Mkasa
huu unasimuliwa na Padri Moses au kwa kifupi Faza Moze lakini si jina lake
halisi , akiweka bayana mambo aliyoyafanya mpaka kujutia. Padri Moses hakutaka
kuweka wazi ni wa kanisa gani kwani Mapdri hutumiwa na makanisa ya Anglikani na
Romani. Anasema:
“Ilikuwa
mwaka 1999, mwezi Desemba wakati wakristo wanajiandaa kwa sherehe ya Krismasi,
kanisani walikuja wazee wawili ambao ni wageni machoni pangu miongoni mwa waumini
wa kanisa langu hilo .
Walikaa
fomu moja na waumini wengine, lakini katika kukaa walitenganishwa na mzee
mmoja. Nikiwa naendelea na ibada, kila wakati niliwaona wale wazee wageni
wakiangaliana kwa kupitia mgongoni kwa yule mzee aliyewatenganisha.
Kwa
sababu moyo wangu ulikosa amani na wao, nikawa nawakazia macho hatua kwa hatua
ili nione kila walichokuwa wakikifanya.
Kuna
wakati nilishtuka sana kuona mmoja wao akibadilika sura na kuwa kama ya bundi,
lakini nilipojiweka sawa kushangaa, akarudi katika sura ya kawaida, na mwenzake
akacheka kama vile alijua mwenzake amegeuka sura na mimi nimeogopa.
Ndipo
nilipoanza kukumbuka ujaji wao kama ulifanana na mazingira ya kuwa waumini
wangu.
Nikakumbuka
kuwa, wakati wanaingia, walipitia njia zote za uumini, na pia walionekana ni
wanyenyekevu kupita hata waumini wangu wa kila siku.
Wakati
nikiwaza hayo, ghafla mmoja wa wale wazee alisimama mbele yangu bila kumwona
akitoka kwenye fomu kuja mbele, nikashituka, lakini kumbe waumini wengine
waliniona nilivyoshituka, wakakaza macho kiwangu wakishangaa.
Nilikatisha
maneno ya ibada na kuinua mikono juu kisha nikafanya ishara ya msalaba, kwa
jina la baba, la mwana na la roho…
Akapotea
mbele ya macho yangu na kuonekana amekaa na mwezake kama mwanzoni, wakacheka
sana lakini si kwa kutoa sauti.
“Nilishtuka
sana , nikafikicha macho kuyaweka sawasawa kwani yalionekana kama yana ukungu
wa moshi.
Yalipokaa
sawasawa, nikaendelea na ibada lakini mwili wangu ukiwa umechoka sana, hauna
nguvu tena mwilini kama kuna vitu vunatembeatembea.
Baadhi
ya waumini walipata picha hiyo, kwamba sikuwa sawasawa, lakini walikuwa hawajui
kama nilikuwa naona watu wa ajabu.
Nilipofika
eneo la kuongea maneno ambayo ikawalazimu waumini wasimame, wale wazee wawili
wakawa wa kwanza kusimama kabla sijamaliza maneno na wakawa warefu kuliko
waumini wangine.
Kurefuka
kwao kama kuliambatana na moshi mkubwa wa moto wa kuni.
Nilipowaangalia
waumini wengine walionekana hakuna wanalolijua kuhusu maono yangu kwani
walisimama, wakafunga mikono kwa unyenyekevu mkubwa wakinisikiliza.
Kama
wangekuwa wamegundua kitu, basi hata wale waumini waliokaa jirani wangejua,
kwani wao walikuwa wakinitazama tu wakati jirani yao kuna mambo ya ajabu!
Nilikata
maneno ya ibada na kuwaamuru waumini wakae, wakatii lakini mshangao:
“Humu
ndani kuna watu wawili naona kama si wa imani yetu,” nilisema.
Waumini
wote wakawa wanageukageuka na kutazamana wakiwatafuta wao watu wawili.
Walichokifanya
wale wazee sasa, muumini aliyekaa katikati yao alipogeuka kumwangalia mmoja
wao, wakaonekana wote wamekaa pamoja na yule muumini akawa amekaa pembeni yao,
kwa hiyo alipogeuka akawa anamwangalia muumini ambaye anamfahamu.
“Naamini
hakuna atakayeweza kuwaona, maana wanatumika sana na ibilisi,” nilisema.
Ninawapa
muda wa wao kujisema ni akina nani?” Nilisema huku nikiwaangalia kwa kuwakazia
macho huku waumini nao wakinikazia macho mimi na kuyafuatilia
ninakoangalia.
