NAULI ZA MABASI YA MASAFA MAREFU NA MIJINI
1.0 UTANGULIZI
Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2014 bei ya mafuta yatumikayo katika vyombo vya usafiri wa abiria nchini ilianza kushuka. Kufuatia kushuka huko kwa bei, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ilikuwa ikipokea wito wa kupitia upya viwango vya juu vya nauli ambavyo viliwekwa na Mamlaka mwezi Aprili, 2013. Hivyo SUMATRA ikaamua kuandaa mikutano ya wadau kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu haja ya kurekebisha viwango vya nauli zilizopo.
Aidha, tarehe 09 Machi, 2015, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na SUMATRA (SUMATRA Consumer Consultative Council (SCCC)) liliwasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) maombi ya kushusha nauli za mabasi ya masafa marefu na mijini. Katika maombi hayo Baraza liliainisha sababu za kuomba punguzo hilo kuwa ni kushuka kwa bei za mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya kutoka asilimia 25 hadi 10; punguzo hilo lilianza Julai, 2014.
1.1 MAOMBI
- Usafiri wa Mijini: Katika usafiri wa mijini, maombi yalikuwa ni kupunguza nauli kwa asilimia 25; hivyo kwa njia yenye umbali wa kilomita 10, nauli iliyopo sasa ya TZS 400 ilipendekezwa kushushwa hadi kufikia TZS 300.
- Usafiri wa Masafa Marefu: Maombi
yalikuwa ni kushusha nauli iliyopo kwa kilometa moja anayosafiri abiria
katika basi la kawaida kutoka TZS 36.89 hadi TZS 28.05; punguzo la
asilimia 23.96. Aidha, kwa basi la hadhi ya juu (luxury bus) kushusha
kutoka TZS 58.47 hadi TZS 47.19; punguzo la asilimia 19.29.
2.0 UTARATIBU WA KUFANYA MAPITIO YA NAULI
SUMATRA iliyafanyia kazi maombi hayo kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Sheria ya Bunge Na.9 ya Mwaka 2001, na Kanuni za Tozo za Mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo watoa huduma, watumiaji wa huduma pamoja na wananchi kwa ujumla ili kupata maoni yao. Ushirikishwaji huo ulifanywa kupitia mikutano iliyofanyika tarehe 9 Machi, 2015 Mkoani Mwanza; tarehe 12 Machi, 2015 Mkoani Kigoma; na tarehe 18 Machi, 2015 Jijini Dar es Salaam. Maoni yaliyotolewa katika mikutano hiyo yalizingatiwa katika tathmini na Mamlaka.
Taarifa ya tathmini na mapendekezo ya viwango vipya vya nauli iliwasilishwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA kwa ajili ya maamuzi.
3.0 NAULI ZA MIJINI
Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA ilikutana Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili, 2015 ili kupitia taarifa ya tathmini na mapendekezo ya viwango vya nauli kwa ajili ya maamuzi.
3.1 Masuala Yaliyobainika
Kufuatia tathmini iliyofanywa ya usafiri wa mijini, BODI ilibaini kwamba:
- Bei ya mafuta ilikuwa imeshuka ikilinganishwa na bei iliyokuwepo wakati viwango vilivyopo sasa vilipoanza kutumika Mwezi Aprili, 2013; ambapo kwa wastani bei ya lita ya dizeli iliuzwa TZS 2,071.67 kufikia Machi, 2015 wastani wa bei ya Dizeli kwa lita katika vituo ulishuka mpaka TZS 1,665.38; mwezi Aprili, 2015 bei ya wastani ilipanda kufikia TZS 1,779.57.
- Mwenendo wa bei za mafuta kufikia Aprili, 2015 unaonyesha kuwa bei ya mafuta imekuwa ikibadilikabadilika na kwamba kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda.
- Gharama za mafuta zilikuwa muhimu kuzingatiwa pamoja na gharama nyinginezo, ambazo zilifikia asilimia 70 ya gharama za uendeshaji.
- Kulikuwa na mabadiliko katika viashiria vya kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na thamani ya shilingi na mabadiliko hayo yalipaswa kuzingatiwa katika kukokotoa viwango vya nauli.
