SIKU moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume
maalumu ya kuchunguza matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi
karibuni, wanasiasa na wasomi wamempinga wakidai ni kupoteza muda na
fedha kwa kuwa hoja binafsi ya Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
ilikuwa na majibu.
Kwa nyakati tofauti katika mahojiano na gazeti hili, Katibu Mkuu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, na
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana
walihoji ni tume na kamati ngapi zimeundwa na kutolewa taarifa kuhusu
matatizo ya elimu katika miaka 15 iliyopita na hatua zipi zimechukuliwa
kurekebisha dosari zilizoonekana.
Dk. Slaa alishangazwa na hatua hiyo ya Waziri Mkuu kuunda tume kwa
ajili ya kufuatilia kufeli kwa wanafunzi, akisema ni juzi tu Bunge
limemaliza kikao chake Dodoma na kuitupilia mbali hoja binafsi ya
Mbatia.
Alisema hoja binafsi ya Mbatia ilikuwa na nia ya kupitisha azimio la
Bunge kuunda kamati teule ya kuchunguza tatizo la udhaifu katika sekta
ya elimu, lakini kwa ushabiki wa wabunge wa CCM akiwemo Waziri Mkuu,
ilikataliwa.
“Wiki mbili hazijapita wameumbuliwa na matokeo, na sasa Waziri Mkuu
anaunda tume. Huku ni kuwadanganya Watanzania. Pinda ni kiongozi wa
shughuli za serikali bungeni na kiranja wa mawaziri wote, Waziri wa
Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa alilidanganya Bunge na taifa kuhusiana na
swala la mitaala, ambalo lina uhusiano mkubwa na ubora wa elimu.
“Waziri Mkuu alikuwepo, hakuchukua hatua wala ya kumsahihisha
Kawambwa au kusema ukweli na kuchukua hatua kwa waziri huyo kwa jambo
lililotokea mbele ya macho na masikio yake,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa hilo, Pinda hastahili kuchukua hatua ya kuunda
tume, bali kujiuzulu kwa kushindwa kuwajibika na pia kushiriki
kulidanganya taifa.
Dk. Slaa alisema kuwa Serikali ya CCM imeunda tume na kamati nyingi,
lakini taarifa zilizotolewa hazijawahi kufanyiwa kazi, na kwamba kama
hali ndiyo hiyo, hata tume hii inayoundwa hakuna jipya.
“Suala la elimu halihitaji kuundiwa tume wala kamati ya uchunguzi.
Serikali ya Rais Kikwete na Pinda kweli hawajui matatizo yanayofanya
elimu yetu kudorora mpaka waunde tume?” Alihoji Dk. Slaa na kuongeza
kuwa Serikali ya CCM haijui kwamba bajeti ya elimu ni ndogo
ikilinganishwa na zile za majirani zetu katika sekta hiyo.
Dk. Slaa alisema kuwa ni usanii na kuendeleza ufisadi kwani tume
itaendelea kuangamiza fedha kwa vile serikali haijaonesha utashi wa
kisiasa kuboresha elimu ya watoto ya Watanzania.
Alisema kinachotakiwa sasa ni kuunganisha nguvu na kukataa usanii
wowote katika masuala ya msingi. Kwamba wale wote waliodanganya taifa
wawajibike kwa kujiuzulu au wawajibishwe.
Aliongeza kuwa, watoto waliofeli waandaliwe utaratibu wa kunusuru
maisha yao badala ya kuunda tume wakati maisha yao ya baadaye
yakivurugika.
Naye Dk. Bana alimbeza Pinda kwa hatua hiyo ya kuunda tume kwa
masuala ya mtihani, akisema tatizo la kufeli kwa wanafunzi halihitaji
tume kwani kasoro ziko wazi.
Alisema kuwa matatizo ya walimu yanajulikana, huku serikali
ikijidanganya kutengeneza sera ya elimu kinyemela bila kushirikisha
wataalamu.
“Mtihani ni sehemu ndogo sana, lakini siasa za zimamoto ndizo
zimetufikisha hapa. Tujue kuwa siasa za zimamoto hazisaidii Watanzania,
tunapoteza muda na fedha zetu, lakini mfumo wa elimu unapaswa
uangaliwe kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.
“Utaratibu huu wa kuanza kuunda tume kila darasa likifeli zitaundwa
ngapi?” alisema na kuongeza kwamba tatizo la elimu ni la kitaaluma, si
siasa.
Alisema kuwa wanangoja kuona wale watakaoteuliwa kutoka katika chuo
hicho kuingia kwenye tume ya Pinda kama watakuwa tayari kwenda kuungana
na suala hili ambalo halizingatii utaalamu, badala yake linatibu
ugonjwa na kukwepa dalili zake.
No comments:
Post a Comment