Walichokifanya
wale wazee sasa, muumini aliyekaa katikati yao alipogeuka kumwangalia mmoja
wao, wakaonekana wote wamekaa pamoja na yule muumini akawa amekaa pembeni yao ,
kwa hiyo alipogeuka akawa anamwangalia muumini ambaye anamfahamu.
“Naamini
hakuna atakayeweza kuwaona, maana wanatumika sana na ibilisi,” nilisema.
Ninawapa
muda wa wao kujisema ni akina nani?” Nilisema huku nikiwaangalia kwa kuwakazia
macho huku waumini nao wakinikazia macho mimi na kuyafuatilia
ninakoangalia.
Mara
walipotea machoni pangu. Niliwaambia waumini kuwa, wametoweka na nikaonesha
mahali walipokuwa wamekaa.
Yule
mzee aliyewekwa kati akasema, anachojua yeye ni kwamba, waumini waliokwenda
kukaa kulia na kushoto kwake ni wanawake na alitaka kuwauliza kisa cha kukaa
upande ule wa wanaume.
Basi,
niliendelea na ibada huku kila muumini akionekana hana amani moyoni. Hata pale
alipoingia mtu na kuliza mlio wa viatu sakafuni, waumini wote waligeuka
kuangalia mpaka ikabidi mimi nisitishe kuendelea na ibada ili waumini wamalize
kuangalia.
Ibada
ilipokwisha, niliingia kwenye chumba nikavua mavazi ya utumishi, nikabaki na
mavazi yangu ya kawaida. Nikiwa natoka nje ya chumba, ghafla nikaona giza nene
mbele.
Nikawahi
kushika flemu ya mlango huku nikiwa nahakikisha sianguki au kukanyaga sehemu
ambayo siyo ardhi. Mpaka hapo nilikuwa siunganishi tatizo la kuona giza na
uwepo wa wale waumini wawili wa ajabu ajabu.
“Mtumishi
wa Mungu kwema?” Nilisikia sauti ikiniuliza.
“Siyo
kwema kabisa.”
“Unaona
nini mbele?”
“Naona
giza .”
“Fumba
macho.”
Nilifumba.
“Haya
fumbua sasa.”
Nilifumbua.
Nikaendelea
kuona kama kawaida, lakini hakukuwepo na mtu yeyote aliyesimama mbele, nyuma,
kulia wala kushoto kwangu.
Lakini
pamoja na hali hiyo, niliisaka ile sauti akilini mwangu na kuigundua kuwa,
ilikuwa ya yule mzee aliyekaa jirani na wale watu wa ajabu.
“Khaa!”
Nilijikuta nikishangaa sasa.
Nilitembea
kwa mwendo wa haraka hadi kwa waumini waliokuwa wamesimama nje ya kanisa
wakiongea, wengine wakisalimiana na kuulizana maisha, kwani waumini wengi
huitumia Jumapili kuonana na kuongea mambo yao mbalimbali ya maisha.
Nilizungusha
macho kumwangalia yule mzee, nikamwona katikati ya watu akicheka na kupiga soga
na wazee wenzake, nikamfuata, lakini huku waumini ninaowapita wakinisalimia,
wengine wakionekana kutaka kujua kile kisa cha ndani ya kanisa.
Wakati
nakaribia kumfikia, nilijiuliza mwenyew, je, kweli kwa sauti ile kama angekuwa
ni yeye angeshafika katikati ya watu?
“
Kama ni hivyo, mbona sasa wakati nafumbua macho sikumwona mbele yangu?”
“Faza
pole na majukumu bwana,” yule mzee niliyekuwa namfuata alinisalimia na kuwawahi
wenzake wote aliyosimama nao. Sauti yake niliikumbuka vizuri sana, ndiyo ile
iliyonielekeza mpaka nikafumbua macho.
“Nimeshapoa
mzee wangu.”
Wazee
wengine nao pia wakanisalimia huku wakinipa mikono.
“Eti
mzee ulikuwa unasemaje?” Nilimuuliza yule mzee.
“Wapi?”
Na yeye aliniuliza.
“Hukusimama
na mimi pale mlangoni?”
“Mlangoni!
Wapi?”
“Kule
kwenye chumba?”
“Hata,
hapana.”
Wazee
wengine nao wakaonesha kunishangaa mimi, nikajisikia soni kwa nafasi yangu ya
u-Padri.
“Oke,
sawa basi.”
Nilitembea
kwenda kwenye ofisi yangu, lakini nyuma nikamsikia mzee mmoja akisema.
“Kwani
mzee Makwaya imekuwaje?”
“Sijui
chochote,” mzee Makwaya alijibu, hali ya mshangao na minong’ono ya chini kwa
chini iliendelea hadi ilipofika mahali nikawa siwasikii.
