MWAKA 2012 ndio uko ukingoni, ambapo Jumanne ijayo panapo majaliwa yake Mungu tutaingia katika mwaka mwingine, yaani 2013.
Leo kwa vyanzo na kumbukumbu nyingi za habari za kisanii tutakuletea baadhi ya matukio yaliyotikisa katika mwaka huu.
Katika mwaka wa 2012 wamiliki wengi wa bendi walionekana na kutawaliwa
na mzimu wa kunyakuliana wanamuziki huku kila mmoja akiamini kwamba
hiyo ndiyo ilikuwa njia ya kujipatia jina na kuzoa mashabiki.
Mwanzoni mwa kwaka huu bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta
ilipata mtikisiko mkubwa kwa kunyakuliwa aliyekuwa muimbaji kiraka wa
bendi yake, Charles Gabriel ‘Chalz Baba’ aliyenyakuliwa na bendi ya
Mashujaa.
Kama hiyo haitoshi, pia msanii huyo akiwa na rapa wa bendi ya FM
Academia 33 waliandaliwa usiku maalumu wa utambulisho uliofanyika kwenye
ukumbi wa Business Park, Dar es Salaam.
Charlz Baba alinyakuliwa mara tu baada ya bendi hiyo kutoka katika
ziara yake nchini Uingereza ilikokwenda kwa mwaliko maalumu.
Aliyekuwa mnenguaji tishio na mwenye mvuto katiba bendi ya Twanga
Pepeta, Aisha Mbegu ‘Queen Aisha’, maarufu kama Aisha Madinda alijikuta
akishuka kiwango chake cha uchezaji pindi awapo jukwaani na wakati
akiwa katika matibabu na mipango ya kujiweka sawa ili aweze kurudi tena
jukwaani, akachukuliwa na bendi ya Extra Bongo na baadaye akashindwa
kuendelea na kazi hiyo na sasa inasemekana ameachana na muziki wa dunia
na kuamua kuokoka na kuwa kati ya waumini wa kanisa moja.
Msanii Kalala Hamza Kalala ‘Kalala Junior’ alitangaza kuachana na
muziki na bendi aliyoiasisi ya Mapacha Watatu na kurudi katika bendi
ya Twanga Pepeta na kwa mara ya kwanza akatunga kibao kinachovutia wengi
sasa.
Mashujaa walizidi kuchukua wasanii Twanga Pepeta kwa kumchukua mnenguaji wake, Lilian Internet na Meneja Martin Sospeter.
Extra Bongo nayo haikubaki nyuma wakachukua wanenguaji wawili Maria Soloma, Sabrina Mayonise na muimbaji Khadija Kimobitel.
Mwinjuma Muumini alitimkia bendi ya Victoria akapiga kambi Mtwara na yeye anadaiwa kunyemelea wasanii katika bendi ya Twanga..
Bendi ya Skylight ilizinduliwa kwa makekeke huku katika bendi hii
kukiwa na sura ya baadhi ya wanamuziki walioing’arisha bendi ya Machozi
inayomilikiwa na Judith Wambura ‘Lady Jaydee’.
HABARI ZA UGONJWA
Kwa upande wasanaa ya filamu, ugonjwa wa Juma Kilowoko ‘Sajuki’, wazua jambo, kila kona ni michango.
Wasanii mbalimbali pamoja na viongozi wa kisiasa walijitokeza
kumchangia na kupata fedha za kumpeleka nchini India kwa matibabu,
akatibiwa na kurudi nchini, lakini hivi karibuni alianguka jukwaani
akiwa katika onesho la kuchanga fedha za kumrejesha kwenye matibabu
nchini India.
Jack Wolper alipata mchumba Dallas na kubadilisha dini sasa ni Ilham
ila uchumba huo ulivunjika huku yeye akiahidi kubaki katika imani ya
dini ya Kiislamu kwa kuwwa anaipenda na mama yake ana asili hiyo.
Mchekeshaji wa siku nyingi, Said Ngamba ‘Mzee Small’, alishikwa na
ugonjwa wa kiharusi ghafla akitokea katika kazi jijini Mwanza, hadi sasa
hali yake bado ni mbaya.
Mwanamuziki aliyetikisa kwa miondoko ya kutikisa kiuno na sauti nzuri
na mwenye haiba awapo jukwaani, Rehema Chalamila ‘Ray C’, alijikuta
akipoteza mvuto na mashabiki wake kutokana na ugonjwa ambao haukuwekwa
wazi, hali iliyosababisha kusaidiwa na Rais Jakaya Kikwete hadi afya
yake ilipotengemaa.
Akizungumza katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, Ray C anasema
anamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumsaidia gharama za kutibiwa
ugonjwa wake ambao ulibaki kuwa siri.
Tamasha la Fiesta larindima huku likizinduliwa na msanii mahiri wa Hip Hop kutoka nchini Kenya.
Kwa mara ya kwanza katika tamasha hilo wasanii wa filamu wahusishwa
akiwamo Jacob Steven ‘JB’, Vincent Kigosi ‘Ray’, Wema Sepetu, Aunt
Gwantwa na Steve Nyerere.
