Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Aloyce Masanja (kushoto).
KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Bonde la Mto Rufiji
(RUBADA), Aloyce Masanja na wenzake wawili wamesimamishwa kazi kwa
tuhuma za ubadhirifu wa fedha na kujilimbikizia madaraka.Viongozi wengine waliosimamishwa kuanzia jana ni Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji, Tatu Ndatulu na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Filozi Mayayi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira alisema baada ya kuwepo kwa malalamiko yaliyokuwa yanatolewa na wawekezaji kwa muda mrefu, serikali iliamua kuunda Tume Novemba mwaka jana.
Tume hiyo ilikuwa chini ya Semroki Mwanyika, ambaye sasa ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ukaguzi wa Ndani wa Serikali katika Wizara ya Fedha (Hazina).
Wassira alifafanua kuwa viongozi hao wanasimamisha kazi kwa tuhuma za kuiibia Serikali kwa miaka miwili, utovu wa nidhamu na kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu kama watumishi wa umma.
Pia alisema licha ya kuwasimamisha kazi viongozi hao, ripoti iliyoibua ubadhirifu huo, itapelekwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Mimi kama Waziri nimeamua kuwasimamisha kazi watu hao kutokana na kutowajibika ipasavyo katika nyadhifa zao, pia wamekuwa watovu wa nidhamu. Suala la makosa ya jinai nitawaachia Polisi na Takukuru ambao watajua ni lini watawafikisha katika vyombo vya sheria,’’ alisema Wassira.
Waziri huyo alieleza katika miaka hiyo miwili, Rubada walikusanya zaidi ya Sh bilioni 2.7 kutoka kwa wawekezaji. Aidha, alisema kati ya hizo, Sh milioni 740 tu ndizo zilizotumika kihalali, huku kiasi kingine kikiwa hakijulikani kilipo.
Alifafanua kuwa, kati ya zilizotumika, Sh milioni 13.9 imeelezwa zimetumika kwa matumizi yao binafsi huku Sh milioni 13 zimetumika kwa ajili ya masurufu ambayo hayajarudishwa.
‘’Pamoja na hayo, Sh milioni 326 zilitengwa kwa ajili ya kujenga Kambi ya Kilimo maeneo ya Mkongo na hazikufanya kazi iliyotakiwa. Pia walichukua Sh milioni 58 ambazo zilitakiwa zipelekwe Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), lakini hazikupelekwa,’’ alidai.
Aliongeza; ‘’Kwa maana hiyo wafanyakazi walioko kazini kwa sasa wakistaafu, hawataweza kulipwa mafao yao kutokana na pesa zilizotakiwa kupelekwa hazijafikishwa sehemu husika’’.
Hii ina maana kwamba, mbali ya Sh bilioni 2 ambazo hazijulikani zilipo, kiasi kingine cha Sh milioni 384 kutoka mradi wa kambi ya Kilimo Mkongo na zile za NSSF, jumla ya fedha ambazo hazijulikani zilipo ni Sh bilioni 2.3.
Wassira, mmoja wa wanasiasa na viongozi wakongwe walioshika nyadhifa za uwaziri tangu enzi za utawala wa
Awamu ya Kwanza chini ya Rais Julius Nyerere, alidai watumishi hao walikuwa wanatembea na fedha mifukoni, wakijifanya wao ni wahasibu, ambapo fedha nyingine walikuwa wanaweka kwenye akaunti ya serikali huku nyingine wakiweka katika akaunti zao binafsi.
Aidha, alisema Rubada kulikuwa na uongozi mbaya kwa kuwa na ubinafsi, rushwa na kwamba mfumo wa ndani ulikuwa na ubadhirifu.
Akizungumzia suala la uteuzi wa viongozi wapya, Wassira alisema ameiagiza Bodi ya mamlaka hiyo kutafuta watu weledi na waaminifu, watakaokaimu nafasi hizo.
Akijibu swali kuhusu ubadhirifu unaofanywa na viongozi wanaokaimu nafasi mbalimbali, alisema; ‘’Suala la kukaimu sio sababu ya kuwa fisadi na kuwa mbadhilifu wa fedha za serikali, kwani wapo wengine wanakaimu na wanafanya vizuri hata kuthibitishwa na kuwa wakurugenzi.’’
(CHANZO: HABARI LEO)
No comments:
Post a Comment