JESHI la Polisi wilayani Bunda linamshikilia Elifinya Batholomeo
(28), mkazi wa jiji la Dar es Salaam kwa tuhuma za kumgonga mwanafunzi
wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kabalimu, Maria Peter (7), na
kusababisha kifo.
Tukio hilo limetokea juzi saa 10:00 jioni katika eneo la mtaa wa
Posta, barabara ya Musoma –Mwanza, ambapo mwanafunzi huyo alikuwa
akitembea kando ya barabara.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo gari hilo lilikuwa katika mwendo
kasi wakati likipishana na gari jingine ndipo lilipomgonga mwanafunzi
huyo ambaye alikufa papo hapo.
Walisema kuwa dereva huyo ambaye alikuwa akiendesha gari aina ya
Pajero lenye na T 651
BMZ mali ya kampuni ya Geodata, baada ya kubaini
kuwa ameua, hakusimama kutokana na kuhofia maisha yake.
Aidha mashuhuda hao walilazimika kutoa taarifa polisi ambao walifika
na kuchukuwa mwili wa mwanafunzi huyo ambao umehifadhiwa katika
hospitali ya wilaya.
Walisema kuwa baadaye polisi walilifuatilia gari hilo ambalo lilipitia
njia za mkato na kufanikiwa kulikamata katika kijiji cha Nyamatoke.
Akizungumzia tukio hilo mama wa mwanafunzi huyo aliyejitambulisha kwa
jina la Ghati Wambaura alisema kuwa mtoto wake aliondoka siku hiyo
asubuhi kwenda kanisani lakini majirani walimpa taarifa juu ya kugongwa
na gari.
“Mtoto wangu huwa anashinda kanisani na wenzake lakini ilipofika jioni
niliambiwa na watu kuwa kuna mtoto amegongwa na nilipoenda polisi na
kujulishwa kuwa mwili upo hospitali ndipo nilipobaini kuwa ni mtoto
wangu,” alisema.
Polisi walisema kuwa wanatarajia kumfikisha mahakamani dereva huyo ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
No comments:
Post a Comment