27th July 2015
B-pepe
Chapa
Hatimaye mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umefikia ukingoni na sasa jina la mgombea huyo linatarajiwa kuwekwa hadharani wakati wowote kuanzia sasa.
Taarifa kutoka chanzo kimoja miongoni mwa vigogo wa Ukawa ziliiambia NIPASHE jana kuwa, kazi kubwa ya uteuzi wa jina hilo iliyohusisha wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa imeshakamilika na kwamba kilichokuwa kikisubiriwa kabla ya kutangazwa kwa jina la mgombea ni maridhiano ya ndani ya vyama; kazi ambayo pia ilikamilika mwishoni mwa wiki. Ukawa unaundwa na muungano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
"Watanzania wanaopenda mabadiliko hawana sababu ya kuwa na hofu. Wakati wowote kuanzia leo (jana) jina la mgombea wetu tutaliweka hadharani na baada ya hapo tutaendelea na maandalizi yetu kabambe kuhakikisha kuwa tunahitimisha utawala wa CCM," chanzo hicho kiliiambia NIPASHE jana kwa sharti la kutotajwa. Uhakika wa kuelekea ukingoni mwa maridhiano kuhusu jina la mgombea wa Ukawa umetokana pia na kile kinachodaiwa kutokea kwenye kikao cha Baraza Kuu la CUF kilichofanyika juzi visiwani Zanzibar na pia kikao cha Kamati Kuu Maalum ya Chadema kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Inaelezwa kuwa wakuu wa CUF wamekwishajadili kwa kina suala la Ukawa na kimsingi wameridhia maamuzi kadhaa yatakayoupa nguvu umoja huo, huku Chadema kupitia kikao chake cha jana ikiridhia pia jina la mgombea kupitia majadiliano yao yaliyohusisha ajenda mbili kuu, ambazo ni maandalizi ya uchaguzi na taarifa za mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani unaoendelea nchini kote. Aidha, imeelezwa kuwa kilichobaki hivi sasa ni masuala madogo ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi kupitia vikao mbalimbali vinavyoendelea miongoni mwa vyama vinavyounda Ukawa kabla ya kumtangaza mgombea huyo.
Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote kutoka miongoni mwa vyama vinavyounda Ukawa aliyepatikana kuzungumzia rasmi suala hilo.
MKUTANO UKAWA NA WAHARIRI
Jana, Ukawa waliitisha mkutano maalum na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, ilitarajiwa kuwa wangeeleza juu ya mchakato wao wa kumtangaza mgombea wa nafasi ya urais. Hata hivyo, mkutano huo uliahirishwa na haikuelezwa ni lini utafanyika tena.
KUKOMBA VIGOGO CCM
Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa Ukawa bado wako katika majadiliano na baadhi ya makada maarufu wa CCM wanaotarajiwa kuhamia upinzani kwa makundi na hivyo kuupa nguvu zaidi umoja wao.
"Suala hili la kumtangaza mgombea limefikia mahala pazuri. Ila kuna majadiliano zaidi yanaendelea kuhusiana na uwezekano wa kuvuta vigogo zaidi kutoka ndani ya CCM," chanzo kingine kiliiambia NIPASHE.
Wiki iliyopita, wabunge waliokuwa makada muhimu wa CCM, Esther Bulaya (Viti Maalum) na James Lembeli wa Jimbo la Kahama walihamia Chadema na kutambulishwa ramsi kwenye mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya watu jijini Mwanza.
"Kile kilichoonekana Mwanza kwa kina Bulaya na Lembeli ni rasharasha tu... kuna vigogo zaidi wako mbioni kuhamia upinzani na hili linachangia kwa kiasi fulani kutangazwa kwa jina la mgombea wa Ukawa," chanzo hicho kilieleza.
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ni miongoni mwa vigogo wa CCM wanaotajwa zaidi kupitia mijadala mbalimbali ya kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni miongoni mwa vigogo watakaohamia Ukawa.
Wakati CCM ikikamilisha mchakato wa kumpata mgombea wake na kumtangaza John Magufuli kupeperusha bendera yao katika uchaguzi mkuu tangu Julai 12, Ukawa wameendelea kuwa na kibarua kigumu cha kukamilisha kazi hiyo.
Awali ilidaiwa kuwa Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD walishafikia hatua nzuri lakini wakalazimika kuwasubiri wenzao wa CUF ili nao waridhie kupitia kikao chao cha Baraza Kuu kilichofanyika juzi visiwani Zanzibar.
Uchaguzi Mkuu nchini unatarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu ili kumpata rais wa awamu ya tano atakayemrithi Rais Jakaya Kikwete aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment