Baraza Kuu la Waislamu nchini umemchagua aliyekuwa Kaimu Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi Bin Ali, kuwa Sheikh Mkuu wa Tanzania.
Sheikh Zuberi amepita bila kupingwa baada ya mpinzani wake Sheikh Ally Muhidin Mkoyogole kuamua kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Alhaji Ndassiwa amesema majina mawili yaliyotoka kwenye Baraza la Ulamaa yalikuwa ni ya Sheikh Ally Muhidini Mkoyogole na Sheikh Zubeiri.
Mara baada ya uchaguzi huo Sheikh Zuberi mbali na kuwashukuru washiriki wa mkutano huo, amewataka Watanzania kumtanguliza Mungu ili awapatie kiongozi bora katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Sheikh Zuberi, ameyasema leo Mjini Dodoma, kwenye mkutano mkuu wa Bwata uliompitisha kuwa Mufti Mkuu wa Tanzania kwa kura za wajumbe wote 310 baada ya mtu aliyeingia naye katika ushindani huo kujitoa.
Katika hotuba yake Mufti Zuberi, amewataka Watanzania kumuomba Mungu ili ailinde nchi katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaowashirikisha madiwani, wabunge na urais. Amewataka Waislamu kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu.
Amewaagiza Masheikh wote wa Mikoa, Wilaya na Kata kuomba dua kwa Mungu, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu 2015, ili Mwenyezi Mungu aendelee kudumisha amani ya nchi.
Katika kinyang’anyiro hicho Sheikh Zuberi, alikuwa na wenzake watatu ambaye ni Sheikh Hamis Mtupa, Sheikh Hassan Kiburwa kutoka mkoa wa Kigoma na Sheikh Ally Mkoyogole kutoka Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban amesema mkutano huo umemalizika kwa amani na kwamba wajumbe wamempitisha kwa kauli moja sheikh Zuneri kuwa Sheikh Mkuu.
Wajumbe wa mkutano huo ni masheikh wote wa mikoa na wilaya ambao wanaunda Tume ya Dini, wenyeviti wote wa halmashauri za mikoa pamoja na makatibu wao na wenyeviti wote wa wilaya nchini pamoja na makatibu wao.
Aidha, wajumbe wengine ni wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Baraza la Ulamaa na wajumbe wa Halmashauri Kuu.
No comments:
Post a Comment