EFM RADIO

EFM RADIO

HERICONY

Tangaza hapa

Tangaza hapa

TANGAZA NA BLOG YAKO HAPA

TANGAZA NA BLOG YAKO HAPA

Wednesday, July 22, 2015

Lembeli, Bulaya rasmi Chadema

Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kahama mkoani Shinyanga, Mhe. James Daudi Lembeli.
Hatimaye Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, ametangaza kukipa kisogo Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Pia, Lembeli ameomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya ubunge katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu katika Jimbo la Kahama Mjini.  Naye, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya, anatarajiwa kutambulishwa rasmi jijini Mwanza leo wakati viongozi wa juu wa Chadema watakaopofanya mkutano mkubwa wa hadhara.  Pia ameandaliwa mapokezi makubwa na viongozi wa Chadema mkoani Mara na kutambulishwa kwa wananchi wa mkoa huo.
2160EE3E-A242-3CD6-E6CC-B1027830C58C_Esther-Bulaya-Mbunge-CCM
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya.
LEMBELI
Akitangaza kuhama chama hicho tawala jana mbele ya waandishi wa habari, Lembeli alisema kilichomsukuma kukihama chama hicho ni mizengwe yenye hujuma inayofanywa na viongozi wa CCM mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Kahama, kukithiri kwa rushwa na kukiukwa kwa kanuni na  taratibu za chama.
Alisema CCM siyo mbaya lakini baadhi ya viongozi ndiyo wabaya kwani licha ya watu kupiga kelele juu ya rafu zinazoendelea lakini wamezifumbia macho huku viongozi husika wakiwa nyuma ya mchezo huo mchafu.
Alisema kabla ya jimbo hilo kugawanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kupatikana Jimbo la Ushetu, kulikuwa na jimbo moja la Kahama ambalo mwaka 2010 kulikuwa na mizengwe na watu kupewa fedha ili kufanya kampeni chafu dhidi yake.
Lembeli ambaye amewahi kuwa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) hadi 2005, alisema mizengwe hiyo ilianza kwa kuwapo kwa jimbo hewa la Kahama Mjini ambalo yaliwekwa majina hewa ya wagombea na lake (Lembeli) na kwamba Rais Jakaya Kikwete ndiye alirejesha jina lake.
Alisema kwa mchakato wa watangaza nia wa sasa, Julai 12, mwaka huu, siku mbili kabla ya siku ya kuchukua fomu, baadhi ya wagombea walikuwa vijijini kuorodhesha majina na kadi za wanachama huku wakizikusanya kwa kutoa fedha cha Sh. 3,000 kwa kila anayechukuliwa kadi.
“Sipendi rushwa niliwataadharisha juu ya rushwa inayoendelea, Lembeli hawanitaki ndani ya chama na wilayani, na sina sababu ya kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho,” alisema na kuongeza:
“Nilishasema mizengwe ikiendelea sitakuwa sehemu yake, wajibu wangu ni kuhudumia wananchi, jimbo siyo mali yao (viongozi), nililelewa ndani ya CCM nakishukuru lakini sipo tayari kulea wizi, rushwa na mizengwe.”
Lembeli alisema ametafakari na amejadiliana na mama yake kwa saa 10, mke na watoto wake pamoja na wananchi wake wameunga mkono uamuzi wake wa kukihama chama hicho na kugombea jimbo hilo hilo kwa tiketi ya Chadema.
Lembeli ambaye katika Bunge la 10 alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, alisema kilichotokea Jimbo la Monduli kwa madiwani wake 20 kukihama chama ndicho kitatokea katika jimbo hilo.
“Najitoa ndani ya CCM ambacho nilikipenda sana, nililelewa ndani ya CCM ila nimelazimika kuchukua uamuzi mgumu sana, walinipenda na wapo watakaonichukia na kukereka ila nawataka warejelee yanayotokea wilayani Kahama na ndani ya CCM kwa ujumla,” alisema  Lembeli ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Bunge ya Kuchunguza madhara ya Operesheni Tokomeza iliyopelekea mawaziri wanne kujiuzulu.