Kule
ofisini nilikuwa peke yangu, nikainamia mezani na kuwaza ile hali mwanzo hadi
pale ilipofikia nikaona giza nene mbele yangu.
“Hivi,
wale ni akina nani?”
“Ni
kwanini walinijia kanisani?”
“Wametumwa
au?”
Nikiwa
naendelea kuwaza hivyo, mara nikasikia sauti ndani ya ofisi.
“Unaendeleaje
mtumishi wa Mungu?”
Ilikuwa
ni sauti ya yule yule mzee Makwaya.
Nilishtuka
sana , nikaangalia kila kona ya ofisi.
“Hakuwepo
popote pale jambo lililonifanya nizidi kuogopa.
Nikiwa
natafakari huku kijasho chembamba kikinichuruzika, mara nikasikia kishindo
kikuu kwa nje kama vile kuna kitu kizito kinatua toka juu kwenda ardhini.
“Wewe
ni nani?” Niliuliza lakini sauti yangu ikitoka kwa woga.
Sikusikia
jibu wala sauti yoyote, ulipita ukimya, nikaendelea kutafakari huku kama
nashikwa na usingizi mzito na macho yangu hayaoni.
Ghafla
nilihisi kiumbe kusimama mbele yangu, nikajitahidi kufumbua macho.
Niliona
binadamu mwenye mguu mmoja, sikio moja, mkono mmoja, tundu moja la pua, jicho
moja amesimama mbele yangu akiachia tabasamu la kutisha.
“Kwa
jina la baba na la mwana na la…”
Kabla
sijamaliza kusema, alipotea mbele yangu, lakini bado macho yangu yakawa yana
kivuli chake kwani alikuwa wa kutisha sana sijapata kuona mfanowe.
Nilitamani
waumini wangu, hata mmoja tu aje, lakini ajabu ni kwamba hakukuwa na dalili na
si haikuwa kawaida yao, kwani mara zote, kila baada ya ibada waumini walikuja
ofisini kwangu na kueleza matatizo yao.
Ilifika
mahali nikahisi labda siko mahali salama, labda mimi niliona nipo ofisini
lakini kumbe sikuwa ofisini, ingawa nilipojaribu kutupa macho huku na kule,
akili yangu iliamini niko ofisini kwangu.
“Ngo
ngo ngo.”
Mlango
uligongwa.
“Karibu,
ingia,” niliitikia haraka.
Waliingia
wanawake wawili, wakiwa wamejitanda vitenge hadi kichwani na kubakiza uso tu.
Walikuwa wageni machoni pangu, nikiwa na maana sijawahi kuwaona hata siku moja
katika maisha yangu ya utumishi.
“Karibuni
sana akina mama.”
Hakuna
aliyejibu hata kwa kutingisha kichwa.
Waliangalia
wenyewe sehemu ya kuketi, wakaketi na kunikazia macho mimi.
Na
mimi niliwaangalia kwa uso wa kuwauliza shida yao . Lakini hakuna aliyesema
mpaka mimi nilipotoa sauti yangu.
“Niwasaidieni
nini akina mama zangu?”
Ajabu
iliyotokea hapo sijapata kuona wala kuisikia siku yoyote ile.
“Tuna
shida na wewe Padri,” alisema mmoja, lakini kwa sauti nene na nzito, ya
kiume.
Kwanza
nilishtuka sana kusikia sauti ya kiume ikitoka kwenye mwili ule mwembamba.
“Shida
gani mama zanguni?” Niliwauliza kwa sauti yenye woga woga kwani sasa nilianza
kuyaona maisha yangu kama yanajaribiwa.
“Tunataka
kuwa na wewe kazini kwetu,” alisema yule wa pili ambaye naye sauti yake ilikuwa
nene zaidi kupita ya wa kwanza hadi nikajikuta nikitetemeka.
“Mna…mnanitaka
kwe…kwenye kazi gani?” Niliuliza huku sauti yangu ikitetemeka kwa wasiwasi
mkubwa moyoni, jasho jembamba lilizidi kuchuruzika licha ya kwamba nilipoingia
niliwasha pangaboi.
“Ina
maana hutujui?” Wote walisema kwa wakati mmoja huku wakisimama na kujivua
vitenge. Nilishangaa sana kuwaona wamebaki na suruali na mashati, ina
maana kumbe ni wanaume kama mimi na walivaa vile kike ili kinipoteza
mawazo ya awali, niliwaza kwa wasiwasi huku nikiwakodolea macho pima.
“Mtumishi
wa Mungu aliye hai, tunakutaka kwenye kazi yetu bwana, eee?”
