Mfanyabiashara maarufu, Mohamed Majid Seif akitaharuki.
Boniphace ngumije
Mkopo noma! Mfanyabiashara maarufu, Mohamed Majid Seif, mkazi wa Mikocheni A, Kinondoni jijini Dar, ametolewa vitu ndani ya nyumba yake namba A35/210 baada ya kushindwa kulipa mkopo wa Sh. Milioni 210 aliouchukua kwenye Benki ya Boa (Bank Of Africa) mwaka 2011.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, katika tukio hilo lililojiri nyumbani hapo, Seif alikopa kiasi hicho cha fedha akiwa na wenzake, lakini baada ya kushindwa kulipa kwa muda wa miaka miwili kama makubaliano yalivyoonesha, wenzake waliingia mitini na kumuachia msala.
Vyombo vikipakizwa kwenye gari.
Ilidaiwa kwamba, baada ya Seif kuachiwa msala huo, aliiomba Boa kumuongezea muda ili aweze ‘kuklia’ deni hilo lakini benki haikuwa tayari kutokana na makubaliano waliyoweka Aprili 18, 2011 kuwa zikizidi siku sitini (60) kwenye muda wa makubaliano ya mkopo, bila kulipwa kwa fedha hizo pamoja na riba nyumba iuzwe.
“Baada ya makubaliano kushindikana, benki hiyo ilitangaza kuipiga mnada nyumba hiyo kupitia magazeti ya kila siku ambapo siku ya mnada, ilinunuliwa na Mwanaiba Mohamed Mzee, mkazi wa hapohapo Mikocheni kwa Sh. Milioni 56,” kilisema chanzo hicho.
‘Ubuyu’ uliendelea kudondoshwa kuwa, Seif hakuridhishwa na uamuzi huo uliochukuliwa na benki hiyo, jambo lililomfanya kukimbilia kwenye Mahakama ya Ardhi na Makazi, Kinondoni kuomba kutenguliwa kwa mnada huo.
Ilisemekana kwamba, Seif aliiomba mahakama hiyo kupewa muda zaidi ili alipe deni, lakini baada ya shauri lake kusikilizwa inadaiwa mahakama ilitoa ridhaa ya taratibu za kibenki kuendelea huku baadaye ikiipa kazi kampuni ya mawakili ya Rimina Auction Mart kumuondoa kwa nguvu kwenye nyumba hiyo.
Ilielezwa kwamba, ilipofika Agosti 19, mwaka huu ndipo Kampuni ya Rimina walipofika nyumbani hapo na kutupa vitu vyote nje bila kumuuliza mtu yeyote yule na kuikabidhi nyumba kwa mwenyewe (aliyeinunua) kupitia muwakilishi wake.
Barua ya makabidhiano.
Wakati akitolewa vitu nje, mfanyabiashara huyo hakuwepo eneo la tukio, alipotonywa kilichokuwa kinaendelea nyumbani kwake, aliibuka na kutaka kuleta utata lakini tayari mwenye nyumba alikuwa ameshakabidhiwa mali yake huku jamaa huyo na mkewe wakitafuta hifadhi mpya.
No comments:
Post a Comment