Aidha, aliwaomba wananchi wa jimbo jipya la Ushetu ambako ndipo alipozaliwa kumsamehe na kwamba amepima na kuona Kahama Mjini ndiko kunakomfaa na anafanya hivyo kwa kuwa awali lilikuwa jimbo moja na aliliongoza kwa miaka tisa.
Lembeli ambaye mara zote amekuwa na misimamo ya kupinga mambo ambayo anaona hayako sahihi, alisema ana amini katika uadilifu na kwamba kosa ni kurudia kosa na kwamba mwaka 2010 hakuhama chama kwa kuwa alikuwa katika mshangao wa kilichofanywa na viongozi wake wa chama.
“This time (safari hii) naona mizengwe inajirudia tena ndiyo maana nimeona nijiondoe, kwani ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji, ni heri kuepusha shari kuliko kusubiri shari kamili,” alisema na kuongeza:
“Kinachonikimbiza CCM ni mizengwe ya wana- CCM kwa CCM na rushwa iliyokithiri kuanzia ngazi ya shina, kata, wilaya hadi mkoa, rushwa imetapakaa hadi ngazi ya chini kabisa, watu wanapewa fedha.”
“Rushwa ndani ya chama na serikali kwa sasa ni kubwa, zamani waliohusishwa na rushwa walikuwa wakubwa pekee, ila kwa sasa hata ngazi ya shina inatolewa na kupokelewa, makatibu kata ndiyo waandaaji wa mikutano ya watangaza nia ambayo sheria hairuhusu,” alisema.
Alisema kwa sasa ugonjwa wa ukimwi ni afadhali kwa kuwa ukiingia mwilini unapata dawa za kuongeza maisha lakini rushwa imesambaa kama saratani ambayo mgonjwa wake atakufa wakati wowote.
Alisema wapo wanaoshinda kura za maoni ndani ya chama hicho lakini majina yao yanakatwa kwa sababu ya rushwa  na kwamba hajawahi kutoa rushwa tangu alipogombea ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2005.
KUSAFISHWA MAWAZIRI
Lembeli alisema yeye ni mtetezi wa kila mtu na alishangazwa na uamuzi wa Ikulu kumsafisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, huku wakiachwa mawaziri wengine wanne ambao waliwajibika kutokana na wizara zao kuhusishwa na makosa yaliyotokea na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye alihusishwa na sakata la Richmond.
“Katika kusafisha watu wapo ambao hawakutendewa haki hasa Lowassa, unawezaje kusafisha wengine na wengine kuwaacha wakati uwajibikaji wao unafanana?” Alihoji.
AIFAGILIA CHADEMA
Mbunge huyo alisema Chadema ni chama kikuu cha upinzani nchini kwa sasa na hakina rushwa na kwamba itachukua miaka 50 ijayo kwa rushwa kusambaa hadi ngazi ya mashina kama ilivyo ndani ya CCM.
BUNGE LA KATIBA
Alisema msimamo wake ndani ya Bunge la Katiba ulikuwa wazi kwa kuwa alipiga kura ya hapana kwa uwazi kwa kuunga mkono rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na kwamba kubaki kwake ndani ya Bunge hilo baada ya upinzani kutoka nje kusitafsiriwe kuwa anaunga mkono Katiba inayopendekezwa.
KUNGURUMA JULAI 25
Lembeli alisema anatarajia kujitambulisha akiwa na mavazi ya Chadema kwa wananchi wake Julai 25, mwaka huu.
BULAYA KUPOKELEWA LEO
Kiongozi mmojawapo wa juu ndani ya Chadema aliithibitishia NIPASHE jana kuwa Bulaya atatambulishwa jijini Mwanza katika mkutano wao mkubwa hadhara jijini humo leo.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa kutoka mkoani Mara, ambazo zimethibitishwa na Mwenyekiti wa Chadema mkoa, Vimcent Nyerere, Bulaya amempigia simu kuwa kuanzia sasa ni mwanachama wa Chadema.
“Amenithibitishia kwamba ni mwenzetu ndani ya Chadema na kuanzia kesho nina mikutano naye ya kumtambulisha kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kumkabidhi kadi ya uanachama…pia tunapokea viongozi wengine kutoka CCM,” alisema Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini.
