WAKATI ujio wa Kocha Marcio Maximo ukiwa njiani kukamilika, ambapo mpaka sasa ni asilimia 95, klabu ya Yanga ipo tayari kumpa mamilioni kila atakapofanikiwa kubeba taji.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa pamoja na gari la kutumia na nyumba ya kuishi, Mbrazili huyo amepewa ofa ya dola 12,000 (Sh milioni 19) kila atakapobeba ubingwa wa Tanzania Bara au Kombe la Cecafa.
Imeelezwa kuwa katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Yanga na Maximo suala hilo limeshapitishwa moja kwa moja, na pia kuna ofa nyingine iliyozungumzwa kuwa iwapo ataifikisha Yanga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, pia atapewa kitita cha kama hicho cha dola 12,000.
Mmoja wa watu wa karibu na wakala anayeshughulikia suala la Maximo kuja nchini ameliambia Championi Jumamosi kuwa mambo yanakwenda vizuri na Maximo amevutiwa na ofa hizo.
Championi Jumamosi ambalo lilikuwa gazeti la kwanza kuandika ujio wa Maximo, lilipohoji juu ya siku rasmi ya ujio wa kocha huyo, mtoa habari alifunguka:
“Bado hakuna uhakika sana lakini ni kati ya tarehe 14 au 15 ya mwezi huu (Juni), lakini inaonekana kila kitu kinakwenda vizuri sana na mambo yanaenda kwa mpangilio.
“Wakala wake amekuwa akilishughulikia suala hilo kwa ufasaha na utaratibu mkubwa na sasa Maximo anajua anakuja kufanyakazi akianza na makocha wazawa,” kilifafanua chanzo.
Maximo ambaye amewahi kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars na kufanikiwa kuivusha hadi michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan), ameelezwa kuwa ataanza kazi na usaidizi wa Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali.
Yanga imeamua kuanza kusaka makocha na katika maombi 44 ya makocha wa ndani na nje ya Tanzania, kamati ya ufundi ya Yanga iliona Maximo ndiye ameonekana kuwa na uzoefu zaidi na rekodi ya juu.
Hivyo, mazungumzo yakaanza kupitia Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye hivi karibuni wanachama wake waliamua kumuongezea muda wa miezi 12 kuendelea kuwepo madarakani baada ya muda wake wa awali kwa mujibu wa katiba kumalizika.
Katika hatua nyingine wachezaji wakongwe wa timu hiyo wameanza kujawa na hofu ya kupoteza nafasi zao.
Hali hiyo inatokana na nyota hao kukumbuka yaliyopita juu ya Maximo wakati alipokuwa akiifundisha Taifa Stars ambapo alikuwa ni muumini wa wachezaji wenye umri mdogo.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wachezaji wenye umri mkubwa katika kikosi cha Yanga wameanza kuingiwa na hofu ya kupoteza nafasi zao pindi Maximo atakapokabidhiwa jukumu hilo la kuifundisha timu hiyo ambayo msimu uliopita ilimaliza ligi kuu ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Azam.
Mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu ya Yanga ambaye aliomba kutotajwa jina lake gazetini, alisema baada mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji kutangaza kuwa wapo katika hatua za mwisho za kumalizana na Maximo, baadhi ya wachezaji wenye umri mkubwa walikuwa wakimpigia simu wakitaka kujua ukweli juu ya jambo hilo.
“Mchezaji mmoja kati ya hao alionyesha wasiwasi mkubwa juu ya nafasi yake kutokana na umri wake kuwa mkubwa ambapo alisema: “Ngoja tuone jinsi itakavyokuwa.”
“Nilipomuuliza kwa nini anasema hivyo, aliniambia kuwa Maximo ni muumini wa wachezaji wenye umri mdogo na siyo wakongwe, hivyo atakapoanza kazi inawezekana atatimua wengi, labda awe amebadilika,” alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, wasiwasi huo pia ulionyeshwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo ambaye sasa ni kocha mkuu wa JKT Ruvu, Fred Felix Minziro lakini aliuonya uongozi wa Yanga kutomwingilia Maximo katika maamuzi yake atakayokuwa akiyafanya kwa manufaa ya klabu hiyo.
“Najua Maximo atakapofika klabuni hapo, atafanya mabadiliko makubwa ya kiufundi lakini pia nafikiri wachezaji chipukizi huo ndiyo muda wao wa kuonyesha kuwa wanaweza kwa sababu jamaa ni muumini mzuri wa vijana,” alisema Minziro.
CHANZO CHAMPIONI JUMAMOSI 7/6/2014
No comments:
Post a Comment