- Punguzo la ushuru wa forodha kwa uagizaji wa mabasi mapya ulikuwa na faida katika kuchochea uingizaji wa mabasi mapya nchini ili kuboresha hali ya usafiri nchini. Hata hivyo sehemu kubwa ya mabasi yaliyopo nchini kwa sasa hayakupata punguzo hilo kwa kuwa yaliingizwa kabla ya Julai, 2014 punguzo hilo lilipoanza kutumika.
- Mazingira ya uendeshaji na utoaji huduma za usafiri mijini yanapaswa kuzingatiwa ili kufikia viwango vya nauli ili kuifanya huduma ya usafiri kuwa endelevu. Kwa upekee, ongezeko la msongamano wa magari mijini na athari zake katika utoaji wa huduma za usafiri mijini zinapaswa kuzingatiwa.
- Gharama za utoaji huduma za usafiri mijini zinapaswa kutazamwa kwa ujumla wake, ikiwa ni pamoja na punguzo la bei ya mafuta, ili kufikia viwango vya nauli vinavyostahili.
- Baada
ya kuzingatia vigezo muhimu katika ukokotoaji wa nauli, punguzo
lililojitokeza katika viwango vya nauli kikomo ni kama inavyobainishwa
hapa chini:
Viwango Vya Nauli Kutokana na Ukokotoaji
Njia |
Nauli ya Sasa
|
Nauli iliyokokotolewa
|
%
|
0 - 10 km (+CBD) |
400
|
376.77
|
5.8
|
11 - 15 km |
450
|
448.62
|
0.3
|
16 - 20 km |
500
|
485.34
|
2.9
|
21 - 25 km |
600
|
583.34
|
2.8
|
26 - 30 km |
750
|
742.74
|
1
|
3.2 Maamuzi ya BODI
Baada ya kutafakari viwango vilivyotokana na ukokotoaji uliozingatia masuala muhimu yaliyoainishwa, BODI imeridhia viwango vya nauli vilivyopo sasa kuendelea kutumika.
Uamuzi huu unatokana na punguzo lililokokotolewa Kuwa dogo ikilinganishwa na viwango vilivyopo sasa. Aidha, viwango vilivyokokotolewa iwapo vitapitishwa vitasababisha usumbufu katika malipo.
- Viwango vya Nauli Mpya kwa Watu Wazima
Viwango vipya vya nauli kikomo vya mabasi ya mjini vilivyoridhiwa kwa watu wazima ni kama ifuatavyo:Viwango Vya Nauli Mjini Vilivyoridhiwa
Njia |
Nauli ya Sasa
(TZS)
|
Viwango Vilivyoridhiwa
(TZS)
|
0 - 10 km (+CBD) |
400
|
400
|
11 - 15 km |
450
|
450
|
16 - 20 km |
500
|
500
|
21 - 25 km |
600
|
600
|
26 - 30 km |
750
|
750
|
- Viwango vya Nauli Mpya kwa Wanafunzi
BODI imeamua kuwa nauli ya mwanafunzi nayo ibaki kama ilivyo nauli ya sasa ambapo mwanafunzi analipa TZS 200.
- VIWANGO VYA NAULI ZA MABASI YA MASAFA MAREFU
BODI ilipokea tathmini kuhusu nauli za usafiri wa masafa marefu.
4.1 Masuala Yaliyobainika
Kufuatia tathmini iliyofanywa ya nauli kikomo za usafiri wa masafa marefu, BODI ilibaini kwamba:
- Bei ya mafuta ilikuwa imeshuka ikilinganishwa na bei iliyokuwepo wakati viwango vya sasa vilipoanza kutumika Mwezi Aprili, 2013; ambapo kwa wastani bei ya lita ya dizeli iliuzwa TZS 2,071.67 kufikia Machi, 2015 wastani wa bei ya Dizeli kwa lita katika vituo ulishuka mpaka TZS 1,665.38; mwezi Aprili, 2015 bei ya wastani ilipanda kufikia TZS 1,779.57.