Mmoja
wao alisema akinisogelea nilipokuwa nimekaa mimi. Sasa niliibaini sauti yake,
ndiyo ile ya yule mzee muumini wangu.
“Nyinyi
si mliingia kanisani kwangu loe mkawa mnafanya maajabu?”
“Eee,
ni sisi,” walinijibu huku yule wa pili naye akisimama, akanisogelea na kusimama
sambamba na mwenzake.
“Sasa
mnataka nikafanye kazi gani na nyinyi, ya maajabu kama nyinyi?”
“Eee,
ndiyo,” walijibu wote.
“Mnatoka
wapi?”
Mmoja
wao akajibu:
“Tunatoka
kwa Mungu.”
“Yupi?”
Niliwauliza huku nikiwa nataka kusema ‘kwa jina la baba na la mwana…lakini
wakaniwahi wao kwa kusema:
“Mungu
kama wako, ametutuma kwako, amesema unatakiwa kupata nguvu ambayo na sisi
tunayo, kwa hiyo na sisi tunakupa nguvu hii, POKEA!”
Waliposema
‘pokea’ walinigusa kwa pamoja kwenye paji la uso, nikaanguka chini na kupoteza
fahamu.
Nilipokuja
kuzinduka, nilikuwa katikati ya pori lenye miti minene, mirefu na matawi yakiwa
juu sana .
Nililala
kwenye nyasi, pembeni yangu nilizungukwa na watu wengi ambao niliwaona miguu
tu. Kwa haraka haraka nilihesabu miguu ile na kupata idadi ya ishirini na sita,
ina maana watu waliosimama walikuwa kumi na watatu.
Niliinuka
ili kukaa, lakini mmoja wa wale watu alinizuia nisikae, niendelee kulala,
nikatii kwa vitendo na kurudi kujilaza majanini.
Ghafla
nikasikia sauti nzito, yenye tetemeko.
“Umetakiwa
kupokea nguvu ya kwetu,” ilisema ile sauti.
Yakapigwa
makofi pale, halafu ukafuatia ukimya wa muda mrefu kama vile nililala peke
yangu bila kuwepo mtu mwingine.
“Simama,”
ile sauti ilisema kwa haraka na kwa amri.
Nilijikuta
nasimama lakini nikiwa ndani ya ofisi yangu. Nilijiangalia na kujiona niko kama
nilivyovaa awali, kila kitu ndani ya ofisi kilikuwa sawasawa, hakuna hata kitu
kimoja kilichoharibika au kutokuwepo.
Hofu
ikaniingia kuhusu waumini wangu nje, kwamba kama walikuja wakakuta mazingira yenye
utata wataelewaje?
Niliusogelea
mlango na kushika kitasa, nikaufungua polepole na kuangalia nje. Hakukuwa na
muumini hata mmoja, hata mtoto.
“Khaaa!”
Nilishangaa.
“Ina
maana nimetumia muda mwingi sana ?” Nilijiuliza.
Niliangalia
saa ya ukutani na kugundua kuwa, wakati namaliza ibada ilikuwa saa nne na nusu,
muda ule naangalia saa ilikuwa saa saba mchana, ina maana kuingia kwa wale
watu, kupoteza fahamu hadi kuzinduka ilipita saa tatu?!
Mlango
uligongwa, akaingia mtu mmoja, simfahamu. Nilimkaribisha, akakaa kwenye fomu.
“Nikusaidie?”
“Ee
baba, mimi nimekuja uniombee,” alisema akijiweka sawasawa.
“Nikuombee
nini?”
“Uniombee
naumwa.”
“Unaumwa
nini?”
“Huwa
nikilala usiku naona watu wanakuja kunikaba.”
“Unaona
au unaota?”
“Naona,
wakati mwingine huwa napiga kelele kwa kuwaogopa.”
“Wewe
ni muumini wangu?”
“Hapana,
nasali mjini.”
“Sasa
kwanini usiende kwa mtumishi wa Mungu wa kanisa lako?”
“Ameshaniombea
sana lakini hakuna mafanikio.”
“Sasa
unaamini nini kuja kwangu, kuna mafanikio?”
“Naamini
yapo mtumishi.”
Nilihisi
ni miongoni mwa wale watu walionijia na kunifanyia maajabu yao, lakini sijui ni
nini, kwani ghafla nilijawa na ujasiri wa kutoogopa lolote na kuamua kumwombea
kweli.
Nilisimama,
nikamtaka yeye apige magoti kisha nikamwekea mkono wangu wa kulia kichwani
kwake na kuomba sana mpaka akaanguka chini.
