UFISADI uliokithiri katika fedha za misaada zinazotolewa na
serikali kusaidia wajasirimali umekuwa kikwazo kwa Watanzania
kujiendesha.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa Chuo cha
Ufundi Mtakatifu Gaspar kilichopo Kunduchi, Achileus Mutalemwa katika
mahafali ya chuo hicho.
Alisema fedha za misaada zimekuwa haziwafikii walengwa, hivyo
kuishauri serikali kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha inapotoa
fedha zinawafika walengwa.
“Tunakumbuka kuna mabilioni yalitolewa kwa wajasiriamali, lakini ni
wachache waliopata, lakini fedha nyingi zilichukuliwa na mafisadi,”
alisema.
Alisema chuo hicho kinazalisha bidhaa zenye ubora na zinazofaa
kununuliwa na serikali kutokana na uimara na kutumia mbao za hapa
nchini.
Mkuu huyo wa chuo alisema ni muhimu serikali kuweka mkazo kwa viwanda
vya ndani, hasa wajasiriamali wadogo ambao wamekuwa wakizalisha kwa
kutumia nguvu nyingi, lakini mauzo yake yanakuwa hafifu.
“Hapa kwetu tunafundisha useremala, mapishi na hata udereva, na
vijana wamekuwa wakifanya vyema katika uzalishaji wa bidhaa,
kinachotukwamisha ni kitendo cha kuingizwa kwa bidhaa za nje ambazo
hazina ubora, lakini zinauzwa kwa bei ya juu,” alisema.
CHANZO TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment