Na Sweetbert Lukonge
SIKU chache baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Amiss Tambwe, kutangaza kuikacha timu hiyo kutokana na ndoto zake za kutaka kushiriki michuano ya kimataifa kufeli, sasa yupo mbioni kujiunga na Azam.
Tambwe ambaye anaongoza kwa kuzifumania nyavu katika michuano ya ligi kuu msimu huu akiwa na mabao 19, amesema yupo tayari kutua klabuni hapo mara tu mipango yake itakapokamilika.
Mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe (kushoto) wakishangilia moja ya bao katika Ligi kuu ya Vodacom Tanzania.
Akizungumza na Championi Jumatano, Tambwe alisema kuwa taratibu za kujiunga na Azam zimepamba moto na tayari ameshafanya nao mazungumzo kupitia kwa wakala wake.“Baada ya kuzungumza na wakala wangu aliwaambia kuwa mimi nipo tayari kujiunga nao ila wanapaswa kumalizana na Simba kwanza kwa sababu bado nina mkataba nao, hivyo siwezi kufanya lolote bila yao kuridhia.
“Lakini kwa upande wangu sina tatizo lolote na endapo nitajiunga na Azam, kwangu litakuwa ni jambo jema na nitafurahi,” alisema Tambwe ambaye alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi.
Hivi Karibuni Tambwe aliliambia gazeti hili kuwa anataka kuondoka Simba kwa kuwa nia yake ni kucheza michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor, alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema kuwa kwa sasa hawezi kulizungumzia lakini ikitokea akampata Tambwe basi litakuwa ni jambo jema kwao.
“Tambwe ni mchezaji mzuri na kila kiongozi wa timu angependa kuwa na mchezaji kama yeye lakini kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kuhusiana naye kwani bado ni mali ya Simba lakini endapo itatokea tukampata itakuwa ni jambo zuri na jema kwetu,” alisema Nassor.
CHANZO NI CHAMPIONI JUMATANO
No comments:
Post a Comment