Dar es Salaam.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye alizua kizaazaa bada ya kutofautiana na maaskofu wenzake kuhusu Kura ya Maoni, jana alizungumzia suala la urais, akivitaka vyama vya siasa kuwaengua makada wake wanaotumia fedha kusaka urais.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye alizua kizaazaa bada ya kutofautiana na maaskofu wenzake kuhusu Kura ya Maoni, jana alizungumzia suala la urais, akivitaka vyama vya siasa kuwaengua makada wake wanaotumia fedha kusaka urais.
Kardinali Pengo alisababisha mkanganyiko wakati alipotofautiana na tamko la Jukwaa la Wakristo lililotaka waumini waisome Katiba Inayopendekezwa, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na siku ya Kura ya Maoni, wapige kura ya hapana kukataa mabadiliko hayo ya Katiba.
Tamko hilo lililotolewa na maaskofu wa madhehebu
mbalimbali ya Kikristo, lilieleza sababu kadhaa za kupingana na mchakato
wa kuandika Katiba Mpya, hasa suala la Serikali kuahidi kuingiza
Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba kwa lengo la kutaka Waislamu waipitishe
Katiba Inayopendekezwa.
Lakini Kardinali Pengo akakosoa tamko hilo akisema waumini hawana budi kuachiwa kufanya uamuzi wao bila ya kushurutishwa, kauli ambayo ilisababishwa akosolewa na wengi, akiwamo Askofu Josephat Gwajima ambaye amefunguliwa mashtaka ya kumdhalilisha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.
Jana, Pardinali Pengo alizungumzia masuala ya
kisiasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu alipokuwa mgeni rasmi
katika mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT)
ambako alionya dhidi ya matumizi ya fedha.
Akionya juu ya matumizi ya fedha katika harakati
za kuingia Ikulu, Kardinali Pengo alisema kwa mujibu wa imani na kanuni
za dini, uongozi ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na
“Kama wapo watu wanaotumia fedha kutaka kuingia
Ikulu, ni bora wakaachwa mara moja na vyama vyao. Hata wasipitishwe na
kuja kuomba kura kwetu. Ni vyema wakatambua kuwa uongozi haununuliwi,”
alisema Pengo.
Alifafanua kuwa rushwa ni kitu kibaya kama
itatumika kupata kiongozi katika ngazi yoyote ile na kwamba endapo
mtoaji atapewa nafasi aitakayo, bila shaka gharama alizozitumia atataka
zilipwe na wananchi anaowatumikia.
“Rushwa ni kitu ambacho kila kiongozi anapaswa
kukiepuka ili kuwaondolea wananchi uwezekano wa kuingia katika mchakato
wa kulipa deni ambalo kiongozi atataka alipwe (akiwa Ikulu) ingawa
alitoa kwa hiari yake wakati wa kujinadi na kuwawishi wapigakura,”
alisema. “Ni bora tumchague Rais maskini ambaye hatakuwa na madeni
binafsi ya kuyalipa na kwa pamoja tuelekeze nguvu zetu katika ujenzi wa
uchumi wa Taifa kwa ujumla. Watoa rushwa mwisho wa siku watataka tulipe
gharama walizotumia kutushawishi,” alisema kiongozi huyo wa kiroho
nchini.
Pamoja na hayo yote, Askofu Pengo alisema ni
lazima ushindani uwepo kuanzia ndani ya vyama kabla havijapata
mwakilishi atakayesimama kuviwakilisha mbele wa wananchi ili wachague
anayefaa zaidi kulitumikia Taifa.
Alisema ni vyema demokrasia ikaanzia huko kabla
haijahubiriwa nje kwani hilo huonekana kabla hata vyama hivyo havijasema
namna vinavyojiendesha.
Askofu huyo ametoa kauli hiyo wakati Taifa likiwa
kwenye mjadala kuhusu sifa za wagombea urais, huku kukiwa na malalamiko
mengi, hasa kutoka chama tawala cha CCM, dhidi ya makada wanaotuhumiwa
kutumia fedha kushawishi wanachama wao wawapitishe kuwania urais.
CCM, ambayo mgombea wake ndiye amekuwa akishinda urais tangu
siasa za ushindani wa vyama ziliporejeshwa mwaka 1992, imekuwa ikieleza
mara kwa mara kuwa makada hao hawatavumiliwa na vikao vya uamuzi
vitawaondoa katika mbio za kuwania kuteuliwa kugombea urais.
Mapema wiki hii, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip
Mangula aliwaambia viongozi wa chama hicho mkoani Dar es Salaam kuwa
fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama “kama maandazi”, zitakuwa
kitanzi chao kwenye Uchaguzi Mkuu, akisisitiza kuwa wanachama hao
watang’olewa.
Hata hivyo, chama hicho kimekuwa hakiripoti
vitendo hivyo kwenye vyombo vilivyoundwa kwa ajili ya kuzuia na
kupambana na rushwa na juzi, Takukuru ilisema chama hicho kikitoa
ushirikiano, itaweza kukomesha uovu huo.
Akizungumzia demokrasia ndani ya vyama, Kardinali
Pengo alitaka wagombea wengi zaidi kujitokeza ili kuwapa wananchi wigo
mpana wa kuteua mtu anayefaa.
“Wajitokeze wengi zaidi ndani ya vyama vyao.
Endapo vyama hivi vitadhihirisha demokrasia baina ya wanachama wao, ni
dhahiri itakuwa sifa ya ziada kwa wananchi ambao ndiyo wapigakura wenye
uamuzi wa mwisho,” alisema Kardinali Pengo.
Afya yake
Kwa muda wote wa sherehe hizo, Kardinali Pengo
alikuwa ameketi kutokana na afya yake kutokuwa nzuri ikiwa ni muda mfupi
tangu atoke India kwa matibabu ya mgongo na alitumia fursa hiyo kuwatoa
hofu wote kuhusu hali yake.
Alisema kuwa maradhi hayo yalianza tangu mwaka
2013 na baada ya kwenda Ujerumani alibainika kuwa na tatizo hilo ambalo
baadaye alishauriwa akatibiwe Hospitali ya Manipal iliyopo Bangalore,
India.
“Ninaendelea vizuri. Maumivu yamepungua kwa kiasi
kikubwa. Naomba wote wanaonitakia mema wasiwe na wasiwasi kwani matibabu
niliyopata yalikuwa mazuri na yenye msaada mkubwa kwangu,” alisema
kiongozi huyo ambaye anatembelea mkongojo.
CHANZO; MWANANCHI
CHANZO; MWANANCHI
No comments:
Post a Comment