WAKATI zoezi la uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa kielekrtioniki uitwao Biometric Voters Registration (BVR), jijini Dar es Salaam ukiendelea, mengi yameibuka kwenye baadhi ya vituo vya uandikishaji na kuwafanya wananchi wengi kukata tamaa wakidai kuwa zoezi hilo kwao sasa ni mateso.
Wananchi kadhaa waliohojiwa na gazeti hili walisema zoezi hilo la uandikishaji ni gumu kwa sababu baadhi yao huamka saa sita usiku kuwahi vituoni lakini baadaye wanajikuta wakiandikishwa siku ya pili.
Mama mmoja aliyekutwa Kituo cha Shule ya Msingi Kisiwani, Ubungo Dar, Mariam Ally alisema katika kituo hicho Jumamosi iliyopita wananchi walipigana kutokana na mwingiliano wa namba zinazotolewa kwa kila anayefika kujiandikisha.
Mwandikishaji akiandikisha wapiga kura kwenye mfumo wa BVR.
“Kuna watu walifika saa sita usiku, lakini asubuhi walipofika wakakuta waliochelewa wanaandikishwa, fujo ilitokea ikabidi polisi kuitwa wakaweka mambo sawa, kifupi ni kwamba haya ni mateso,” alisema Mariam.
Nao wananchi waliokutwa katika Kituo cha Kimara walisema kuwa katika kituo hicho watu hukesha.
…Akichukuliwa alama za vidole.
Mkazi wa eneo hilo, Massawe J. Massawe alisema japokuwa amepata kitambulisho cha kupigia kura lakini alifika kituoni hapo saa tisa usiku.
“Ilinibidi niamke mapema ili niwahi kupata kitambulisho lakini tangu saa 9 usiku nilivyoamka nimekuja kupata kitambulisho saa 6 mchana, kiukweli watu wanateseka sana hasa wale wenye watoto wadogo na wazee, hawapewi kipaumbele na wananchi.
Mmoja wa waandikishwaji akikabidhiwa kadi yake ya mpiga kura mara baada ya kukamilisha taratibu za kujiandisha.
Naye Frida George mkazi wa Mbagala Rangi Tatu alipokutwa akitoka katika kituo cha kujiandikisha alisema: “Nimewahi tangu saa kumi usiku na sasa hivi ni saa kumi na nusu jioni, pima mateso niliyoyapata, ilikuwa nimlete mama yangu mzazi kuandikisha, sitafanya hivyo kwa sababu ni mtu mzima ana zaidi ya miaka themanini.”
Naye mkazi wa Sinza aliyejitambulisha kwa jina moja la Pius aliliambia gazeti hili kuwa wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia uongozi kwa kutofuata mfumo unaotakiwa na kusababisha watu wengi kuishia kuchukua namba na kutorudi tena baada ya kuona usumbufu.
“Mimi nilikwenda pale saa moja asubuhi, nilipofika nikakuta foleni ya namba nikachukua namba tisini nikaamua kuchana namba na kwenda kuendelea na shughuli zangu kwa maana nahisi muda unakwenda bure labda nijipange tena kwa mara nyingine niamke mapema zaidi.”
Wakazi wa Kinondoni jijini Dar waliliambia gazeti hili kuwa, uandikishaji unakwenda taratibu hali inayofanya mtu mmoja kuchukua dakika 30 au zaidi kupata kitambulisho cha mpiga kura akiingia ndani.
“Hapa tulipo huwezi kuamini kama wengine tumekuja saa nane usiku lakini mpaka muda huu (saa sita mchana) tupo tu kwenye foleni ambayo haitembei, yaani ni mateso, tunapata shida sana serikali itambue hili, ikibidi iongeze siku,” alisema Fatuma Abdallah.
Festus Yohana aliyekuwa kwenye kituo cha kujiandikishia wapiga kura cha Shule ya Msingi Mwenge alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilipaswa kujua kuwa Dar ina watu wengi, hivyo mashine zingeletwa nyingi ili kuondoa mateso hayo wanayopata wananchi.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa licha ya zoezi hilo kuwa na changamoto nyingi lakini katika vituo vingi ambavyo waandishi wetu walitembelea kwa siku tatu walikuta zoezi likiendelea kwa hali ya utulivu huku akina mama wenye watoto wadogo na wazee wakilalamikia utaratibu wa kutowapa kipaumbele kuandikisha, wengine wakidai kuandikisha kwa rushwa katika baadhi ya vituo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema kwa njia ya simu juzi kuwa wanaendelea kufuatilia mchakato huo ili kubaini dosari zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wake huku akiweka wazi wanafuatilia taarifa za kuwapo baadhi ya wanaoendekeza vitendo vya rushwa katika zoezi hilo.Pia, alisema wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha wataalamu wa mashine hizo za BVR wanapelekwa vituoni ili kufanya matengenezo iwapo kutatokea mashine kuwa na tatizo linalokwamisha uandikishaji.
No comments:
Post a Comment