Mahakama yaamuru Kafulila akamatwe mara moja
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mbunge wa Kigoma Kusini aliyemaliza muda wake, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), baada ya kushindwa kuhudhuria mahakamani kwa ajili ya kesi yake inayomkabili mahakamani hapo.
Kafulila anakabiliwa na shitaka la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Khadija Nyembo, kwa kumwambia hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho kingeashiria uvunjifu wa amani.
Hakimu wa Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sylvester Kainda, alitoa hati hiyo jana baada ya upande wa mashitaka kuomba hati ya kumkamata mshtakiwa kwa kutohudhuria mahakamani pamoja na wakili wake, Daniel Rumenyela.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Shabani Masanja, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na mshtakiwa.
Masanja aliiomba mahakama hiyo kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa pamoja na hati ya kuwaita wadhamini wake.
Kutokana na hali hiyo, Masanja aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu Kainda alikubaliana na ombi hilo na kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa pamoja na ya kuwaita wadhamini wake.
Aidha, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, mwaka huu mshtakiwa atakaposomewa mshtakiwa maelezo ya awali.
Awali, mshtakiwa huyo aliposomewa shitaka lake alikana kutenda kosa hilo na yuko nje kwa dhamana ya mdhamini mmoja na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni mbili.
Mapema, akisoma hati ya mashitaka, Masanja alidai kuwa Agosti mosi, mwaka 2013, katika kata ya Nguruka eneo la Rest House Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwa Nyembo kuwa hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho kingeashiria uvunjifu wa amani.
Kafulila alipotafutwa na Nipashe kuhusiana na amri hiyo ya mahakama, alisema kuwa hakwenda kortini kutokana na wakili wake kutompa taarifa za kuwapo shauri hilo kwa siku ya jana.
Aidha, Kafulia alisema alikuwa akimtafuta wakili huyo ili amweleze sababu za kutompatia taarifa hiyo.
Chanzo: Nipashe
Last edited by tpaul; Today at 10:29.
No comments:
Post a Comment