- Mwenendo wa bei za mafuta kufikia Aprili, 2015 unaonyesha kuwa bei ya mafuta imekuwa ikibadilikabadilika na kwamba kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda.
- Gharama za ununuzi wa mafuta zilikuwa muhimu kuzingatiwa pamoja na gharama nyinginezo, ambazo zilifikia asilimia 70 ya gharama za uendeshaji.
- Kulikuwa na mabadiliko katika viashiria vya kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na thamani ya shilingi na kwamba mabadiliko hayo yalipaswa kuzingatiwa katika kufikia viwango vya nauli.
- Punguzo la ushuru wa forodha kwa uingizaji wa mabasi mapya lilikuwa na athari chanya katika kuchochea uingizaji wa mabasi nchini. Hata hivyo sehemu kubwa ya mabasi yaliyopo nchini kwa sasa hayakupata punguzo hilo kwa kuwa yaliingizwa kabla ya punguzo hilo kuanza kutumika.
- Katika ukokotoaji wa nauli ni muhimu kuzingatia madaraja ya mabasi kama yalivyoelekezwa katika Kanuni za Huduma za Abiria, 2014 (The Road Transport (Passenger Service) Regulations, 2014 zinazoainisha madaraja manne ya mabasi;daraja la kawaida la chini, daraja la kawaida la juu, daraja la hadhi ya kati na daraja la Juu.
- Gharama za utoaji huduma za usafiri kwa ujumla wake zinapaswa kuzingatiwa kwa madaraja mbalimbali ili kufikia viwango vya nauli vinavyostahili.
- Udhibiti
wa nauli unapaswa kujielekeza katika madaraja matatu yafuatayo: (1)
daraja la kawaida la chini, (2) daraja la kawaida la juu na (3)daraja la
hadhi ya Kati ili kutimiza wajibu wa kuwalinda watumiaji wenye kipato
cha chini.
4.2 Maamuzi ya BODI
Baada ya kutafakari tarifa iliyowasilishwa BODI iliridhia viwango vipya vya juu vya nauli kwa mabasi ya masafa marefu kuwa kama vinavyoonyeshwa hapo chini:Viwango Vipya vya Nauli za Mabasi ya Masafa Marefu
Daraja la Basi |
Nauli ya Sasa
(TZS/Abiria/Km)
|
Viwango Vipya vya Nauli Vilivyoridhiwa
(TZS/Abiria/Km)
|
%
|
Daraja la Kawaida la Chini (Lower Ordinary bus -Lami |
36.89
|
34.00
|
7.8
|
Daraja la Kawaida la Chini Lower Ordinary Bus) - Vumbi |
46.11
|
42.50
|
7.8
|
Daraja la Kawaida la Juu (Upper Ordinary Bus) |
-
|
44.96
|
-
|
Daraja la Kati (Semi-Luxury Bus) |
53.22
|
50.13
|
5.81
|
BODI pia imeamua kwamba nauli za mabasi ya hadhi ya juu ( luxury bus) hazitadhibitiwa ili kuchochea ubunifu katika utoaji huduma na ushindani kati ya huduma za barabara na njia nyinginezo za usafiri.
Mamlaka imeandaa majedwali ya nauli kwa kuzingatia viwango vipya. Majedwali hayo yanaweza kupatikana katika tovuti ya Mamlaka www.sumatra.go.tz.
HITIMISHO
Viwango hivi vipya vinapaswa kuanza kutumika siku 14 baada ya taarifa kutolewa kwa umma. Hivyo basi viwango hivi vitaanza rasmi tarehe 30 Aprili, 2015.
Wamiliki wa mabasi pamoja wafanyakazi wao wanaagizwa kutoza viwango vya nauli vilivyoridhiwa na Mamlaka.
Aidha, abiria na wananchi kwa ujumla wanahamasishwa kutoa taarifa SUMATRA kupitia namba za simu za bure ambazo ni 0800110019 na 0800110020 pale wanapotozwa nauli ya juu zaidi ya nauli kikomo iliyoridhiwa.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
SUMATRA
15 Aprili, 2015
No comments:
Post a Comment