Alipokuja
kusimama, akasema anajisikia mwepesi, ana imani amepona kabisa.
“Usijali,
nenda kwa amani lakini jilinde na dhambi.”
“Sawa
Padri.”
Alipoondoka
tu, mzee mmoja, aliyevaa shuka jeusi kuzunguka kiuno, chini akiwa hana kiatu
wala sendoz, pekupeku, ju mabega wazi, mkononi alishika mkia wa mnyama,
alisimama mbele yangu bila kujua aliingiaje?
“Karibu
mzee wangu,” nilimkaribisha kwa ujasiri mkubwa sana, moyoni sikuwa na hofu wala
wasiwasi. Pamoja na kuvaa kiajabu kama vile, lakini nilimwona kama mtu wa
kawaida sana kwangu.
“Fumba
kiganja cha mkononi,” aliniambia kwa amri.
Nikajikuta
nafumba bila kuhoji yeye ni nani na ametoka wapi na kaja kwangu kufanya nini.
“Fumbua.”
Nilipofumbua,
unga mweusi ulikijaza kiganja changu.
“Jipake
kidogo usoni.”
Nilijipaka
kidogo huku nikiwa nimeinama kuangalia chini.
“Unaona
nini?”
“Sioni
kitu.”
“Haya,
hiyo dawa ndiyo tunayotumia kufanyia kazi, tunapotoka usiku kwenda kazini kila
mmoja anakuwa na dawa hiyo, ndiyo inayosaidia watu wasituone…
“Fumba
kiganja.”
Nikafumba.
“Fumbua.”
Nilipofumbua,
sikuona ile dawa, kiganja kilikuwa cheupe kama mwanzo.
“Fumba
tena kiganja.”
Nikafumba…
“Fumbua.”
Nilipofumbua
mkononi, nusu kulikuwa na unga unga wa kijani nusu unga unga mweusi.
“Chota
huo unga kisha changanya.”
Nilitii,
kisha akaniambia nijipake kidogo usoni, nikafanya hivyo na kujikuta nakuwa
mwepesi kuliko kawaida ya siku zote.
“Unaona
nini?”
“Najiona
mwepesi sana .”
“Unaweza
kujaribu kupaa?”
“Nijaribu?”
“Jaribu
basi.”
Niliinua
mikono kama vile ndege anavyoinua mabawa, taratibu nilijiona napaa juu huku
miguu ikiiacha ardhi taratibu bila ridhaa yangu.
“Unaonaje?”
“Napaa
sasa.”
“Shusha
mikono.”
Niliishusha,
taratibu miguu ikakanyaga ardhi na kusimama kama mwanzo.
Baada
ya hapo yule mtu akapotea machoni pangu na kuniacha nikiwa na maswali kibao.
Nilijiweka
sawa, nikafunga madirisha ili kutoka, nikafunga mlango na kuondoka kabisa
katika eneo la ofisi.
Nilikwenda
kwenye makazi yangu, lakini kwa wakati huo nilijihisi mnyonge sana, mwili
ulikuwa hauna nguvu, macho hayaoni vizuri mbele na miguu mizito.
*
* *
Saa
saba za usiku, nilishtuka kutoka usingizini baada ya kushikwa na kuvutwa kidole
cha mguu wa kulia na mtu. Kulikuwa na giza kwa hiyo sikujua nani alifanya zoezi
lile.
Swichi
ya kuwashia taa haikuwa mbali na nilipolala, nikaiwasha chapchap, chumba
kilipojaa mwanga sikuona kitu, nikaendelea kulala.
Baada
ya muda nikawa katika ndoto.
“Wewe
Padri, unadhani utafanya kazi mpaka lini?”
“Mungu
apende,” nilijibu.
“Je,
asipopenda?”
“Atapenda
tu.”
“Kwanini
unafanya kazi lakini huna nguvu.”
“Nguvu
gani?”
“Ya
kiroho.”
“Kwa
sababu bado.”
“Bado
nini?”
“Wakati
wa kuwa na nguvu.”
“Ni
sasa.”
“Kwa
maana ipi?”
“Njoo.”
Nilimfuata
huyo mtu, akanishika na kunivuta hadi mahali, akasimama na kuniambia.
“Nenda
kaingie kwenye kanisa lile.”
Mbele
yangu kulikuwa na kanisa, nikaenda kuingia.
Lilikuwa
kanisa langu, waumini wangu, wake kwa waume wengine wamekaa wengine wamesimama.
Walikuwa wengi sana.
Mimi
nikapita hadi mbele kwenye madhabahu na kusimama pale.
“Wale
wenye matatizo waje niwaombee.”
