Marehemu Gebo Peter enzi za uhai wake.
STRAIKA wa zamani wa timu ya Simba na Sigara, zote za jijini Dar es Salaam, Gebo Peter, aliyefariki dunia jana majira ya saa 11 alfajiri, anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Kigurunyembe mkoani Morogoro.
Peter ambaye pia enzi za uhai wake aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Manyema Rangers, alikutwa na umauti huo baada ya kuugua kwa muda mfupi na kulazwa katika hospitali ya Mwananyamala, kisha kuhamishiwa Muhimbili ambako ndiko alikofikwa na mauti.
Kifo hicho kimewasononesha watu wengi, hususan wanafamilia wa soka hapa nchini ambao walikuwa wakimfahamu mchezaji huyo tangu alipokuwa uwanjani, mpaka anastaafu alikuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza vifaa vya michezo.
Msemaji wa familia ya marehemu Peter, Supear Mbwembwe ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu ya Simba na Lipuli ya Iringa, alisema zoezi la ibaada na kuuaga mwili wa marehemu litafanyika saa 4:00 asubuhi huko nyumbani kwake Sahara Vingunguti.
“Baada ya zoezi hilo tutaanza safari ya kwenda nyumbani kwao mkoni Morogoro ambako ndiko alipo mama yake mzazi kwa ajili ya kuupumzisha mwili wa ndugu yetu.
“Hakika hili ni pigo kubwa kwa soka la Tanzania kwani tumempoteza mtu aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua zaidi katika soka na sekta nyingine,” alisema Mbwembwe.
Marehemu Peter ameacha mke na watoto watatu, wa kike wawili na mmoja wa kiume.
No comments:
Post a Comment