Wakati kampeni za mgombea urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupitia Chadema zikiingia siku ya sita, chama hicho kimetangaza kuanza kampeni zake kwa kutumia helikopta (chopa) nne ambazo zitatikisa anga katika mikoa yote nchini kuomba ridhaa ya wananchi kukichagua katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, akiwahutubia maelfu ya wananchi, alisema kwa sababu Chadema imejipanga kushinda uchaguzi na usalama ni kazi ambayo ni ya wote.
Alisema Tanzania nzima kuna majimbo ya uchaguzi 265 ambako Zanzibar yako 50 na Tanzania Bara 215.
Aliongeza kuwa siku za kampeni ni siku 60 mgombea urais Ukawa hawezi kufikia majimbo yote hivyo Chadema imeunda vikosi vinne vya askari wa mapambano ambavyo vitaundwa na wabunge makini na baadhi ya viongozi ambao watafanya kampeni nchi nzima kwa kutumia helikopta nne.
Aliwataja wabunge hao watakaounda kikosi hicho wanaomaliza muda wao kuwa ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Ezekiel Wenje (Nyamagana), David Silinde (Momba), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mbeya Mjini), John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe) na yeye (Mbowe) ambaye ni wa Hai.
“Vikosi hivi vitachana nchi nzima kwa kutumia helikopta kuanzia wiki ijayo, hivyo majimbo ambayo mgombea urais hatafika vikosi vitafika na maeneo mengine atakwenda mgombea mwenza,”alisema.
Mbowe alisema CCM wameshakuwa laini kama maini hivyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni lazima wataondoka madarakani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment