Mchezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Lionel Messi.
MONACO, Ufaransa LIONEL Messi ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumpiku Cristiano Ronaldo katika tuzo zilizotolewa jana ambazo pia dunia ilishuhudia Manchester United ikirejea kwenye michuano hiyo hatua ya makundi. Messi, staa wa Barcelona, aliingia hatua ya fainali ya tuzo hizo pamoja na straika wa timu yake, Luis Suarez pamoja na Ronaldo wa Real Madrid, ambapo waandishi wa habari wa michezo ndiyo waliompigia kura.
Upande wa Man United ambao ni mabingwa wa michuano hiyo mwaka 2008, wamepangwa katika kundi ambalo linaonekana kuwa jepesi kwao ambapo wapo Kundi B wakiwa pamoja na PSV Eindhoven ya Uholanzi, CSKA Moscow (Urusi) na Wolfsburg (Ujerumani).
Lionel Messi (kushoto)akipokea tuzo ya mchezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka kwa Michel Platini (kulia) na Cristiano Ronaldo akiwa kwa nyuma.
Vijana wa Kocha Arsene Wenger, Arsenal, wamepangwa Kundi F wakiwa pamoja na vigogo wenzao, Bayern Munich ya Ujerumani pamoja na Olympiacos (Ugiriki) na Dinamo Zagreb (Croatia). Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho atakutana na timu yake ya zamani ya FC Porto katika Kundi G, ambapo wapo pamoja na timu za Dynamo Kyiv na Maccabi Tel Aviv. Ratiba kamili na jinsi makundi yalivyopangwa soma ukurasa wa 24.
No comments:
Post a Comment