na 58 kupitia kwa
Salim Amlima na Bashiru Chanache, ilijikuta ikipachikwa bao la tano
dakika ya 65 baada ya shuti kali la Chanongo kumbabatiza beki Bakari
Mtama na kumpoteza kipa wake.
Dakika ya 76, Tambwe alihitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la
sita kwa penalti, baada ya Peter Mwalianzi kuunawa mpira katika eneo la
hatari.
Hadi mwamuzi Jacob Adongo wa Mara aliyekuwa akisaidiwa na Ferdnand
Chacha, Grace Wamara kutoka Kagera, akiashiria dakika 90 kukamilika,
Simba 6, Mgambo 0.
Simba: Abel Dhaira, Miraji Adam/William Lucian, Issa Rashid ‘Baba
Ubaya’, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Henry
Joseph/Ramdhani Chombo ‘Redondo’,
Betram Mwombeki/Twaha Ibrahim, Amis
Tambwe, Haruna Chanongo.
Mgambo JKT: Kulwa Manzi/Kavishe, Francis Anyosisye, Salum Mlima,
Bakari Mtama, Novat Lufunga/Bashiru Chanache, Salum Kipaga, Nassoro
Gumbo, Peter Mwalianzi, Mohamed Neto, Fully Maganga, Salum Gilla.
Kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, wenyeji Azam FC walilazimishwa sare
ya bao 1-1 na vibonde wanaoburuza mkia, Ashanti United.
Jijini Mbeya, mabingwa watetezi Yanga licha ya kutangulia kujipatia
bao dakika ya 43 likifungwa na Jerry Tegete kwa kifua akiunganisha
krosi ya Simon Msuva ilijikuta ikimaliza mchezo kwa sare ya 1-1.
Prisons ilisawazisha dakika ya 72, kwa bao la Peter Michael
akiitendea haki kona ya mchezaji aliyetokea Yanga msimu uliopita, Omega
Seme. Hii ni sare ya pili mfululizo kwa Yanga. Jumamosi iliyopita
ililazimisha sare ya 1-1 kwa Mbeya City kwenye uwanja huo wa Sokoine.
Prisons: Beno David, Salumu Kimenya, Mika Shaban, Juma Elfadhil,
Nurdin Issa, Lugano Mwangama, Jimy Shoji, Fredy Chudu, Ibrahim Issake,
Six Ally, Jeremia Juma, Subu Ibrahimu, Beniphese Hau, Julius Uwage,
Peter Michael, John Esen, Omega Seme, Hamis Rajab.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Lihende, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Simon Msuva,
Salum Telela, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Haruna Niyonzima.
Kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, mkoani Pwani, waliokuwa vinara wa
Ligi, JKT Ruvu walitulizwa na ndugu zao Ruvu Shooting, baada ya
kukubali kulala kwa bao 1-0, mfungaji akiwa Stephano Mwasika.
Jijini Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wenyeji Coastal Union
walitoka sare ya bao 1-1 na Rhino ya Tabora, wakati huko Manungu,
Turiani Morogoro, Mtibwa ililazimishwa sare ya bila kufungana na Mbeya
City.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar walikwenda sare ya 1-1 na JKT Oljoro ya Arusha.
Kwa matokeo ya mechi hizo za mzunguko wa nne, Simba imefanikiwa
kukamata usukani wa ligi, ikifikisha pointi 10 na kuwashusha Ruvu JKT
wenye pointi 9.
No comments:
Post a Comment