Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, vimepata kigugumizi na kutupiana mpira kuhusiana na ufafanuzi juu ya madai kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, anakiuka sheria na kanuni za uchaguzi mkuu kwa kuanza kampeni kabla ya wakati.
Dk. Magufuli amekuwa katika ziara kwenye maeneo mbalimbali nchini katika kile ambacho chama chake kinaeleza kuwa ni kumtambulisha kwa wananchi baada ya kuibuka mshindi katika mchakato mkali wa kumpata mgombea urais wa CCM uliohusisha makada 38 kitendo kinacholalamikiwa na baadhi ya wapinzani kwa madai kuwa huko ni kuanza kampeni kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanjyika Oktoba 25, mwaka huu.
Baada ya kuteuliwa kwake, Magufuli ameshafanya mikutano ya hadhara ya kujitambulisha katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Shinyanga, Morogoro, visiwani Zanzibar na pia mkoani Pwani na mara kadhaa amesikika akiahidi mambo mazuri kwa Watanzania, huku ahadi yake kubwa kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine ikiwa ni "Sitawaangusha".
Katika kufahamu kama kinachofanywa na mgombea huyo kipo ndani ya kanuni na sheria ya uchaguzi, NIPASHE iliwasiliana na viongozi wa Nec na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa nyakati tofauti, ambao walitoa maelezo ya kutupiana mpira.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva, alipoulizwa kama kinachofanywa na mgombea urais huyo CCM ni sahihi, alisema mikutano inayofanywa na Dk. Magufuli ni ya ndani ya chama, hivyo tume hiyo haina mamlaka ya kuingilia.
Lubuva alisema NEC itaanza kuzifuata sheria na kanuni za uchaguzi Agosti 21 baada ya tume hiyo kupitisha rasmi uteuzi wa wagombea wa vyama vyote kufanyika.
“Kinachofanywa na mgombea urais wa CCM ni suala ambalo lipo ndani ya chama chao, kama tume hatuwezi kuingilia ni mambo ya ndani ya chama, uteuzi ukifanyika ndipo tume itaanza kuangalia kama kanuni na sheria zinafuatwa na wagombea, wa kuwauliza kwa sasa ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.
Wakati Nec wakitoa maelezo hayo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sixtus Nyahoza, alisema suala la wagombea na kampeni siyo kazi ya ofisi yake bali ni Nec.
“Kwa upande wetu tunaona anayepaswa kulielezea suala la kama mgombea urais CCM anakiuka sheria ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi sababu wao ndio wanahusika na masuala ya kampeni na wagombea,” alisema.
Nyahoza alisema ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inachofahamu ni kwamba kama kuna mambo yanafanyika ndani ya chama kama vile kuitisha mkutano wa hadhara, wanachotakiwa ni kutoa taarifa polisi na hivyo suala hilo lipo chini ya ofisi hiyo.
“Sheria ya uchaguzi inasema ukitaka kufanya mkutano unatoa taarifa polisi. CCM wamekuwa wakifanya hivyo na hata Chadema wanafanya hivyo na hivi majuzi waliitisha (Chadema) mkutano Mwanza,” alisema.
SHERIA YA UCHAGUZI
Licha ya kuwapo kwa maelezo hayo ya Nec na Msajili wa Vyama vya Siasa, NIPASHE inatambua kuwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, Nec imepewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi kupitia vifungu vya 35B(1), (3) (a), 37 (1) (a) na 46 (1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ambayo inabainisha kuwapo kwa ratiba ya uchaguzi ikiwamo kuanza kwa kampeni. Aidha, msajili wa vyama huhusika pia na masuala ya uchaguzi kupitia Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment