Mhe.
Mwigulu Lameck NCHEMBA Naibu Waziri wa Fedha na Mhe. Adam Kighoma Ali
MALIMA (Mb) Naibu Waziri wa Fedha na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya
fedha. (PICHA NA IKULU)
MAWAZIRI na manaibu waziri walioteuliwa kushika
nafasi mbalimbali jana waliapishwa na Rais Jakaya Kikwete katika viwanja
vya Ikulu jijini Dar es Salaam, huku baadhi yao wakianza na tambo za
uwajibikaji na wengine wakiomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau
ili waweze kutimiza majukumu yao.
Rais
Kikwete na Mhe. Mathias Meinrad CHIKAWE (Mb) Waziri wa Mambo ya Ndani
wakiwa na wakuu wa vyombo vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya mawaziri hao, Saada
Mkuya Salum (Wizara ya Fedha na Uchumi), Juma Nkamia (Naibu Waziri
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Dk. Asha-Rose Migiro
(Wizara ya Katiba na Sheria), kila mmoja aliomba ushirikiano kutoka kwa
wadau na Watanzania kwa ujumla.Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema changamoto ya kwanza atakayokabiliana nayo ni kuimarisha eneo la fedha ili nchi iweze kujitegemea na kuwabeza wanaomwita ‘waziri mzigo’, wasubiri waone utendaji wake.
Akizungumzia suala la mishahara ya wafanyakazi, alisema kama kuna upungufu uliojitokeza kipindi cha nyuma kwa mishahara kuchelewa, halitajirudia na kwamba mishahara itatolewa kwa wakati husika.
Alisema wanachotarajia kufanya kama wizara ni kuimarisha mapato ya ndani ili kuweza kuondokana na utegemezi wa mataifa mengine, hasa katika miradi ya ndani.
Alisema lazima serikali ijielekeze katika kupata miundombinu ya kiuchumi kwa ajili ya kuondoka katika hatua ya sasa na kuelekea hatua nyingine.
Aliongeza kuwa wakati wa uhai wa William Mgimwa, kuna mipango mingi ya kimaendeleo waliyofanya na kuahidi kuitekeleza kwa nafasi yake mpya ya uwaziri.
“Mimi sijui dhana ya kuitwa mizigo ina tafsiri gani, ninachojua ni kuwa Katibu Mkuu wetu, Kinana, alikuwa mikoani na wananachi walikuwa wanalalamikia baadhi ya mambo, hivyo ilikuwa ni wajibu wake kutuita na kupata ufafanuzi wa yale yaliyokuwa yanalalamikiwa na wananchi na si kwamba sisi ni mizigo,” alisema Mkuya.
Mwigulu aahidi kupambana na fedha chafu
Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi (Sera), Mwigulu Nchemba, amesema jambo la msingi atakalolitilia mkazo ni udhibiti wa fedha chafu na kwamba hiyo ni moja ya sekta iliyo katika Benki Kuu.
Alisema taasisi za kifedha zitafanya uchambuzi wa kitaalamu na kisha kuwasilisha bungeni mipango dhabiti ya kuwabana watu wanaotafuta njia ya kusafisha fedha haramu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema alipokuwa nje ya majukumu ya kiserikali amejifunza mengi ambayo atayatumia katika majukumu yake ya sasa, huku akieleza kuwa uzalendo utatawala katika suala zima la upatikanaji wa Katiba mpya.
Alisema hataruhusu hisia za kichama zitawale katika kuwapatia Watanzania katiba waitakayo, kwa kile alichoeleza kuwa mchakato wa katiba unamhusu kila Mtanzania pasipo kuangalia itikadi yake ya chama.
Nkamia alilia ushirikiano kwa waandishi
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, kwa upande wake alisema pasipo ushirikiano kutoka kwa wadau wasitegemee miujiza katika sekta nzima ya habari.
“Naomba kila mmoja wetu kwa nafasi yake ashiriki na tushirikiane, katika hili hakuna muujiza utakaofanywa na mtu mmoja, hasa ninyi ndugu zangu waandishi ni nguzo muhimu katika kutoa ushirikiano, naomba tushirikiane,” alisema Nkamia.
Mwanza waponda
Naye mwandishi, Sitta Tumma, kutoka Mwanza, anaripoti kuwa baadhi ya wananchi wakiwemo wanasiasa jijini Mwanza na mjini Musoma, mkoani Mara, wameponda na kubeza uteuzi huo, ambapo wameuita ni mtindo wa kupeana fadhila na kutesa kwa zamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi na wanasiasa hao walisema baraza hilo ni mzigo usiobebeka kwa wananchi, na Rais Kikwete amejitwisha mzigo ambao hatima yake ni kiama kwa taifa, kwani Watanzania walitarajia kuona mawaziri wawajibikaji, na si watu wa kutafuta fedha za uchaguzi mwaka 2015.
Walieleza kushangazwa na kuingizwa wizarani Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, ambaye amepewa Unaibu Waziri wa Fedha (Sera), Dk. Titus Kamani (Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Shukuru Kawambwa (Wizara nyeti ya Elimu), Hawa Ghasia (TAMISEMI), Juma Nkamia (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Lazaro Nyalandu (Wizara ya Maliasili na Utalii), pamoja na Mathias Chikawe kupewa Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, jijini hapa, Athumani Zebedayo, alieleza kushangazwa na hatua ya Rais Kikwete kumbakisha serikalini Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa na mawaziri wengine mizigo waliotakiwa na CCM kuondolewa.
Alisema kuachwa kwa mawaziri hao kunatia shaka iwapo kuna dhamira ya kweli ya kuwasaidia wananchi kupata maendeleo yaliyodumaa, na kwamba ni maajabu pia kuingizwa katika baraza hilo, Nchemba, Dk. Kamani, Ghasia, Chikawe, Nyalandu, Tibaijuka na Nkamia, kwani watu hao hawawezi kuwasaidia wananchi maskini.
(CHANZO NI TANZANIA DAIMA/ PICHA NA IKULU)
No comments:
Post a Comment