Lakini wakiwa katika matamasha kadhaa na kwenye mikoa mbalimbali
wasanii Wema na Aunt walijikuta wakiingia katika kashfa ya kuonesha
sehemu zao nyeti walipokuwa jukwaani.
Kufuatia kadhia hiyo, Shirikisho la Filamu nchini liliwataka waiombe
radhi jamii kwa kuikosea nao wakafanya hivyo katika mkutano uliofanyika
kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Msanii nyota katika filamu nchini Aunt Ezekiel alichumbiwa na kufunga ndoa na Sunday ‘Mzee wa Dubai.’
MAADHIMISHO
Klabu yenye hadhi ya kimataifa nchini, Club Bilicanas ilisherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.
Kampuni kubwa ya burudani nchini ya Clouds FM nayo ilisherehekea
miaka 13 tangu kuanzishwa na kumleta msanii galacha kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Antoine Koffi Olomide na tamasha kubwa
kufanyika kwenye viwanja vya Leaders Club Kinondoni Dar es Salaam.
MAMA SAKINA APIGWA MWELEKA
Wakiwa katika uzinduzi wa albamu ya pili ya bendi hiyo mmiliki wa
bendi ya Mashujaa, Mamaa Sakina, alianguka na kuzirai baada ya kuingia
uwanjani Leaders Club na kukuta uwanja mtupu tofauti na alivyotarajia .
Uzinduzi wa bendi ya Mashujaa wakwama kuzinduliwa kama ilivyopangwa,
huku onesho la mwanamuziki JB Mpiana likidorora na uzinduzi wa albamu
ya bendi yake kushindikana kuzinduliwa kama ilivyopangwa.
MUZIKI WA KIZAZI KIPYA
Shindano la Bongo Star Search lafanyika na kuwaacha wenye vipaji nje
ya wigo. Wadogo wa aliyekuwa mshindi wa 2009, Misoji Nkwabi, watupwa
nje katika dakika za mwisho za shindano.
UDAKU KIDOGO
Uhusiano wa kimapenzi kati ya wasanii nyota Wema na Diamond waota
mbawa, vyombo vya habari vikaripoti Diamond anatoka na aliyekuwa Miss
Tanzania namba 2 Jokate Mwegelo. Lakini hawakudumu katika uhusiano wao.
Uvumi wa kuvunjika kwa ndoa ya msanii Irene Uwoya na mumewe Kataut Ndikumana, wazinguana na baadaye mambo yakawa sawa.
Wasanii wa kike wakanyambuana katika kipindi cha Take One kinachorusha na Zamaradi Mketema.
Irene Uwoya na Wema Sepetu wakamkashifu sana Jacqueline Wolper pamoja na Mama Wema kuingilia kati ugomvi wa mwanaye.
Wema ajitangaza na kujionesha jinsi nyumba yake ilivyo, mwenye nyumba amjia juu kwa kuinadi nyumba yake.
Msanii huyo alilazimika kufanya hivyo kufuatia kukashifiwa na Wolper
kwamba hana pa kulala ndiyo maana ana tabia ya kuhamia kwa mwanaume,
naye si mwingine bali ni Naseeb Abdul Diamond.
WASANII WA KIMATAIFA WALIOTUA BONGO
Msanii Rick Ross alitua nchini kwa ajili ya kunogesha tamasha la Fiesta 2012.
Msanii JB Mpiana alitua nchini akafuatiwa na Koffi Olomide.
Azonto akatua katika Sikukuu ya Krisimasi.
HABARI ZA SIMANZI NA VIFO
Kifo ya Steven Kanumba ‘The Great’ aliyefariki dunia ghafla nyumbani
kwake maeneo ya Vatican Sinza, jijini Dar es Salaam, msiba wake utabaki
kuwa na historia ya kuhudhuriwa na watu wengi waombolezaji waliotoka
mikoani na hata nje ya nchi.
Hadi sasa msanii mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’, anashikiliwa kwa kusababisha kifo hicho.
Msanii John Stephano aliyefariki dunia kwa kutokuwa na umakini wa
ugonjwa wake, alisumbuliwa na kongosho lakini madaktari wa Hospitali ya
Mwananyamala wakampiga picha na kuona kwamba utumbo wake umetoboka,
hivyo wakamfanyia upasuaji uliosababisha mauti yake.
Msanii wa filamu na mchekeshaji, Salum Mkieti ‘Sharo Milionea’
alifariki dunia kwa ajali ya gari alipokuwa akienda nyumbani kwao Tanga.
Aliyekuwa msanii wa kundi la Kaole Mohamed Khalid ‘Mlopelo’ afariki dunia.
Kwa upande wa muziki wa taarabu wapata pigo kwa kuondokewa na
aliyekuwa msanii mwenye mvuto na mashabiki wengi, Mariam Khamis ‘Paka
Mapepe’. Mungu azipumzishe roho za marehemu wote mahali pema peponi.
Amina.Habari hii na Khadija Kalil.
No comments:
Post a Comment