MWANAZUONI aliyebobea katika sheria, Profesa Issa Shivji na Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla wamekosoa
hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni, Mbunge wa Arusha
Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa Lema, Method Kimomogoro amepinga madai hayo akisema wanaoipinga pengine hawajapata nafasi ya kuliangalia kwa undani suala la haki ya mpiga kura kupinga matokeo mahakamani.
Profesa Shivji kwa upande wake alieleza kushangazwa na maelezo ya Mahakama ya Rufani kuwa mpiga kura hana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi na kusema hiyo ni sawa na kutunga sheria mpya na si kutafsiri zilizopo.
Alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi, Katiba ya nchi na Mahakama, vinampa haki mpiga kura kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi.
“Sheria ya Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja (Chediel ya mwaka 1980), vinampa haki mpiga kura kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Sijaona hoja nzito ya Mahakama ya kufuta haki hiyo ya mpiga kura,” alisema Profesa Shivji.
Katika shauri hilo namba 84 la mwaka 1980 lililofunguliwa na William Bakari na mwenzake dhidi ya Mgonja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mahakama Kuu Tanzania iliamua kuwa, mpiga kura ana haki kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Walalamikaji walishinda.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika kesi ya Lema, iliamua kwamba hukumu katika kesi ya Mgonja ilikosewa kwani si sahihi kwamba mtu yeyote bila kujali mahali alipojiandikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo katika jimbo lolote nchini hata kama haki zake hazijakiukwa kwa namna yoyote.
Lakini Profesa Shivji aliitetea hukumu hiyo ya Mgonja akisema imekuwapo kwa zaidi ya miaka 30 sasa na kwamba kwa muda wote huo imekuwa ikifuatwa katika uamuzi wa mashauri mbalimbali, huku akisisitiza kuwa Mahakama haiwezi kuifuta kirahisi tu.
Profesa Shivji alisema mpiga kura ni mwananchi na kwa vyovyote ana masilahi katika uchaguzi husika na hivyo anatarajia kuona uchaguzi ambao ni huru na wa haki.
“Hivyo huwezi kusema hahusiki na nani kashinda au kashindwa kwa kuwa uchaguzi ni muhimu katika kujenga na kukuza demokrasia,” alisema Profesa Shivji.
Chama cha Wanasheria
Kwa upande wake, Stolla alisema: “Nimesikiliza hata maoni ya wanasheria mbalimbali wakizungumzia kutofurahishwa na tafsiri ya Mahakama ya Rufani kuhusu haki ya mpiga kura ‘ku-challenge’ (kupinga) matokeo ya uchaguzi mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Katika uamuzi wa kisheria, inaonekana Mahakama imetunga sheria mpya na wengi tunajiuliza kama siyo, sababu ya kuwa mpiga kura ni ipi nyingine inampa haki mpiga kura kupinga matokeo?”
Stolla alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi ya tangu mwaka 1985, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, kabla ya kutungwa upya mwaka 2005, inampa haki mpiga kura kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
“Mwaka 2002, sheria zote zilifanyiwa marekebisho na baadaye mwaka 2005, Bunge likatunga sheria mpya inayoitwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ikafuta ya mwaka 1985. Sheria hiyo na marekebisho yake, ndiyo inayotawala uchaguzi hadi sasa,” alisema.
Alisema hata kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo ya Uchaguzi ya mwaka 1985, tayari kulikuwa na uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja ambayo iliamua kuwa mpiga kura ana haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
“Uamuzi wa kesi ya Mgonja ulikuja ‘ku-reflect’ (kuakisi) hata kwenye Sheria ya Bunge ya mwaka 1985. Tangu hukumu hiyo ya Mgonja hakuna uamuzi mwingine wa Mahakama ambao umeshautengua huo, ndiyo maana hata wanasheria wanashangaa uamuzi huu wa Mahakama ya Rufani,” alisema.
Alisema kumekuwa na kesi nyingi mahakamani za wapiga kura kupinga matokeo na kwamba nyingine hata yeye amezisimamia na hakuna wakati ambao Mahakama imewahi kusema kuwa hawana haki hiyo.
Alitoa mfano wa kesi iliyofunguliwa na wapiga kura dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Mbulu, Phillip Marmo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Alisema kesi hiyo ilishindwa kuendelea kutokana na wapiga kura hao kushindwa kuweka mahakamani fedha ya amana kwa ajili ya kuiendesha na si kwa sababu hawakuwa na haki.
Akizungumzia hoja ya Mahakama ya Rufani kuwa hapakuwa na ushahidi kama walalamikaji walikuwa wapiga kura, Stolla alisema hilo halikuwa na ulazima kwa kuwa halikuwa jambo lililokuwa likibishaniwa.
“Hata hivyo, kabla ya kuanza kesi Mahakama Kuu, Jaji Mujulizi (Aloyce) aliitisha vithibitisho ili kujiridhisha kama ni wapiga kura,” alisema Stolla na kuongeza:
“Lakini Mahakama ya Rufani wenyewe walianza kutafuta kama liliibuka Mahakama Kuu na licha ya Mahakama Kuu kuonyesha kuwa ilijiridhisha katika hilo, wao wakakosoa kuwa uthibitisho huo ulipaswa uwe sehemu ya mwenendo.”
