VINARA Yanga wanahitaji matokeo mazuri kwenye mchezo wao muhimu
wa leo dhidi ya Azam FC ili kujiimarisha zaidi kileleni mwa msimamo wa
Ligi Kuu Bara.
Yanga inawakaribisha Azam wanaolingana nao kwa pointi kwenye msimamo katika mechi iliyoteka hisia za mashabiki wengi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kila timu ina pointi 36, lakini Yanga ikifaidika kileleni kutokana na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Azam inayokuja kwa kasi.
Endapo Yanga itapiga mwereka kwenye mchezo huo, basi itakuwa imeiruhusu Azam kupanda kileleni kwa mara ya kwanza katika mzunguko wa pili.
Mbali na matokeo mazuri yanayowaniwa na kila timu,
upande wa pili wa mchezo huo ni Azam kuja na jaribio la kulipa kisasi
baada ya mchezo wa kwanza kuogelea na kichapo cha mabao 2-0.
Ni wazi Azam itaingia uwanjani safari hii kwa lengo la kulipa kisasi ingawa Yanga nayo itapigana kuhakikisha inavuna pointi tatu na kuendeleza ubabe wake.
Mashabiki wa soka nao wana hamu ya kujua nani
zaidi kati ya viungo mahiri na chipukizi, Salum ‘Sure Boy’Abubakari wa
Azam na Frank Domayo wa Yanga.
Wachezaji hao siyo tu tegemeo kwenye klabu zao, lakini pia ni tegemeo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa, Taifa Stars. Domayo anayecheza kama kiungo namba nane na Abubakar anayecheza nafasi ya kiungo namba sita, wana sifa zinazoshabihiana wakisifika kwa pasi zenye ‘macho’ na kutopoteza mpira ovyo.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts ataendelea kumwamini mshambuliaji “Jerryson Tegete katika kusaka mabao, wakati Kocha wa Azam, Stewart Hall atamtumia John Bocco kwa shughuli kama hiyo.
“Ubingwa wetu uko mikononi mwa Azam ndiyo maana tumejifua kikamilifu ili kuhakikisha tunawafunga na kuweka pengo kubwa baina yetu,” alisema Tegete akizungumzia mchezo huo.
Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankema amethibitisha kuwa wachezaji Brain Omony na Kipre Balou wapo fiti kuikabili Yanga leo.
Mechi nyingine leo hii ni Prisons iliyopokea
kipigo cha bao 1-0 kutoka Simba katikati ya wiki hii dhidi ya Polisi
Morogoro Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mgambo JKT watapepetana na wenzao wa Ruvu Shooting katika pambano litakalorindima kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
No comments:
Post a Comment