Jitihada za NIPASHE kumpata Bulaya kuthibitisha suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya kiganjani kutopatikana na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.
Bulaya amenukuliwa katika ukurasa wake wa Facebook akieleza kuwa CCM wilayani Bunda haimtaki, hivyo ameona aelekee kwingine ambako hakuweka wazi ni wapi.
Tofauti na ilivyotarajiwa Mbunge huyo wa Viti Maalum hajachukua fomu ya kugombea ubunge tofauti na ahadi yake kuwa atasimama katika jimbo hilo ambalo Mbunge wake ni Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira.
NATSE ANG’ATUKA KARATU
Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Karatu kwa tiketi ya Chadema, Mchungaji  Israel Natse, amejitoa rasmi katika siasa na kurudia kazi yake ya uchungaji katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu ya kiganjani jana, alisema makubaliano yake na chama walimwomba agombee kipindi kimoja tu na sasa anapisha mwingine.
“Mimi ninarudi kwenye kazi yangu ya uchungaji naachana na siasa, huu ndiyo wito wangu nilioitiwa na mungu wa uchungaji,” alisema.  Akizungumza kwa njia ya simu ya kiganjani, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro, alisema kwa Jimbo la Karatu waliochukua fomu za kugombea ubunge ni Lazaro  Masai, Fransisca  Duwe, William Kumbalo, Kwamala  Aloyce na Pascal Gutt.
MWENYEKITI MONDULI AHAMIA CHADEMA
Kasi ya viongozi na wanachama wa CCM wilayani Monduli kukihama chama hicho imeendelea baada ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Lashaine, Lesineti Mungaya, kurejesha kadi na kujiunga na Chadema.
Mungaya alirudisha kadi hiyo Julai 19, mwaka huu katika ofisi za Chadema wilayani humo na kukabidhiwa kadi mpya ya chama hicho.
Akizungumza baada ya kurudisha kadi hiyo, Lesineti alisema ameamua kutangaza uamuzi huo katika mkutano wa wananchi wa kijiji chake ili awashukuru na pia kuwaaga kwa kuachia nafasi yake ya uenyekiti wa kijiji na kuamua kujiunga na Chadema.
Alisema uamuzi huo aliufanya yeye binafsi na hajashawishiwa na mtu yoyote.
“Nawashukuru kwa kunichagua ila nawaaga rasmi nahamia Chadema na ahadi yangu ilikuwa ni kutatua tatizo la maji kijijini hapa nimetimiza kwa kutumia fedha zangu za mfukoni Sh. milioni 14 japo nimekaa muda wa mwaka mmoja,” alisema.
Pia, aliwaeleza viongozi wa Chadema wilaya hiyo kuwa kuna wenyeviti saba wa vijiji vya kata hiyo ya Lashaine ambao Alhamisi ya wiki hii nao watarudisha kadi na kujiunga na Chadema katika mkutano mkubwa utakaofanyika katika kata yao.
Akimpokea ofisini kwake, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Monduli, Japhet Sironga, alimshukuru kwa uamuzi wake wa kuamua mapema kuvua gamba na kuvaa gwanda.
‘’Nakupongeza sana Mungaya wewe ni kijana mwenye mtazamo mkubwa wa mbali, umeamua kwa hiari yako tena bila kusubiri hata siku ya mkutano umerejesha kadi ya CCM na kujiunga nasi tunakuahidi ushirikiano ndani ya chama na nakuomba uwe mvumilivu katika changamoto utakazokutana nazo ndani ya chama hiki,” alisema.
Katika hatua nyingine, Lesineti ambaye anatajwa ni miongoni mwa watu wa karibu na aliyetangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM na jina lake kuondolewa katika hatua za awali Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa,  baada ya kujiunga na Chadema, aliamua kuchukua fomu ya kuwania udiwani katika kata ya Lashaine kupitia chama hicho.
Imeandikwa na Salome Kitomari, Dar na Cynthia Mwilolezi, Arusha
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