Katika uamuzi wake Mahakama ya Rufani ilisema kumbukumbu za Mahakama hazionyeshi iwapo vitambulisho vya wapiga kura viliwasilishwa na kupokewa mahakamani na ikaenda mbali zaidi kwa kutilia shaka jinsi rekodi ya kadi hizo zilivyochukuliwa.
Ilisema kinachoonekana katika kumbukumbu za Mahakama ni kiambatisho na maelezo tu kuwa wajiburufani ni wapiga kura waliosajiliwa na kwamba badala yake wakili wao ndiye aliyejaribu kuthibitisha hilo kwa maelezo, badala ya vielelezo.
Ilisema Wakili wa wajibu rufaa, Alute Mughway aliwasilisha kadi za wateja wake kwa Jaji Aloyce Mujulizi kuthibitisha kuwa walikuwa wapiga kura halali, lakini Mahakama hiyo ikasisitiza kuwa utaratibu huo ni kinyume cha sheria kwa kuwa ushahidi kama huo ulipaswa uwasilishwe moja kwa moja mahakamani na utolewe na wamiliki wa nyaraka husika.
Ilisema hata kama ingethibitika kuwa wajibu rufani walikuwa wapiga kura waliosajiliwa, bado hawakuwa na haki kisheria kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi kwa madai ya mrufani kutumia lugha za matusi kwenye kampeni zake.
Mugway ashangaa
Wakili Alute Mughway aliyekuwa akiwatetea wajibu rufaa katika rufaa hiyo, alisema Mahakama imeacha jukumu lake la kutafsiri sheria na badala yake ikatunga sheria mpya ambayo inapingana na Sheria ya Bunge na Katiba ya nchi, Ibara ya 26 (2).
Alisema Kifungu cha 111 (1) cha Sheria ya Uchaguzi, Hukumu ya kesi ya Mgonja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vinampa haki mpiga kura kufungua shauri mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi.
Alisema kwa mujibu wa kifungu hicho, miongoni mwa watu wanaoweza kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi ni aliyepiga kura au aliyekuwa na haki ya kupiga kura na kwamba tangu wakati huo kifungu hicho hakijawahi kufanyiwa marekebisho.
Wakili wa kujitegemea, Vedasto Audax alikaririwa na gazeti dada la The Citizen akisema: “Swali langu ni kwamba ni lini uamuzi wa kesi ya Mgonja ulionekana kuwa na makosa kisheria? Ni kuanzia leo baada ya Mahakama ya Rufani kutamka kuwa una makosa?”
Wakili wa Lema
Kimomogoro alisema hukumu ya kesi ya Mgonja haijitoleshelezi kwa sababu haikusema ni katika mambo gani mpiga kura ana haki ya kufungua kesi kupinga matokeo mahakamani huku akisema kwa maoni yake, anakuwa na haki pale tu haki zake kama mpiga kura zinapokiukwa.
“Mpiga kura hawezi kuwa na haki sawa na mgombea. Mgombea haki zake ni kubwa kuliko mpiga kura kwa sababu kwanza yeye ni mpiga kura na pili ni mgombea,” alisema na kuongeza:
“Ndiyo maana mpiga kura anaruhusiwa kupiga kura katika kituo kile alichojiandikisha tu lakini mgombea huweza kupiga kura katika kituo chochote.”
Alisema mwananchi wa kawaida tu ambaye hajajiandikisha hata kama akimwona mgombea akitoa rushwa hadharani, hana haki ya kufungua kesi mahakamani, lakini alipoulizwa kwa upande wa mwananchi aliyejiandikisha kupiga kura alisema hakuwa na rejea za sheria kwa kuwa alikuwa Karagwe kwa mapumziko.
Kesi ya Lema
Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, mwaka huu kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake.
Walikuwa wakidai kuwa katika kampeni zake alikuwa akitumia lugha za matusi, kejeli na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Buriani.
Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila ilimtia hatiani kwa kutumia lugha ya matusi na kutengua matokeo yaliyompa ushindi.
Lema alikata rufaa Mahakama ya Rufani kupitia kwa mawakili wake, Kimomogoro na Tundu Lissu ambayo Desemba 21, mwaka huu ilimrejesha tena bungeni baada ya kuikubali.
Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo ilisema kwa kuwa kisheria hayo ni masilahi ya umma kufikishwa mahakamani chini ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba na kwamba mlalamikaji anapaswa kuonyesha haki zake au masilahi ambayo yameingiliwa na athari alizozipata.
“Hivyo mpiga kura hana haki ya kisheria kufungua kesi kuhoji matokeo ya uchaguzi pale ambapo haki zake hazikukiukwa,” ilisema Mahakama ya Rufani.
Ilisema kwa mujibu wa Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Tanzania, raia anakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kwa masilahi ya jamii, kama ilivyotokea katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa SerikaIi ya mwaka 1995.
Ilisema kesi dhidi ya Lema haikufunguliwa chini ya Ibara ya 26 (2) ambayo inampa fursa na haki raia yeyote kufungua shauri mahakamani lenye masilahi ya umma, huku ikisisitiza kuwa madai ya wajibu rufani katika kesi hiyo hayagusi masilahi ya jamii yote.
No comments:
Post a Comment