Karibu
kanisa zima walipita mbele kuombewa.
Ule
wingi wao, nikaanza kuogopa kwamba nitaweza kweli?
Wa
kwanza nikamwekea mikono juu kichwani na kumwombea, pale pale aliposimama
akaanza kupiga kelele na kuanguka chini kisha akasimama akiwa amepona na
kurukaruka huku akimtukuza Mungu wake.
“Hee,
hee nimekuwa mzima sasa.”
“Nenda
usitende dhambi tena, sawa?”
“Sawa.”
Niliombea
karibu kanisa zima, nilipomaliza nikawa natoka huku napigiwa makofi na waumini
waliokuwa wamesimama kulia na kushoto kwangu.
“Padiri
Padiri Padiri,” walisema wakipiga makofi, pwa pwa pwa.
Kufika
nje, nikakutana na yule mtu aliyenichukua nyumbani.
“Umefanikiwa?”
“
Sana ,” nilimjibu.
“Umekubali?”
“Nini?”
“Kwamba
wakati wa kuwa na nguvu ya kiroho ni sasa?”
“Nimekubali.”
“Haya,
sasa twende kwa aliyekupa nguvu.”
“Kwa
Mungu?”
“Wetu
sisi.”
Tuliongozana
hadi kwenye mti mmoja mkubwa, mrefu sana kwenda juu.
Chini
walikaa watu wengi wakiwa kama wapo kwenye maongezi.
Kilichonishangaza
miongoni mwa hao watu walikuwepo waumini wangu wa kanisani.
“Afadhali
umekuja faza.”
“Faza
nimefurahi sana kukuona.”
“Faza
karibu sana .”
Wale
waumini wangu wote walinikaribisha kwa furaha, amani na upendo wa hali ya juu.
Nilikaa
sehemu ambayo kulikuwa na nafasi ya mtu mmoja, yule mtu niliyekwenda naye
sikumwona tena alikopotelea.
“Bwaba
umekuja huku, uko tayari kwa lolote?” Aliniuliza mzee wa kanisani ambaye sikuwa
na mazoea naye.
“Kwani
hapa ni wapi?” Nilihoji.
“Hapa
ni kwa wachawi.”
“Wachawi!”
“Eee,
umekuja kwa wachawi, kazini kwetu, karibu.”
Alipomaliza
kusema, alikaa chini, akasimama sasa yule mzee ambaye siku ile kanisani
walipoingia wale watu wawili wa ajabu, yeye alikaa katikati yao.
“Eee,
nina kila sababu ya kujisifu kwa kupewa heshima hii ya kumkuza kazini mtu
mkubwa kama huyu,” alisema yule mzee.
Yakapigwa
makofi kwa muda wa dakika tano nzima huku yule mzee akiwa amesimama tu
akisubiri yaishe ili aendelee kuongea.
Lakini
kwa jinsi nilivyokuwa namwangalia mimi, alikuwa anaongea kwa kujiamini sana na
hakuonekana kujali kama mimi ni kiongozi wake wa kiroho.
“Kwa
hiyo kuanzia leo mtumishi utakuwa chini yangu ukizitii na kuzifuata amri zangu,
sawa bwana mdogo?”
Nilimjibu
kwa sauti ya unyonge sana :
“Sawa.”
Pale
pale alitembea kuelekea nilikokuwa mimi, akaniwekea mkono kichwani.
***
Wiki
moja ilikatika toka hayo yatokee, lakini hakukuwa na jipya jingine, sikuwahi
kumwona mtu mwingine akinijia nyumbani wala kanisani ninapokuwa nafanya kazi za
Mungu.
Lakini
siku hiyo, nikiwa nimelala majira ya saa saba usiku, nilishtuka ghafla.
Nikatupa macho mlangoni. Kwa sababu ya giza sikuona vizuri, ila dalili ya kama
kitasa cha mlango kikifunguliwa.
Nilinyoosha
mkono hadi kwenye taa ya kitandani (bed switch) nikawasha kwa umakini sana ili
mlio wa swichi usisikike.
Kitasa
kikawa kinakaribia chini, lakini kikanata kwa muda. Nadhaani ni baada ya mimi
kuwasha taa.
Hali
hiyo ilinifanya nitoke kitandani na kusimama katikati ya chumba huku macho yote
yakiwa kwenye kile kitasa mlangoni.
Huku
taa ikiwa bado inawaka, kitasa kiliendelea kwenda chini, yaani kufunguka,
lakini ilionekana aliyekuwa anakifungua yupo makini sana kwani kwa kukitazama
haraka tu ilikuwa vigumu kujua kitasa kinafunguka kwa kwenda chini.
