NIANZE kwa kulitaja kwa fahari kubwa jina la
Mwenyezi Mungu, Baba muweza wa kila jambo, kwa kutuwezesha kuwa wazima
wa afya, ambao leo kwa mara nyingine, tunakutana katika ukurasa wetu huu
wa kubadilishana mawazo mawili matatu.
Baada ya malumbano ya zaidi ya mwezi mzima ya jinsi gani upigaji kura utakuwa wakati wa kupitisha rasimu ya katiba katika Bunge Maalum, hatimaye ufumbuzi umepatikana kwamba sasa wajumbe watakuwa huru kuamua aina ya upigaji wake wa kura, iwe kwa siri au wazi.
Sasa kazi rasmi ya kupitisha rasimu inaanza kwa kamati zilizoundwa na Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kuanza kupitia kifungu kwa kifungu, mstari kwa mstari na neno kwa neno ili baadaye wawasilishe makubaliano ya wajumbe wa kamati hizo mbele ya Bunge Maalum kwa makubaliano ya pamoja.
Katika siku hizo za mvutano wa kanuni za kuendesha bunge hili maalum, mambo mengi sana yalijitokeza na kuleta majibizano ya maneno baina ya wajumbe wa chama tawala na wale wa kutoka upinzani kuhusiana na masuala mbalimbali, lakini zaidi yakiwa ni kuhusu aina ya muundo wa Muungano, uwe wa serikali moja, mbili au tatu.
Kimsingi, suala hili linalohusu Muungano, ndilo hasa lililosababisha mvutano wa aina ya upigaji kura, kwani inavyoonekana watu wamepania sana kulijadili suala hili, kitu ambacho ni kizuri kutokana na umuhimu wake.
Ninajua watu wengi sana wangependa kuona hatima ya majadiliano ya wabunge wetu kuhusu katiba mpya, wanasubiri kusikia wawakilishi hao watatoa aina gani ya katiba ili wananchi waipigie kura ya maoni. Mjadala mkubwa kwa idadi kubwa ya watu ni kujua kama muungano wetu utakuwa ni ule wa serikali mbili kama ilivyo sasa au tatu.
Binafsi, sina tatizo kabisa na aina ya muungano, uwe wa serikali moja, mbili au tatu. Kwangu mimi kitu cha kwanza ambacho nisingependa kipotee ni Tanzania. Nimezaliwa katika nchi yenye jina hili, nimekulia hapa na kwa kweli ninaipenda sana.
Nina uhakika hakuna anayeitakia mabaya nchi yetu, isipokuwa tu, tunatofautiana mawazo juu ya namna gani tuiendeshe. Sina tatizo na tofauti hizi za kimtazamo, kwa sababu hatuwezi kuendelea bila kufikiri tofauti.
Rai yangu kwa wajumbe wa bunge hili maalum ni kwamba umma wote wa Watanzania, macho yao yako kwenu, hawa wote wanawategemea kuwa mtafanya kila kilicho ndani ya uwezo wenu, kuhakikisha nchi yao inabaki salama, iliyo moja na yenye mshikamano zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Kama nilivyowahi kusema huko nyuma, siku mtakayoondoka hapo ndani ya jengo hilo tukufu na baadhi yenu wakashangilia kwamba wameshinda, basi ni lazima tujue kuwa katiba iliyopatikana siyo bora. Tunataka wajumbe wote wafanye kazi na siku ya mwisho, wote muwe na tabasamu, hata kama hamtakubaliana kwa kila jambo.
Nchi inahitaji mambo mengi zaidi ya uwepo wa serikali tunazopigania. Watu wetu ni maskini na wengi wanakosa haki zao za msingi. Ni wajibu wa wajumbe kuangalia jinsi gani vizazi vyetu, vya sasa na baadaye vitaishi katika nchi nzuri na yenye rasilimali nyingi kwa amani, utulivu, upendo na mshikamano, kama ambavyo waasisi wa taifa letu walivyotaka.
Waasisi wa taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Karume enzi za uhai wao, walikuwa wakisisitiza sana umoja wa kitaifa na kudumisha amani kwani walielewa sehemu yoyote isipokuwa na amani siyo rahisi kuwa na maendeleo.
Kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete anavyosema mara kwa mara, wote tuna dhamira ya kuijenga nchi yetu, hatuwezi kugombea fito. Kila kifungu cha katiba kitakachopitishwa, lazima kilenge kuiboresha Tanzania. Tuwe wakali kwa yeyote mwenye nia ya kututenganisha, bila kujali cheo chake, kwa sababu kama nilivyosema mwanzo, taifa kwanza, vyama baadaye!
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:
Post a Comment