HABARI MBALIMBALI

‘Dk. Cheni’ ‘Sharo Milionea ‘Thea’ African Women AGNESS MASOGANGE AK CLASSIC COSMETICS ALI KIBA Amanda Poshy Ant ANT LULU Ashley Toto Aunt Ezekiel Aunty Ezekiel AUNTY LULU Azam Fc Baby Madaha BAHATI BUKUKU Barnaba BATULI BBA Beauty of the day Belle 9 BI KIDUDE BIBI BOMBA Big Brother Big Brother Africa Bill Gates BINTI KIZIWI BOB JUNIOR Bodi ya Filamu Bongo Movie Bongo Movies CCM CHADEMA Chombezo Christina Shusho Chuchu hans. Clouds Media Group Club Bilicanas DAR LIVE DAVINA Dayna Nyange Diamond Dida Diva Loveness Love Dj Ommy Crazy wa Maisha Club DOGO JANJA DOKI DR.CHENI DSTV Dude Dully Sykes EBSS 2013 Elizabeth Michael Epiq Bongo Star Search (EBSS) ESHA BUHETI Ester Bulaya Feza Kessy FIESTA 2014 Flaviana Matata FLORA MBASHA FLORA MVUNGI Francis Cheka GARDNER GLOAL PUBLISHERS GLOBAL TV ONLINE H. BABA Halima Mdee HAMISA Happy birthday Hemedi Hemedy Suleiman HOTUBA YA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE Hoyce Temu Huddah Monroe HUSINA IRENE PAUL Irene Uyoya ISABELLA J film 4 life Jack Chuz JACK PATRICK Jacob Steven ‘JB’ Jacqueline Dustan JACQUELINE WOLPER Jaji Khamis 'Kashi' Jay Dee JENNIFER KYAKA (ODAMA) JIDE JINI KABULA JK JO Johari Jokate Mwigelo ‘Kidot’. JOTI Joyce Kiria Joyce Kiwia JUX K-LYNN KADINDA kaja Kajala Masanja Kapotive Star Singers KATUNI Kemmy Kero Zetu KHADIJA OMAR KOPA KIKWETUKWETU KILI MUSIC AWARDS KOLETA Lady Jay Dee Lady Jaydee Lake Oil LAVEDA Linah Sanga Linex Lisa Jensen Loveness Diva Lucy Francis Komba Lulu M2 The P MABILIONEA Madam Rita MADELA Magazeti Mahusiano Maimartha Jesse MAINDA MAISHA Makala Malkia Elizabeth MAMTEI MANDELA MARIAM ISMAIL Masanja Mkandamizaji Mashindano ya Miss Tanzania Matangazo Matonya MaxMalipo MAYA MELLIS EDWARD MENINAH MGOSI MKOLONI Mh Halima Mdee mic Michezo MILLEN HAPPINESS MAGESE MISS CHANG'OMBE MISS DAR CITY CENTER Miss East Africa MISS REDD'S IRINGA 2013 MISS TANGA 2013. MISS TANZANIA 2014 Miss Tanzania mwaka 2011 MISS TEMEKE 2014 MISS USTAWI MISS UTALII TANZANIA 2012/13 Miss vyuo vikuu 2013 MKALA MREMBO HUDDAH Mrisho Mpoto Mrisho Ngassa MSHINDI WA REDD'S MISS LAKE ZONE 2013 NI LUCY CHARLES. MSHINDI WA TAJI LA REDDS MISS KANDA YA KATI 2013 Mtitu muziki Mwana FA MWANAMKE BORA WA MWAKA 2013/14 Mzee Majuto Nancy Sumari Nani Mtani Jembe? NAPE Nassoro ‘Nora’ Natasha Nay wa Mitego Necta Nelly Kamwelu NEY WA MITEGO Nisha NSSF;Zantel Nyamwela NYimbo Nyota yako OBAMA TANZANIA OMMY DIMPOZ P FUNK PAM D Peniel Mgilwa ‘Penny’ PETIT MAN Profesa Jay Q - CHILA Q Boy Q Chilla QUEEN DARLEEN RACHEL NDAUKA RAIS KIKWETE Rais Kikwete. Rasimu Ya Katiba TZ Ray Ray C REDD'S MISS KAGERA 2013 REDD'S MISS TZ Redd’s Miss IFM REDDS MISS TANZANIA 2014 Redds Miss wa Mikoa REHEMA FABIAN RICHIE RICHIE Rihanna ROSE MUHANDO Rose Ndauka Ruge Mutahaba. SABASABA 2013 Saida Karoli Saikolojia Sajeti SAJUKI Sandra SHAA Shamsa Ford Sheikh Ponda Shilole Sintah Siwema Skin Tricks Snura Mushi Spika Makinda staa Staa Wetu Stella Mwangi STYLE ZA NYWELE Taifa Stars Tamasha la matumaini TAMASHA LA SERENGETI FIESTA 2013 Tangazo TANZANIA TEGO TENGENEZA WEBSITE NA BLOG TID Tundaman Tupo wangapi? TUZO ZA MWANAMKE BORA WA MWAKA 2013/14 Twanga Pepeta USA PAGEANT 2014‏ VAI Wastara WEMA WEMA SEPETU Yanga Yanga Bingwa 2013 YOUNG D Yvonne Cherry ‘Monalisa’ Z Anton. Zari Zito kabwe

Translate