WAKATI zikiwa zimebaki siku tatu Redd’s Miss Tanzania
ajulikane, viingilio kwa ajili ya shindano hilo linalosubiriwa kwa hamu
vimetangazwa.
Kiingilio cha juu katika shindano hilo linalotarajiwa kufanyika
Jumamosi, ukumbi wa Mlimani City, Mwenge jijini Dar es Salaam ni sh
100,000 viti maalumu, huku vya kawaida vikiwa sh 50,000.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja
wa kinywaji cha Redd’s Original, Victoria Kimaro, ambao ndio wadhamini
wakuu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, wanaamini viingilio hivyo ni vya
kawaida kutokana na ubora wa shindano lenyewe.
Victoria alisema, burudani katika shindano hilo inatarajiwa kutolewa
na msanii mahiri kutoka Uganda, Mike Ross atakayeshirikiana na Judith
Wambura ‘Lady Jaydee’ pamoja na kundi la Mama Afrika katika kukonga
nyoyo za mashabiki watakaojitokeza ukumbini hapo.
“Tunaamini kabisa wasanii hawa watakonga nyoyo za mashabiki wa tasnia
ya urembo hapa nchini, hivyo napenda kutoa wito kwa mashabiki
kujinunulia tiketi mapema ili kuepuka usumbufu,” alisema Victoria.
Naye Lady Jaydee alisema, kwa kushirikiana na bendi yake ya Machozi,
wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa burudani ya nguvu kwa mashabiki
wote watakaohudhuria.
“Nawaomba mashabiki wangu na wale urembo, kujitokeza kwa wingi ili
kufurahia burudani nzuri toka kwangu na bendi yangu ya Machozi, pia
wasanii wenzangu waalikwa naamini watafanya vizuri siku hiyo,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashimu
Lundenga ambao ni waratibu wa Redd’s Miss Tanzania alisema, tiketi za
shindano hilo tayari zimeishaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali jijini
Dar es Salaam.
Alitaja maeneo ambayo yameteuliwa kuuza tiketi za Redd’s Miss
Tanzania kwa mwaka huu ni duka la Shear Illusion lililopo Mlimani City,
City Sports Lounge na Steers zilizopo Mtaa wa Samora, Faberk Fashion,
Rose Garden Pub na ofisi za Redd’s Miss Tanzania ambazo zote zipo eneo
la Mikocheni.
Lundenga alifafanua kuwa, ili kuwapa fursa watu wengi zaidi tiketi
itakayonunuliwa katika vituo vilivyopangwa kabla ya shindano itakuwa ni
Sh 80,000 na kutakuwa na ofa kadhaa.
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred, aliyefanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s
Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL).
No comments:
Post a Comment