Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda akizungumza na vijana wahitimu wa vyuo waliohudhuria mkutano huo.
Makonda akionesha msisitizo wa jambo. Vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali wanaoishi wilaya ya Kinondoni wakifuatilia mkutano huo.
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda, jana amekutana na vijana wahitimu wa sekondari na vyuo mbalimbali wanaoishi katika wilaya yake na kujadili nao jinsi ya kutatua tatizo la ajira.
Katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam, mamia ya vijana walijitokeza kumsikiliza alipozungumza kuhusu changamoto na namna ya upatikanaji wa ajiri.Aliwataka vijana waliojitokeza kujiunda katika makundi matano na kila moja kubuni mradi (project) ambao watauandika wakielezea unavyoweza kutekelezwa na baadaye wauwasilishe ofisini kwake kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Alisema vijana wengi hawana fikra za kujitolea wala kujiajiri mara baada ya kumaliza vyuo, badala yake akili zao huwa ni kuajiriwa moja kwa moja serikalini, kitu ambacho aliwaasa kubadili mfumo katika suala hilo la ajira.
“Vijana wengi wanafikiria mshahara, wakimaliza tu chuo wanafikiria kuajiriwa na kulipwa mishahara mikubwa, nchi yetu haina tatizo la ajira, bali ni fikra finyu za vijana wanaofikiria maisha mazuri kwa haraka,” alisema Makonda na kuwataka vijana hao kujenga moyo pia wa kujitolea.
Aliwataka vijana wote waliohudhuria mkutano huo, kuandika barua za kuomba kujitolea katika kampuni na taasisi mbalimbali na yeye atawadhamini, ili mradi tu waombaji hao wajue sifa na vigezo vya ofisi anayoomba.
“Hakikisheni vijana mnapokuwa mmepata kazi, lindeni heshima za majina yenu kwani msipofanya hivyo mtasababisha heshima na taaluma zenu zinapotea bure, mhakikishe mnazingatia sheria zinazotolewa na sekta mliyopo” alisema Makonda.
(NA DENIS MTIMA/GPL)
No comments:
Post a Comment