Mara
mlango ukaanza kusukumwa polepole na mimi nilisimama nikaza macho kujua
nani aliyekuwa akifanya kazi ile. Wazo kwamba ni mwizi sikuwa nalo kwani
nawajua wezi, wao ni papara au kushtukiza.
Mlango
uliendelea kusukumwa mpaka ukawa wazi wote, yaani kama kuna mtu alisimama
kwenye korido angeona chumbani, lakini cha kushangaza hakukuwa na binadamu wala
kiumbe chochote nyuma ya mlango.
Nilipotaka
kuuliza nani mwenzangu, nikasikia sauti ya mtu kukohoa kwa kujibana. Halafu
nikasikia mlio wa viatu, ko! Ko! Ko! Ko! Ukisikika kuingia ndani ya chumba,
nikarukia kusimama pembeni kwani niliamini aliyekuwa akiingia angeweza
kunikumba.
Mlio
wa viatu kutembea uliposimama ukafuata mlio wa kufunguliwa kwa dirisha la chumba,
na kweli likawa linafunguka hadi mwisho, halafu pazia ikawa inakunjwa na
kufungwa katikati kama vile mkunjaji alitaka upepo uingie kwa vizuri.
Baada
ya hapo, nikiwa nimesimama pembeni, mlio wa viatu ukatembea kwa mwendo ule ule
wa ko! Ko! Ko hadi ukutani kwenye swichi, ghafla nikasikia tap na giza
likatanda. Ina maana huyo mtu alizima taa.
Halafu
mlio wa viatu ukaendelea tena hadi usawa wa kitanda, ukakwamba pale. Giza
likiwa limetanda, nikasikia hali ya mtu anayepanda kitandani kwani kitanda
kilitoa mlio Fulani na baadaye, kama baada ya dakika moja ikasikika sauti ya
mtu kukoroma.
“Khooooo!
Khoooo!”
Niliamini
ni uonevu usiokuwa na maana kwangu kwani sikuwa na kosa la kunifanya nishindwe
kulala na kulala mtu mwingine, nilikasirika sana . Nikatembea kijeuri
hadi ukutani na kuwasha taa.
Ile
inawaka tu, ile swichi ya kitandani ikasikika ikizimika, tap! Kukawa giza tena.
Niliifuata
kwa fujo ile swichi ya kitandani, nikaiwasha na macho yangu yakakimbilia moja
kwa moja kitandani. Mtu mnene, mrefu alikuwa amejifunika shuka huku akiwa
amenyoosha miguu na anaangalia juu, yaani amelala chali.
“Wewe
ni nani?” Nilimuuliza bila woga.
“Msafiri,”
sauti nzito ilijibu kwa mkato.
“Ndiyo
jina lako au msafiri unakwenda mahali?”
“Siendi
popote.”
“Khaa!
Sasa hapa kwako?”
“Hapana.”
“Sasa
kwanini umefungua mlango bila hodi na umepanda kitandani kulala bila ridhaa
yangu?”
“Nisamehe
sana .”
“Basi
ondoka.”
Kauli
yangu hiyo haikupata jibu zaidi ya mlio wa kukoroma kusikika kama mwanzo.
Nilimsogelea
yule mtu pale kitandani kwa lengo la kumfunua shuka na kumwona vizuri.
Niliishika shuka kwenye ncha moja, nikaifunua kwa
nguvu…
“Ha
ha ha ha ha ha!” Alicheka sana yule mtu huku akitoka kitandani na kuficha uso
kwa mkono mmoja.
Nilijitahidi
sana kuhakikisha namwona uso yule mtu, lakini na yeye alikuwa akawa anaangalia
ukutani huku akiendeelea na kicheko chake.
“Wewe
ni nani?” Nilimuuliza kwa ukali kidogo.
“Ha
ha ha ha! Msafiri bwana, si nilikwambia!”
“Umetumwa?”
“Hapana.”
“Umekuja
tu mwenyewe?”
“Ha
ha ha ha! Eee!”
Kusema
ule ukweli nilichanganyikiwa, kwani sasa nikawa sijui ukweli upo wapi, kila
ninachomuuliza ananijibu kinyume na matarajio yangu.
“Basi
mimi naomba uondoke humu chumbani kwangu,” nilimwamuru.
“Ha
ha ha ha ha! Sawa,” alisema akielekea mlangoni na kutoka kweli lakini nikiwa
sijafanikiwa kuona sura.
Kwa hiyo mpaka hapo nikawa sijui ni nani yule.
