Kocha mpya wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm.
Na Hans MloliYANGA inatarajiwa kupambana na Coastal Union leo jijini Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, lakini tayari Kocha wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, ameshaitangazia vita kali mechi hiyo.
Jumapili ya wiki iliyopita, Yanga ilitoka suluhu na Ndanda FC huku timu hiyo ikikosa mabao mengi ya wazi, hali iliyomkasirisha Pluijm na kuahidi kulimaliza tatizo hilo kwa kuonyesha makali ya washambuliaji wake katika mchezo wao huo wa leo.
Wachezaji wa Yanga, wakishangilia ushindi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Pluijm alisema
hali hiyo ya kushindwa kufunga mabao kwenye nafasi nyingi kama hizo
wanazozipata si nzuri na inawarudisha nyuma kwenye mbio za ubingwa,
hivyo atahakikisha wanautumia vyema mchezo wa Coastal kufuta makosa
hayo.“Tumekuwa kwenye mazoezi ya kila siku tukipigania suala hili la kufunga mabao mengi, lakini hali inaonekana si nzuri tukifika kwenye mechi, hali hii imekuwa ikijitokeza kwenye mechi zilizopita pia sasa nahitaji kulimaliza tatizo hilo mapema sana na kuanzia katika mechi inayofuata na Coastal, tutajitahidi kuhakikisha tunaanza kufunga mabao mengi kwa ajili ya kupata pointi muhimu.
“Unapocheza siku zote nia ya msingi ni kufunga mabao kwa ajili ya kujiweka sawa na kuibuka na pointi tatu, sasa kama hilo linakuwa haliwezekani, hapo panakuwa hakuna maana kwa kuwa tunarudi nyuma katika mbio za ubingwa lakini tutajitahidi kuifuta hali hiyo na kuanza upya kuanzia mechi ya Coastal,” alisema Pluijm.
Mpaka sasa inaaminika kuwa Yanga ni moja ya timu zenye safu kali ya ushambuliaji inayoundwa na Mliberia, Kpah Sherman, Mrundi, Amissi Tambwe, Danny Mrwanda, Simon Msuva, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete na Hussein Javu, lakini bado imekuwa na mwendo wa kusuasua katika ufumaniaji nyavu kwenye mechi za Ligi Kuu Bara za hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment