Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
UKIWEKA mguu watu wanaweka kichwa, saa chache baada ya Yanga kumleta kiungo Thabani Kamusoko, Simba imewaleta kipa Ricardo Andrade na straika Makan Dembele kutoka Brazil na Mali.
Kipa Andrade alitarajiwa kuwasili leo alfariji kutoka Brazil na straika Dembele atawasili kesho Jumapili kutoka Mali.
Andrade, 38, ambaye jina lake halisi ni Ricardo Ribeiro de Andrade, mara ya mwisho aliichezea Klabu ya Moreirense ya Ureno lakini mwenye ni Mbrazili aliyezaliwa katika Jiji la Rio de Janeiro.
Kipa huyo mwenye uzito wa Kilogramu 79, katika klabu yake alikuwa anavaa jezi namba 25 na ana nguvu nyingi za kuzuia mipira kwa kutumia mguu wa kulia pia ana urefu wa futi sita na inchi mbili.
Moja ya sifa zake ni uwezo mkubwa wa kucheza krosi na mipira ya karibu kuelekea langoni kwake.
Kwa upande wake, straika Dembele aliyezaliwa Desemba 25, 1986, anatokea Klabu ya JS Kabylie ya Algeria na sifa yake kubwa ni kufunga kwani ameifungia timu yake mabao tisa katika mechi 16.
Dembele aliyezaliwa Bamako, Mali anavaa jezi namba tisa na ana urefu wa futi sita na inchi tatu. Straika huyu amewahi kuichezea Raja De Casablanca ya Morocco kati ya mwaka 2007 hadi 2008 na kufunga mabao manane katika mechi 14.
Simba imeshamalizana kimaslahi na kipa wake, Ivo Mapunda japokuwa bado hajasaini mkataba kwani hayupo kikosini kwa maelezo kuwa ni majeruhi.
Kwa mujibu wa Rais wa Simba, Evans Aveva, kipa na straika huyo watawasili lakini kabla ya kupewa mkataba, Kocha Dylan Kerr na Kocha wa Makipa, Idd Salim watapima uwezo wa kila mmoja wao.
“Bado tunaendelea na zoezi la usajili ili kuhakikisha kikosi chetu kinakuwa bora zaidi kwa ajili ya kukabiliana na timu nyingine, kuna kipa anakuja kesho (leo) alfajiri kutoka Brazil. Pia kuna straika anaitwa Dembele atakuja kesho (leo) usiku kutoka Mali.
“Kipa huyu tumekuwa tukimfuatilia kwa muda mrefu na sisi viongozi tumeona anatufaa lakini makocha nao lazima wajiridhishe,” alisema Aveva.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza Aveva alisema kipa huyo atatambulishwa leo Jumamosi kwa mashabiki wa Simba katika Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kuhusu usajili wa Mapunda, Aveva alisema: “Huyo ni mchezaji wetu jamani sema kwa sasa ni majeruhi tu.”
No comments:
Post a Comment