Alipovuka
tu ukuta wa chumba changu, nikajikuta napata wasiwasi na woga tofauti na mwanzo
alipoingia.
Nilifunga
mlango ili nipande kitandani kulala, lakini kabla sijapanda, nikasikia vishindo
ti ti titi! Watu kama sita walisimama katikati ya chumba changu.
“Mtumishi
wa Mungu vipi? Habari za kulala?”
“Salama.”
“Aaa,
tumetumwa kwako.”
“Na
nani?”
“Aaa,
vaa miwani yako kwanza kisha utuangalie vizuri.”
Nilipeleka
mkono kwenye stuli ndogo iliyokuwa pembeni ya kitanda na kuchukua miwani,
nikaivaa na kuwaangalia.
Walikuwa
tofauti na nilivyowaona wakati wanatua. Walikuwa wamevaa viguo vyeusi (kaniki)
kukatisha kiunoni kwenda chini ya mapaja, kila mmoja alionekana amekasirika na
hana utani na usoni walipaka vitu vyeupe, kama si unga, basi chokaa.
“Unatuona
vizuri sasa?”
“Ndiyo.”
“Basi
ndivyo tulivyo, toa miwani.”
Nilipotoa
tu, walirejea na kuwa kama walivyotua, wamevaa kawaida.
“Unatakiwa
kuhudhuria mateso ya waumini wako usiku wa sasa,” mmoja wao aliniambia, wengine
wakatingisha vichwa kama ishara ya kukubaliana na maneno ya mwenzao.
“Wapi?”
“Katika
kila nyumba yenye muumini au waumini wako.”
“Ni
mateso ya aina gani?”
“Utajua
huko huko na huna hiyari katika hili, kwani ulishapata baraka zote za uchawi.”
Nilijikuta
nasimama, naanza kutembea kuwafuata kutoka nje mpaka uwanjani mbele ya nyumba,
wakaanza kutengeneza duara na mimi nikawa mmoja wa wanaduara.
Mmoja
akapeleka mikono na kuwashika wa kulia na kushoto kwake, wengine wakafanya
hivyo mpaka mimi. Tukawa tumekamatana mikono. Yule aliyeanza kushika, akainama
kama dalili ya kusujudia, wengine wakafuatia na mimi pia, kufumba na kufumbua,
tukajikuta tukipaa juu na kutua chini ya mti mkubwa wa Mvule. Sikumbuki
tulitumia dakika ngapi kuwa angani na kushuka.
Milio
ya ngoma iliyotawala pale ilinifanya niamini kuwa, kweli nilikuwa katikati ya
maskani ya kichawi.
“Bila
kupoteza muda sasa tunaingia mitaani, hasa kwenye nyumba za waumini wa kanisa
ambalo padri wao tunaye kwenye kundi letu na kufanya kazi ya kuwatesa, sawa?”
Sauti nzito, iliyokuwa ikisikika na kitetemeshi ilisema.
Nilipomwangalia
msemaji huyo, ni mzee mmoja aliyekuwa amevaa kanzu ndefu nyeusi, juu, yaani
kichwani alivaa pembe za mnyama, mkononi alishika mkia, pia wa mnyama.
“Sawa,”
wenzangu waliitikia kwa sauti ya juu.
Kifupi
mimi nilikuwa sijui kitu chochote. Nilikuwa sijui watafanyaje huko kwenye
kutesa watu, sijui nani atakayeteswa, kama ni waumini wote pia sikujua. Ila,
mzee mmoja alinifuata na kuniambia:
“Tuondoke
mimi na wewe.”
Nikawa
namfuata hadi kando kando ya ule mti mkubwa, akasimama ghafla hadi nikamkumba.
Kufumba
na kufumbua, tulitua nje ya nyumba ya muumini wangu mmoja ambaye anamiliki
mashine ya kusaga na trekta moja.
“Haa!
Hapa si kwa..?”
Kabla
sijamaliza kusema, yule mzee akaniambia kwa kunikatisha:
“Ulisikia
tulivyoambiwa kule?”
“Kwamba?”
“Tunawatesa
akina nani?”
“Waumini
wangu.”
“Sasa
unauliza nini?” Alinijibu huku akitembea kwa kurukaruka kwa mguu mmoja.
Alipoona
mimi nimezubaa akanifuata:
“Jipige
kifuani kwa mkono.”
Nikafanye
hivyo.
“Hapo
sawa sasa, nifuate mimi kwa kila hatua mpaka ndani na kuanza kazi, sawa?”
Aliniuliza.
Inaendelea!!!!!!!!!!!!!!!! Usikae mbali na Irene Mwamfupe Ndauka pande hizi.
No comments:
Post a Comment