WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki,
amemkabidhi bendera ya Taifa Miss Universe Tanzania, Betty Boniface,
tayari kuondoka nchini kesho kwenda Moscow Urusi katika mashindano ya
kimataifa yaliyopangwa kufanyika Novemba 9.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Kagasheki alisema kuwa Betty ni
balozi wa Tanzania katika mashindano hayo na anaamini ataitangaza vema
nchi katika mashindano hayo.
Kagasheki alisema kuwa sekta ya urembo nchini inakua na wao
wamejipanga kuitumia kutangaza vivutio vya utalii si kwa watu wa nje,
bali hata kwa wa ndani.
“Ni matarajio yetu kuwa atafanya vizuri katika mashindano hayo na
kuitangaza vyema Tanzania; tunamtakia kheri katika mashindano hayo,”
alisema Kagasheki.
Naye Betty, aliwaahidi watanzania kuwa, mbali na kurudi na ushindi
pia atakwenda kuitangazia dunia kuacha kutumia nakshi (mapambo),
yanayotumia pembe za ndovu ili kumaliza tatizo la ujangili nchini.
“Nimejiandaa vyema na ninaahidi kufanya vizuri, naomba Watanzania waniombee na kunipa ushirikiano mkubwa,” alisema Betty.
Naye Mkurugenzi wa Miss Universe Tanzania, Maria Sarungi, alimpongeza
waziri kwa ushirikiano wake katika mashindano hayo, ambayo mwaka huu
yalidhaminiwa na Hifadhi ya Taifa (Tanapa).
No comments:
Post a Comment