SHUGHULI za utoaji tiba katika Hospitali ya mkoa wa Singida zimezorota kutokana na kuibuka kwa utata wa matumizi ya shuka za wagonjwa ambapo wagonjwa wanaolazwa kutumia mashuka wanayoyatoa majumbani kwao na kujifunika bila kuyafanyia usafi suala ambalo ni kinyume na taratibu na kanuni za afya.
Tangu ilipoanza kutoa huduma hospitali hiyo na tangu kuanzishwa kwake ilikuwa mkombozi wa huduma za afya kwa wananchi wa Wilaya zote za mkoa huo na zile zinazozunguka mkoa huo kwa upande wa Singida Kaskazini na Mashariki ambapo wananchi wake kwa sasa wanalazimika kufuata huduma hiyo umbali mrefu, ikiwemo katika Hospitali ya mkoa wa Dodoma au kutumia Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspa iliyopo Itigi.
Wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo wanaelezwa kuwa hatarini kupata maambukizi ya magonjwa mengine kutokana na kutumia mashuka hayo na uhaba wa magodoro.
Mtaalamu mmoja wa afya hospitalini hapo (jina linahifadhiwa) anasema wanajikuta katika mateso makubwa kutokana na kile alichokieleza kuwa ni uzembe wa dhahiri wa Serikali na wataalamu wenzake kwa kukubali hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma tangu awali badala ya kuifunga ili Serikali itoe mashuka na huduma nyingine zinazohitajika.
Muuguzi huyo amebainisha kuwa hata hivyo kwa muda mrefu Hospitali hiyo imejikuta katika msuguano wa chini kwa chini na Ofisi ya Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ambayo ilikuwa inataka vifaa hivyo viombwe kwa watu na mashirika mbalimbali ili vipelekwe kabla ya mwezi wa Aprili, 2015 na kuwa chini ya usimamizi na uangalizi wao lakini hadi sasa hakuna jitihada za kuridhisha zinazofanywa ili kutatua tatizo hilo.
Aidha, amesema hali hiyo inatokana na hospitali hiyo kuwa na mashuka 230 pekee kati ya 2,500 yanayohitajika, kiwango ambacho ni chini ya mahitaji hivyo kuulazimu uongozi kutoa ruksa kwa kila mgonjwa anayelazwa kwenda na shuka lake licha ya kuwa hakuna kanuni za kusimamia mashuka hayo.
Kutokana na sakata hilo, baadhi ya wagonjwa mbalimbali wanaotibiwa katika hospitali hiyo ya mkoa akiwemo Frida James (49), ambao ni wagonjwa wa kawaida na wale waliopatiwa rufaa kutoka kwenye Vituo vya Afya Vijijini, Zahanati pamoja na maeneo mengine jirani na nje ya mkoa huo wa Singida amesema baada ya kutumia mashuka hayo yanafuliwa na ndugu zao.
Ameeleza kuwa wakipata ahueni na kuruhusiwa kwenda makwao, baadhi yao wanaacha mashuka hayo hospitalini kwa kuhofia usalama wa afya zao na wengine huondoka nayo.
Mmoja wa wananchi mkoani humo aliyejitambulisha kwa jina moja la Juma, akizungumzia tatizo hilo alieleza kuwa hatua ya kukosekana kwa huduma muhimu ikiwemo ya malazi ni kuwavunja moyo wagonjwa walioandikiwa rufaa ya kutibiwa katika hospitali hiyo na wengine wanaohitaji matibabu.
Naye kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Daniel Tarimo, ameieleza FikraPevu kwamba licha ya jukumu la kuokoa maisha ya wagonjwa, lakini kuna hatari inayotokana na uhaba mkubwa wa mashuka kwa kipindi cha muda usiopungua miezi minne.
Mbali na kukiri hospitali hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali amesema yeye kama mtaalamu wa afya, wanaotambua kuwa hali hiyo ni hatari kwa wagonjwa wanaotumia mashuka ya nyumbani, huku akiongeza kuwa uongozi wa hospitali haina njia nyingine ya kutatua tatizo hilo wakati wakisubiri kupatiwa msaada na Serikali ili kukubalina na hali halisi.
Hata hivyo, amesema hospitali hiyo pia inakabiliwa na tatizo la uhaba wa magodoro kwa zaidi ya asilimia 75 kwani yaliyopo ni 36 tu kati ya magodoro 230 yanayotakiwa ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo.
Kwa muda mrefu hospitali za Serikali nchini zikiwemo zile za Rufaa, zimekuwa zikilalamikiwa na wadau mbalimbali kuwa hatua ya kukosa huduma muhimu ikiwemo ufinyu wa bajeti, kukosekana kwa vyumba vya kuhifadhia maiti vyenye majokofu (Nyingine hazina), ukosefu wa dawa na mengineyo ni moja ya changamoto kubwa inayopigiwa kelele na Watanzania kila kukicha.
Taarifa zinaonyesha kwamba, ukosefu wa huduma hizo hupelekea wananchi kujiingiza katika kundi la ununuaji holela wa dawa katika maduka maalumu yanayouza dawa hizo na kudidimiza Aaya zao.
Mara nyingi matumizi ya dawa muhimu zijulikanazo kama vijiuasumu au ‘antibayotiki’ zinazopatikana kwenye maduka ya dawa muhimu lakini zisipotumiwa ipasavyo, vinadhuru afya ya mgonjwa kutokana na mazoea ya kutumia dawa pasipokuwa na cheti cha mtibabu kutoka kwa daktari. Uuzaji wa dawa za binadamu kwa njia hiyo unatajwa kama njia moja wapo ya wafamasia kujipatia kipato.
Awali, gazeti hili mtandao la FikraPevu mwezi Februari, 2015 liliripoti taarifa iliyohusu hatua ya kuchelewa kutekelezwa kwa mpango wa Serikali unaotaka dawa zote zinazonunuliwa na kusambazwa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kuwekwa lebo ya utambuzi kwa lengo la kudhibiti wizi wa dawa hizo unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu, na jinsi unavyoneemesha wamiliki wa maduka ya dawa nchini pamoja na kusababisha wananchi kuendelea kukosa huduma katika hospitali za umma.
CHANZO; FIKRA PEVU