Mshambuliaji wa Yanga, Genilson Santos ‘Jaja’ ameondolewa katika kikosi cha timu hiyo na nafasi yake itazibwa na kiungo mkabaji pia raia wa Brazil, Emerson Oliveira Neves Roque.
Jaja, ambaye yuko nchini kwao Brazil kwa mapumziko mafupi ya Ligi Kuu hatarejea nchini na sasa kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo atarejea Jumanne jijini Dar es Salaam akiwa na Emerson pamoja na kiungo mwingine wa timu hiyo, Andrey Coutinho.
Ingawa inaelezwa kuwa Jaja hatarudi nchini kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini presha kubwa aliyokuwa akiipata kwa mashabiki imechangia hilo na hivyo Maximo kuona ni bora ampumzishe kwani akiendelea kumng’ang’ania hata yeye anaweza kutimuliwa.
Mmoja wa wajumbe muhimu kwenye Kamati ya Usajili ya Yanga, Isaack Chanji aliliambia gazeti hili kuwa ni kweli Jaja hatarudi na Yanga, badala yake Maximo atakuja nchini na kiungo Emerson ili kufanyiwa majaribio na kama akifuzu, basi watamsajili.
“Kweli Emerson anakuja badala ya Jaja na atatua nchini Jumanne pamoja na Maximo, ila tutamwangalia kwanza ikiwamo kumfanyia majaribio na baadaye atafanyiwa vipimo vya afya yake na kama akifuzu, basi tutamsajili,” alisema Chanji.
Aliongeza: “Tunataka kuachana na Jaja kwani ni mchezaji ambaye tulitegemea makubwa kutoka kwake, lakini ameshindwa kuonyesha uwezo na hata mashabiki umeona wanalalamikia uwezo wake.
Jaja ambaye alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu hakuonyesha kiwango kilichotarajiwa na wengi na hivyo kila mara kuwakera mashabiki wa klabu hiyo na hata baadhi ya viongozi.
Licha ya Maximo kumtetea mara kwa mara kuwa nimshambuliaji mzuri, hasa kwa kufunga mabao ya vichwa, lakini mashabiki wengi hawakukubaliana na utetezi huo na wengi kuwapa presha viongozi wakishinikiza ‘atoswe’ na wazawa Jerryson Tegete na Hussein Javu wapewe nafasi zaidi uwanjani.
Uzito wake uwanjani, kushindwa kumiliki mpira na pia kushindwa kupachika mabao kama matarajio ya wengi ndizo sababu kubwa zinazomwondoa Jaja Yanga katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Mchezaji huyo aliyejiunga na Yanga kwa mbwembwe, aliifungia mabao matano katika mechi 11 alizoichezea, yakiwamo mawili kwenye mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Azam kabla ya kuanza kwa msimu na moja la Ligi Kuu.
Mabao yake Yanga ni katika michezo ya kirafiki dhidi ya Chipukizi ya Pemba na Thika United ya Kenya, kisha akafunga mawili kwenye mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam na kuiongoza timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3- 0 na kuipa ubingwa na akafunga bao moja katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Stand United mjini Shinyanga.Kwa upande wake, kiungo Emerson ana miaka 24 na alizaliwa katika jiji la Rio de Janeiro nchini Brazil na anatua
Yanga akitokea klabu inayocheza ligi ya jimbo la Rio ya Bonsucesso. Klabu hiyo ilianzishwa 1913.
No comments:
Post a Comment